The House of Favourite Newspapers

Leo Hapatoshi Dar Live

Khadija Kopa

Na WAANDISHI WETU| GAZETI LA UWAZI| SHOWBIZ

WKATIKA kusherehekea Sikukuu ya Wapendanao ‘Valentine’s Day’ leo usiku, Februari 14, ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar patakuwa hapatoshi kufuatia kupaniana kwa bendi mbili zinazofanya vizuri kwenye Muziki wa Taarabu ambazo ni TOT na Africa Taarab.

Bi Mwanahawa

Akichonga na Uwazi Showbiz, Malkia wa Mipasho, Khadija Kopa ambaye usiku huo atakuwa na kundi lake la TOT akichuana vilivyo na mkongwe mwenzake wa Kundi la East Africa Melody alisema amewataka mashabiki wake wajitokeze kwa wingi usiku wa leo Dar Live kwani amepania kuwaonyesha mashabiki wake Taarab ilivyo.

Itakuwaje?

Akizungumza na Showbiz Xtra, Kopa ambaye usiku huo atakuwa na kundi lake la TOT akichuana vilivyo na mkongwe mwenzake wa Kundi la East Africa Melody, Bi Mwanahawa alisema, anajua mashabiki wengi siku hizi wanapenda kuwasikia wakongwe kuliko wasanii wanaoibuka hivyo atatumia nafasi hiyo kuwapa ladha ya kitofauti.

“Sipendi niongee sana, kikubwa tukutane leo Dar Live ili niwape ladha iliyokamilika ya Taarab,” alisema Kopa.

 Bi Mwanahawa naye atamba

Kwa upande wa Bi Mwanahawa alisema hatawaangusha mashabiki wake kwani wamejiandaa vya kutosha.

“Kwa wale wasiojua maana kamili ya mirindimo ya Pwani basi wajisogeze ndani ya Dar Live kwani ni zaidi ya kutoana jasho usiku huo,” alisema Bi Mwanahawa.

Patakuwa hapatoshi

Akizungumzia shoo nzima, Meneja wa Dar Live, Juma Mbizo alisema kuwa, usiku huo vibao vingi vitarindima ambapo kwa upande wa Khadija Kopa atashusha vibao vyake vyote vilivyowahi kubamba na ambavyo vinaendelea kubamba.

“Kopa ataanza na Mjini Chuo Kikuu, Fahari ya Mwanamke, Nimpe Nani, Kadandie, Magumegume na nyingine nyingi huku Bi Mwanahawa akirudisha mashambulizi kwa vibao vikali kama Wakerekwao, Wema na Roho Mbaya Haijengi,” alisema Mbizo.

 Sapraizi kibao kutolewa

Mbizo alimalizia pia kwa kapo 100 wa kwanza watakaopendeza watapata sapraizi kibao ambazo zimeandaliwa na ukumbi huo sambamba na huduma bora ya VIP.

“Siku zote Dar Live huwa tunajali mashabiki wote wa burudani. Mbali na uwepo wa nyama choma, flat screen kila engo na red carpet safi ndani, usiku huo utakuwa wa kipekee kwa kuwapa kipaumbele kapo 100 wa kwanza watakaotoka chicha zawadi na pia huduma bora ya VIP.

“Wapendanao wote niwatoe pia wasiwasi, safu ya ulinzi imepangwa vizuri kwa hiyo si jambo la kuhofia,” alimalizia Mbizo.

Comments are closed.