Familia Ya Saanane Yakataa Matanga! Yahesabu Siku Ya Mtoto Wao Kuonekana

saanane-chadema

STORI: GABRIEL NG’OSHA, GAZETI LA UWAZI, TOLEO 1021, JANUARI 3-9, 2017

DAR ES SALAAM: Mwaka Mpya wa 2017 umeanza ambapo ilikuwa ni saa, siku, wiki, mwezi na sasa inakimbilia mwezi wa pili kasoro siku 15 bila kujulikana alipo Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bernard Saanane ‘Ben’ (32) (pichani) tangu atoweke nyumbani kwake, Tabata- Dampo jijini hapa, Novemba 18, mwaka jana, familia yake imekataa kufanya matanga.

MATANGA NI NINI?

Kwa mujibu wa wataalam wa Kiswahili, matanga ni mkusanyiko wa watu kwenye nyumba yenye msiba ili kuomboleza na kuwaliwaza wafiwa kwa siku tatu au zaidi  baada ya kuzika.

Kwa mtu ambaye hakupatikana maiti au mwili wake, lakini familia ikaamini alikufa pia huweza kuweka matanga na waombolezaji wakajitokeza kufariji.

uwazi-1

HABARI ZILIZOFIKA UWAZI KUHUSU MATANGA

Awali, chanzo kimoja kililiambia Uwazi kwamba, kuna tetesi familia ya Ben ambaye amezoeleka kwa jina la ‘Msaidizi wa Mbowe’ imekataa katakata kuweka matanga nyumbani kwa wazazi, Moshi mkoani Kilimanjaro ili kuhitimisha siku kadhaa za kumtafuta mtu aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha.

“Jamani jaribuni kuwasiliana na familia ya Msaidizi wa Mbowe, kuna watu nasikia wanawashauri waweke matanga baada ya siku 40 za kumtafuta ili kumaliza zoezi hilo kisha watu waendelee na kazi zao nyingine za kila siku kwani kuna wanaosema kwamba ni vigumu kumwona tena akiwa hai lakini nasikia familia haitaki kwa vile inaamini kuna siku Ben ataibuka akiwa hai,” kilisema chanzo.

Chanzo kikaendelea kusema kuwa, pia kwa sasa, wazazi na ndugu wengine wa Ben wanasali na kufunga sana, pengine usiku na mchana ili kujua kilichojificha nyuma ya kupotea kwa mwanafamilia huyo.

“Unajua wale ni Wakatoliki, sasa wana sala zao nasikia ambazo mtu akizisali hizo, hata kama kuna gumu la namna gani linakuwa rahisi tu. Au kama kuna jambo lililofichika, linaibuka juu na kujulikana,” kilisema chanzo.

 

UWAZI NA MSEMAJI WA FAMILIA

Baada ya madai hayo, Uwazi lilimtafuta msemaji wa familia hiyo ambaye pia ni mdogo wa kuzaliwa wa Ben, Erasto Saanane ambaye alikataa katakata kwamba, familia yao inataka kuweka matanga.

“Tetesi za kwamba tunaandaa matanga kwa sababu ya kutokupatikana kwa kaka Ben hazina ukweli wowote. Huo ni uongo mkubwa sana, kama familia bado tunaamini Ben ni mzima huko aliko, siku moja Mungu atatuonesha akiwa hai!

“Hatuwezi kuweka matanga wakati tunaamini Ben atapatikana tu. Sasa matanga ya nini? Hata sisi wanafamilia tunashangaa labda ni watu tu wenye roho mbaya wanatangaza kwa manufaa yao.”

FAMILIA YASHINDWA KUSHEREKEHEA MWAKA MPYA

Erasto akaendelea: “Mwaka 2016 ni mwaka ambao hatutausahau katika kumbukumbu za maisha yetu, kwani kupotea kwa ndugu yetu ni kitendawili kizito sana kwa familia. Pia hatujaweza kusherehekea Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya kama miaka mingine kwa ajili ya kuhangaika kumtafuta kaka.”

