
Na IMELDA MTEMA| RISASI JUMAMOSI| MPAKA HOME
MAMBO vipi mpenzi msomaji wangu, kama kawaida kila wiki ndani ya safu hii maridhawa ya Mpaka Home ni kuwatembelea mastaa mbalimbali majumbani mwao na kufanya nao mahojiano. Leo tunaye mwanamuziki wa kitambo kidogo, Faiza Omary ‘ Sister Fay’ lakini hivi karibuni ameibuka upya baada ya kutoa wimbo wake uitwao Kaja Mwenyewe.


Mwanamuziki huyu ambaye pia ni muigizaji anaishi maeneo ya Kinondoni Mkwajuni na mtoto wake wa kiume pamoja na ndugu zake wengine. Amezungumza mambo mengi kuhusiana na maisha yake ya kila siku nje na kazi yake, ungana nami ili uweze kuyafahamu.

Maisha yake ya kawaida yakoje?

“Maisha yangu hayana tofauti na ya watu wengine, naishi maisha ya kawaida kama unavyoniona hapa hakuna kilichobadilika kwangu kabla sijawa staa na nilivyo sasa, sina tofauti na watu wengine. Ameolewa? Nimeolewa lakini kwa bahati mbaya sana mume wangu haishi hapa yuko nchini Uingereza na kwa kweli ananipa sapoti kubwa katika ishu zangu za sanaa, namshukuru sana kwa hilo.

Anawezaje kuishi mbali na mumewe, kuhusu michepuko kumsumbua?

“Unajua hayo mambo kama mwanamke anajifanya hawezi kuishi muda mrefu bila kuwa na mumewe karibu ni kujiendekeza tu, kikubwa kama hauna tamaa na umejenga uaminifu kwa umpendaye haina shida na michepuko haina nafasi kwenye maisha yangu.

Kwa nini anapendelea kuvaa nguo za kiume?

“Mimi najiona sina umbo zuri la kuvaa nguo za kike sipendezi na nikagundua nikivaa za kiume angalau zinaficha umbo langu ndiyo maana napenda ila nikienda sehemu ambazo zinahitajika kuvaa mavazi kama hayo, navaa bila shida.Vipi ni mtaalamu katika mapishi?
“Katika hilo napenda kujipongeza ni mtaalamu na ninajua kuliteka jiko kama mwanamke niliyefundwa nikafundika najiamini kwa hilo na mume wangu anapenda sana mapishi yangu na ninafikiri kitu ambacho anakimisi zaidi akiwa mbali nami ni mapishi yangu.
Alishawahi kulala sebuleni?

“Mara nyingi sana tena kipindi hiki nilichokuwa narekodi wimbo wangu ni balaa, nikirudi tu nikisema nijipumzishe sebuleni napitiwa na usingizi, nikishtuka ni asubuhi basi nanyata mpaka chumbani
ili wadogo zangu wasinione kuhofia watanicheka.
Kitu gani kilimuumiza maishani?

“Nilipowapoteza wazazi wangu niliumia sana na bado kinaendelea kuniumiza mpaka leo. Anaishije na majirani zake? “Uzuri wewe umekuja umeweza kushuhudia mwenyewe kwa macho yako ninavyoishi nao vizuri na kama mtu hajawahi kuniona kwenye runinga wala kusikia wimbo wangu anaweza kujua mimi ni mtu wa kawaida.

Nini matarajio yake ya baadaye? “Napenda kufika mbali niwe na maendeleo mengine zaidi ya hapa, natamani kuwa na nyumba kwa sababu bado napanga. Kwa nini alikuwa akisema Magali ni baba yake mzazi wakati siyo?

“Hiyo ilikuwa kupaishana tu majina lakini kulikuwa hakuna ukweli wowote wala hatuna undugu.”








Comments are closed.