KILA msanii huwa na njia zake za kupita kabla ya kuja kutusua na kuteka mashabiki. Kuna wale ambao wametoka wakiwa wenyewe kwenye nyimbo zao na wale wengine ambao wametumia migongo ya wenzao kuweza kutesa.
Suala la msanii mmoja kumshirikisha mwenzake ‘kolabo’, ni jambo la kawaida lakini kuna wasanii ambao walitumia nafasi hizo kuweza kutambulika katika ulimwengu wa sanaa na hivi sasa wamekuwa nyota ambao wanatikisa vilivyo.
Ingawa kuna listi ndefu ya wasanii ambao wamefanikiwa kutoka kwa kutumia kuwashirikisha wasanii wenzao lakini hii hapa ni orodha ya miongoni mwa wasanii ambao kolabo na wasanii wenzao ziliwabeba na sasa wanatamba.
DARASSA
Nani asiyemjua msanii huyu ambaye ngoma yake ya Muziki imemfanya kuwa maarufu kwa rika zote kuanzia watoto hadi watu wazima?
Lakini mafanikio aliyonayo leo msanii huyu anayejulikana kama Shariff Thabeet, yalitokana na kolabo yake aliyofanya na msanii mwenzake, Bernard Paul ‘Ben Pol’ katika Wimbo wa Sikati Tamaa ambao ndio uliomtambulisha katika tasnia ya muziki wa Bongo.
Wakati Darassa anautoa wimbo huo hakuwa na umaarufu wa kihivyo lakini Ben Pol tayari alishaliteka soko kutokana na mikwaju yake ya Nikikupata na Samboira na baada ya hapo wameendelea kuwa na ukaribu wa pamoja na hata sasa wote wanatamba na Wimbo wa Muziki ambao wameshirikiana tena.
DITTO
Msanii ambaye ameuambia moyo wake usukume damu na uachane na kujipa kazi za vitu vingine, naye anaingia kwenye makala haya kwa sababu alijulikana kwenye ulimwengu wa sanaa kutokana na kolabo ambayo ndiyo imemfanya afike hapa alipo.
Kwa wale wanaomsikia sasa Ditto, kila kitu chake kwenye muziki wake kilibadilika baada ya kufanya ngoma n a Suleiman Msindi ‘Afande Sele’ katika mkwaju wa zamani wa Darubini Kali ambao ulimpa mafanikio ma kubwa, hasa kujulikana kwa jamii.
MALAIKA
Ni miongoni mwa wadada ambao wanafanya vizuri katika chati ya muziki wa Bongo kutokana na baadhi ya nyimbo zake kama Mwantumu , Sare Sare, Zogo na Raruararua lakini umaarufu wake ulikuja baada ya kupata shavu la kupiga kolabo na msanii Chegge katika Wimbo wa Uswazi Take Away.
Tangu ashirikishwe katika wimbo huo, Malaika hajafanya makosa ya kupotea kwani amekuwa akitoa nyimbo ambazo zinaendelea kumpa nafasi ya kutamba hapa nchini.
STEVE RNB
Ni miongoni mwa wasanii ambao wana ufanya Muziki wa RnB kuendelea kuwa katika chati hapa nchini. Naye alijulikana baada ya kufanya kolabo.
Wapenda muziki wa hapa nchini walianza kumuelewa zaidi baada ya kushirikishwa kwenye Wimbo wa Tabasamu wa Mr Blue ambao aliufanyia kazi kwelikweli kwenye kiitikio na baada ya ngoma hiyo mambo yakamu endea vyema.
SHETTA
Nurdin Bilal ndiyo jina lililo kwenye hati zake za kusafiria lakini kwa wale wapenda muziki wanamtambua kama Shetta ambaye amewahi kutamba na ngoma kali kama Namjua, Nidanganye, Kerewa, Mdananda na nyingine.
Lakini yote hayo yalikuja baada ya ngoma yake ya Nimechokwa ambayo alimpa shavu Mbongo Fleva mwenzake, Abednego Damian ‘Belle 9’ ambaye kwa kipindi hicho alikuwa anatamba mitaani na pini yake ya Sumu ya Penzi. Baada ya kolabo hiyo, Shetta ameendelea kuwika vilivyo hadi kufanikiwa kupiga kolabo na wasanii wakubwa Afrika kama Mnigeria, KCEE katika Ngoma ya Shikorobo.
OMMY DIMPOZ
Staa wa nyimbo ya Achia Body ambaye naye umaarufu wake kwenye muziki wa Kizazi Kipya umekuja baada ya kupitia mgongo wa kolabo.
Wakati anatoka Ommy Dimpoz ambaye hati yake ya kusafiria ina jina la Omari Faraji Nyembo, alifanya ushirikiano na Ally Saleh Kiba ‘King Kiba’ kwenye Ngoma ya Nai Nai ambayo ilimpa jina na umaarufu mkubwa kutokana na kumshirikisha nyota ambaye alishajitengenezea mizizi katika muziki huu.
BILL NASS
Hana muda mrefu kwenye ‘game’ ya muziki wa Kizazi Kipya lakini ngoma zake za Chafu Pozi, Raha na Ligi Ndogo zimemfanya awe maarufu.
Lakini umaarufu huo umetokana na kolabo ambazo amezifanya na wasanii nguli, Naaziz wa Kenya kwenye Raha kablaya kuhamia kwa Top in Dar (T.I.D) ambaye aliwahi kuwa kiongozi wake katika Radar Entertainment ambapo kutokana na kolabo hizo, anaendelea kutikisa vilivyo. Alishirikiana na T.I.D kwenye Ligi Ndogo
Comments are closed.