The House of Favourite Newspapers

Chameleon Aiba 100M Bongo

 

chamilion-1

Jose Chameleone

RISASI MCHANGANYIKO Januari 18 2017

DAR ES SALAAM: Mkongwe wa muziki wa kizazi kipya wa Uganda, Joseph Mayanja ‘Jose Chameleone’ amejipatia zaidi ya shilingi milioni 100, mali ya mzalishaji nguli wa muziki wa Bongo Fleva, Paul Matthysse ‘P Funk’, Risasi Mchanganyiko lina mchapo kamili.

Chameleone anadaiwa kuuza mdundo (beat) mali ya P Funk bila kumpa hata ‘thumni’ na yeye kutia kibindoni zaidi ya dola 50,000 za Kimarekani, (zaidi ya shilingi milioni 100) baada ya kulipwa na kampuni inayojishughulisha na masuala ya filamu, Walt Disney ili kuruhusu mdundo unaosikika katika kibao cha Profesa Jay cha Nikusaidieje, mali ya P Funk, utumike kwenye sinema ya Queen of Katwe iliyotoka mwishoni mwa mwaka jana bila ridhaa yake.

Akizungumzia sakata hilo, P Funk alisema, Chameleone si mtu mzuri kwani alianza kumuingiza mjini tangu mwaka 2006 alipoichukua beat  ya Nikusaidieje na kuiingizia mashairi ya wimbo wake na kuuita Bomboclat.

“Unajua zamani tulikuwa tunatoa wimbo katika mfumo wa CD, tunapeleka redioni. Kwenye hiyo CD tulikuwa tunaweka beat tupu, sauti pekee (akapela) na wimbo wenyewe uliokamilika.

  p-funk

P Funk

“Sasa jamaa (Chameleone) akaiba ile beat, akaingiza mashairi ya Bomboclat bila hata kuniambia chochote. Nikamueleza, akakubali kunilipa dola 2000. Nikamkubalia lakini akaingia mitini. Kama hiyo haitoshi, wimbo huohuo ambao beat yake ameniibia, akaenda kuuza tena Walt Disney, napo nilimcheki akaanza kuleta longolongo zilezile za mwanzoni.

“Akaanza ooh sijui nimefanya ili tuzidi kujitangaza mara ooh sijui wamenipa hela kidogo kama dola 2000, nikaona huyu anataka kuniletea ushenzi, lazima nimfunze adabu, nikazungumza na Cosota (Chama cha Hakimiliki Tanzania), wakawaandikia barua wenzao wa Uganda lakini nao hawakujibu chochote,” alisema P Funk.

Ili kumuonesha kwamba ‘amemaindi’, P Funk kupitia kwa wanasheria wake waliuandikia barua ya kiofisi (official letter) uongozi wa Disney ambao ulishtuka kusikia kwamba yeye ndiye mmiliki halali wa mdundo huo, hivyo ukamuomba suala hilo walimalize kirafiki.

“Wameniambia kwamba watafanya mahesabu yao na kuona natakiwa kulipwa kiasi gani na wao wenyewe watajua Chameleone watamshughulikia vipi,” alisema P Funk.

Risasi Mchanganyiko lilifanikiwa kupata simu ya nyota huyo mkongwe wa Uganda, lakini baada ya kujitambulisha na kumsomea tuhuma hizo, alisema yeye siyo Chameleone, bali ni mtu wa menejimenti yake ambaye alipotakiwa kutoa majibu ya kiofisi kuhusu suala hilo, alisema mwenye majibu ni msanii mwenyewe.

Mtu huyo wa menejimenti alitoa namba binafsi ya mwimbaji huyo wa kibao cha Valuvalu, lakini mara zote kutwa nzima jana, kila alipopigiwa, simu yake iliita bila kupokelewa hadi ilipokatika.

Licha ya kutumiwa pia ujumbe uliojaa tuhuma hizo, Chameleone hakujibu.

Erick Evarist/ GPL

 

Comments are closed.