The House of Favourite Newspapers

Recho: Umesifiwa kukimbia Mpaka Ukapitiliza Kwenu

Recho

    STORI: HASHIM AZIZ | AMANI | MAKALA

“…Kutenda kosa siyo kosa kurudia kosa ndiyo kosa, ahsante kwa kunielewa aaaah! Nikitenda tena yaleyale, usinisamehe, usinisamehe! Nikirudia tena yaleyalee… usinisamehee… nashukuru umerudi, nashukuru umerejeaa, moyoni mwangu umerudi, umesamehe niliyokoseaa…” hicho ni kipande cha mashairi ya Wimbo wa Nashukuru Umerudi, wa mwanadada Winfrida Josephat ‘Recho’, aliye zao la Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT)!

Kizunguzungu ndiyo ngoma iliyomtambulisha Recho kwenye gemu la Muziki wa Kizazi Kipya, mwaka 2011, watu wakaanza kuulizana ‘huyu ni nani anayefanana na Ray C (Rehema Chalamila) kuanzia mwonekano, macho, kiuno mpaka sauti?’

Ray c

Hawakuwa wamekosea kumfananisha Recho na Ray C, hata mimi nilipomuona kwa mara ya kwanza, niliamini lazima atakuwa na undugu na Ray C lakini kumbe hawana unasaba wowote zaidi ya kufanana tu kimwonekano kwa maana ya duniani wawiliwawili!

Recho mwenyewe, anakiri kwamba anafanana sana na Ray C, hali kadhalika Ray C naye analitambua hilo na kwa sababu Recho aliibuka kipindi ambacho mwanadada Ray C alikuwa ameshaanza kupotea kwenye ramani ya muziki Bongo, mrembo huyo  ‘mbichi’ alitabiriwa makubwa.

Ray c

Hata mwenyewe amewahi kusema kwamba Ray C ndiye role model wake, kwa maana ndiye aliyemvutia mpaka kuingia kwenye gemu la muziki Bongo! Mpaka leo ninapoandika makala haya, Recho na Ray C ni kama mtu na mdogo wake, wameshafanya baadhi ya shoo pamoja na kuwakonga vilivyo mashabiki wao.

Ray C

Kila mmoja aliamini kwamba Recho ataliziba pengo la mwanadada Ray C na kweli aliweza kufanya hivyo ipasavyo. Mwaka mmoja uliofuatia, akatoka na ngoma nyingine kali iliyomake headline, Upepo, jina lake likazidi kupaa. Hatujakaa sawa, akatoka na Nashukuru Umerudi, akathibitisha kwamba hakuwa amebahatisha kwenye gemu!

Anabahatishaje sasa wakati ametoa ngoma tatu mfululizo na zote zimehit? Hayo yalikuwa ni mapambazuko makubwa kwenye maisha yake, akatoka kwenye orodha ya wasanii chipukizi na kuwa miongoni mwa wasanii wenye majina Bongo! Akapendwa na watu wa rika zote!

Nani ambaye anaweza kusikiliza Wimbo wa Nashukuru Umerudi akaacha kumsifia Recho? Vijana, watu wazima, wazee kwa watoto, wote waliupenda wimbo huu! Ikawa kila kwenye shoo kubwa Recho lazima atumbuize na shangwe alizokuwa anazipata kutoka kwa mashabiki wake, zilikuwa ni dalili za ushindi mkubwa.

Hata hivyo, Wazungu wana msemo wao maarufu kwamba ‘more money more problems!’ wakimaanisha kadiri mtu anavyozidi kupata fedha nyingi ndivyo anavyozidi kukumbana na matatizo mengi maishani mwake! Sisi Waswahili huwa tuna nahau moja maarufu sana kwamba unaposifiwa kwamba una mbio, kuwa makini usije ukakimbia mpaka ukapitiliza kwenu!

Recho alisifiwa sana kutokana na jinsi alivyoweza kuvivaa vizuri viatu vya Ray C kwenye muziki! Kuanzia sauti, kucheza mpaka mwonekano! Maskini Recho akiwa bado msichana mdogo kabisa, akiwa na ndoto nyingi maishani mwake, akalewa sifa, akakimbia na kupitiliza kwao!

Jina lake likaanza kutajwa kwenye orodha ya wasanii wenye tabia zisizofaa kwenye jamii. Akaanza kuripotiwa kwamba amebadilika na kuwa mlevi, anaonekana kwenye kumbi za starehe usiku akiwa bwiii!

 

Racho na Ditto

 

Racho

Akaanza kuhusishwa na skendo za kutoka na wanaume tofauti. Yote hayo yalikuwa ni madai ambayo mwenyewe alikuwa akiyakanusha mara kwa mara! Yote tisa, kumi akaanza kutajwatajwa kwamba naye ni miongoni mwa watumiaji wa ngada!

Sikuwahi kuamini madai hayo, hata leo ninapoandika makala haya, bado nakuwa mgumu kuamini, hata baada ya jina lake kutajwa na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwamba eti Recho ni miongoni mwa watumiaji wa hiyo kitu, akashikiliwa ‘sentroo’ na mastaa wenzake wengi, wakiwemo Wema Sepetu, TID, Nyandu Tozi, Lulu Diva na wengine ambao hatimaye walipandishwa kizimbani na kuachiwa kwa dhamana!

Recho

Sitaki kumhukumu yeyote kati ya waliotajwa, akiwemo Recho mwenyewe kwa sababu ukweli wa madai hayo, kila mtu anaujua mwenyewe ndani ya moyo wake! Ninachotaka kusema na wewe Recho… inafahamika kwamba Ray C amekuwa mtumiaji wa madawa ya kulevya kwa kipindi kirefu na mwenyewe alishakiri na kueleza kwamba yupo kwenye vita ya kupambana ajitoe (Mungu amsaidie)!

Kwa hiyo Recho ulipogundua kwamba unafanana na Ray C, na ukaona viatu vyake kwenye muziki vimekutosha na umejipatia mashabiki wengi na mafanikio makubwa, umeona haitoshi mpaka ukataka kuiga hata yale yasiyofaa kutoka kwake? Kama madai hayo ni ya kweli, bado hujachelewa, muda wa kujirekebisha unao kwa sababu kiumri bado wewe ni mdogo! Iga yale mazuri tu kutoka kwa Ray C, hakika utafika mbali lakini ukianza na hayo mengine, msemo wa umesifiwa kukimbia ukapitiliza kwenu, utakuwa unakuhusu!

Shinda Nyumba Awamu ya Pili Yatikisa Jiji la Dar es Salaam

Comments are closed.