FAMILIA YASALI NOVENA, YAKANA TAMBIKO

Pia Erasto alikanusha madai kwamba, familia hiyo inataka kufanya tambiko ili kuondoa balaa au kuweza kufanikisha kupatikana kwa Ben.

“Sisi ni Wakristo, hakuna tambiko lolote la kimila ambalo tumelifanya zaidi ya kusali Novena (sala maalumu kwa ajili ya kutatua jambo gumu kwa Wakristo, hasa wa Madhehebu ya Romani Katoliki).”

ANACHOKIJUA KUHUSU POLISI KUMSAKA BEN

“Polisi nao bado wanaendelea na uchunguzi wao, naamini unaendelea vizuri na iko siku watafanikiwa kumpata Ben.”

KUHUSU AFYA YA MAMA YAKE

Kuhusu afya ya mama yao, Renatha Focus Saanane ambaye hivi karibuni aliripotiwa kuugua ghafla ugonjwa wa presha baada ya kusikia kupitia vyombo vya habari taarifa za mwanaye kupotea, Erasto alisema kwa sasa mzazi huyo anaendelea vizuri.

MEYA WA UBUNGO AMZUNGUMZIA BEN

Naye Meya wa Ubungo kwa tiketi ya Chadema, Boniface Jacob akizungumza na Uwazi hivi karibuni kuhusu kupotea kiutata kwa Ben, alisema kuwa, chombo chenye dhamana kubwa ya kumtafuta Ben ni serikali kwa vile ina mkono mrefu.

“Unajua Ben kweli alikuwa ni mwajiriwa na Chadema, alikuwa akifanya kazi za chama. Kupotea kwake hata sisi kunatushangaza sana. Lakini serikali ndiyo yenye dhamana kubwa ya kumtafuta Ben kwa sababu yenyewe ina mkono mrefu wa kuweza kufika popote pale.

“Kwa sasa hivi kutokana na teknolojia ilivyokuwa ni vigumu sana mtu kupotea. Hebu wewe (mwandishi) jaribu tu hapo kumficha mtu nyumbani kwako hata siku mbili tu uone kama hatapatikana.”

TUJIKUMBUSHE

Ben alitoweka Novemba 18, mwaka jana nyumbani kwake Tabata Dampo, ndugu na jamaa zake wamekuwa wakifanya jitihada za kila namna kumtafuta ikiwemo vituo vya polisi, mochwari na hospitali zote kubwa za Jiji la Dar na hata kwenda mkoani Pwani kwenye maiti 7 zilizookotwa mtoni na kuzikwa lakini bila mafanikio.

Jamii imekuwa ikitoa mitazamo tofauti juu ya kupotea kwa Ben ambapo kila mtu anasema sawasawa na anavyoamini, kuona mazingira au kusikia kutoka kwa watu wengine lakini baadhi ya wasomaji wamekuwa wakisema kupotea kwa msaidizi huyo wa Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa chama kikubwa cha siasa nchini kunachukuliwa kama suala dogo wakati ni kitu kizito sana.

“Mbowe kwanza ni mtu mzito sana, unajua Tanzania hakuna chama kikubwa cha siasa cha upinzani kama Chadema. Sasa kwa mtu wao kupotea kama mtu tu wa mtaani, si sawasawa, lazima ijulikane nini kilimpata,” alisema mkazi mmoja wa Kimara, akisema anaitwa Joseph Maragalasa.

Naye Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai nchini, (DCI), Kamishna Robert Boaz amesema taarifa ya kupotea kwa Ben waliipata Desemba 5, mwaka jana.

“Hivi sasa tunaendelea na uchunguzi kubaini alipo kiongozi huyo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo na upelelezi wetu ukikamilika tutatoa taarifa,” alisema Kamishna

halotel-strip-1-1

Videos 5: A-Z Mpambano wa Darassa vs R.O.M.A, Mimi Sisemi Tazama Mwenyewe!


Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment