The House of Favourite Newspapers

Usifanye Biashara Ili Mradi, Lenga Kifanikisha

free-business-plan-templates

UNAPOAMUA kuingia katika biashara ni lazima uwe na malengo ya kibiashara na si kuianzisha na kuiendesha ilimradi. Aidha, unatakiwa ujipime kwa namna inayostahili kuona endapo biashara unayotaka kuianzisha itakuwa na manufaa kwako na kwa unaotaka kuwauzia kama ni huduma au bidhaa zitakazohusika katika biashara hiyo.

Lengo ni kuepuka kupoteza wakati wako na fedha bila sababu za msingi. Mtaalamu wa masuala ya biashara, Bob Phibbs ambaye pia ni mwandishi wa kitabu cha biashara; The Retail Doctor’s Guide to Growing Your Business: A Step by Step Approach To Quick ly Diagnose, ndiye anayeeleza hayo na kusema,

“Ni lazima ujue unataka kuuza vipi uuzacho na kujua kitamfaa vipi mteja wako, si kujiuzia tu ilimradi”.

Kwa mujibu wa Phibbs, ikiwa mfanyabiashara ana nia ya dhati ya kusimama katika biashara yake ili ifikie malengo ya kukua anayoyataka, hana budi kuhakikisha kuwa hata wafanyakazi wake wanaohusika na eneo la mauzo au mapokezi ya wageni wanapatikana kulingana na uzoefu na uelewa mpana wa masuala hayo ya kuuza huduma au bidhaa.

Anasisitiza kuwa, endapo mfanyabiashara ataamua kuchukua tu muuzaji ilimradi amekwenda katika duka au eneo la biashara yake kuomba kazi, atakuwa anajiangusha mwenyewe kwa kuwa mwomba kazi anaweza kuwa hana uzoefu au ujuzi wowote na kazi hiyo ya mauzo, hivyo kuiharibu.

Katika kitabu hicho, Phibbs anasema ni lazima mfanyabiashara ajue nani ataweza kuuza vipi bidhaa au huduma anayoifanyia biashara, vinginevyo kuharibikiwa ni rahisi sana na biashara hiyo inakuwa ni ya ilimradi tu.

Kutokana na hilo, anaeleza kuwa mfanyabiashara husika atakuwa na jukumu la kuhakikisha anapata wasaa wa kufanya mahojiano (usaili) na mtaka kazi hiyo ya mauzo, au kwa kutumia mawasiliano waamini na si kutoa kazi bila kuzingatia vigezo.

Anaeleza pia umuhimu wa kuwa na maswali yenye msingi na maana ya kuisaidia biashara na kusema,

“kwa bahati mbaya wafanyabiashara wengi wanaoanzisha biashara na kutaka wafanyakazi hasa katika eneo la mauzo na mapokezi huchukua wanaoletewa na marafiki au ndugu bila kuangalia vigezo stahiki.”

“Kufanya hivyo kunaweza kusababisha biashara ijae wafanyakazi wasiofaa, hivyo kushindwa kukua au kuendelea kwa muda unaotegemewa,” Phibbs anasema.

Anaweka wazi kuwa hata aina ya maswali yanayoulizwa katika usaili kwa mtaka kazi ya mauzo yana nafasi kubwa ya kuinyanyua au kuiangusha biashara husika.

Anasema hilo linamaanisha kuwa wauliza maswali lazima wajipange na kujiandaa kuwa na maswali yatakayowawezesha kumpata mtu sahihi atakayeisaidia biashara na wala si ilimradi mfanyakazi.

Kwa maelezo yake, kuchukua mtu ilimradi ni mtu au mfanyakazi ilimradi awepo kujaza nafasi kutaisababisha biashara iendeshwe ilimradi na matokeo yake hata kukua kwake kutakuwa ni ilimradi tu.

Kitabu cha Phibbs kinafafanua mambo mengi katika kipengele cha jinsi ya kupata wafanyakazi kwa ajili ya Idara ya Mauzo wenye kuweza kuiinua biashara husika.

Anasema kukosea kwa kuuliza swali lisilo na mantiki au kutokuwa na msaada wa moja kwa moja kwa biashara, kwa maana ya kuhoji jambo la ilimradi tu ili kuonesha kuwa swali limeulizwa, ni kujiharibia. Kuendesha biashara ilimradi kunatokana na mmiliki wa biashara mwenyewe kwa kutojua anataka nini, kifanywe na nani mwenye uwezo gani na kwa sababu gani, kwa wakati gani.

“Hiyo ndio maana wakati wote mfanyabiashara anapolia kupata hasara huangalia alikosea wapi kuanzia katika mchakato wa kuajiri hadi kwenye upande wa kuelekeza mtaji kwenye matumizi,” Phibbs anasema.

Anaongeza kuwa, kuwepo kwa lengo la kuifanikisha biashara yoyote kunatoa msukumo kwa mmiliki na, au watendaji wake kutoruhusu iendeshwe ilimradi.

Anasema linapokumbukwa suala la lengo kuu kwamba ni lazima litimie (kukua kwa biashara) wahusika wote hufuata taratibu na kanuni za kuendesha biashaa husika, jambo linalopaswa kuzingatiwa na kutekelezwa wakati wote katika kipindi chote cha uhai wa biashara husika.

Maelezo ya Phibbs katika kitabu hicho yanatoa ufafanuzi zaidi kuhusu swali lililoulizwa na Mfaume Boniphace wa Bombo, Tanga, aliyetaka kujua ikiwa kuna umuhimu wa kumfanyia usaili mtu anayetaka kazi ya kuuza bidhaa katika biashara ya bidhaa kwenye kampuni ya mtu binafsi.

Sijaanza moja kwa moja na swali kwa sababu niliona kuna umuhimu pia kwa kila mfanyabiashara anayeifuatilia safu hii kufahamu kwamba inawezekana uzembe au kutojali mambo kukachangia kufanya biashara iwe ya hivihivi, yaani iliyodumaa, isiyokufa wala kukua na isiyoleta mafanikio yoyote.

Biashara ya aina hiyo Phibbs ameiita ya ilimradi.

Kuhusu swali la Boniphace, bila kuhitaji utaalamu wa hali ya juu wa masuala ya biashara, ninapenda kujibu kipengele cha biashara ya mtu binafsi kwa kusema kuwa, cha msingi kinachopaswa kuangaliwa hapo ni lengo la biashara.

Ninaamini kuwa kila biashara inalenga mafanikio, hivyo iwe ya mtu binafsi, taasisi ya umma au ya serikali, suala la kupata mafanikio ndio linalopewa kipaumbele zaidi na kutegemewa.

Phibbs ameelezea pia umuhimu wa mfanyabiashara kuhakikisha anachouza kinawafaa wateja wanaonunua na kusema kwamba kuuza tu bidhaa au huduma ilimradi, bila kuangalia ubora na uhitaji kwa wakati husika huenda kusiwe na msaada kwa wanaotaka huduma au biadhaa.

Anashauri ufanyike utafiti kujua nini kinahitajika na ubora uzingatiwe.

Habari na Namsembaeli Mduma Simu; 0752 779 090 au Baruapepe; [email protected].

Comments are closed.