The House of Favourite Newspapers

Fid Q Kajivika Mabomu kwa Joh Makini

Fid Q

 JOHN JOSEPH| CHAMPIONI IJUMAA| MAKALA

WIMBO unaokuwa mzuri na umekamilika kuanzia sauti, uimbaji, utayarishaji na ikiwezekana video nzuri ni rahisi kutamba, lakini katika dunia ya sasa kuna vigezo vya ziada vimekuwa vikitumika kuufanya wimbo utambe.

Nizungumzie kwa Tanzania, ukiondoa ubora wa wimbo na video yake, kuna vitu kama ‘drama’ au ‘kiki’ vimekuwa vikiongeza nguvu. Tangu miaka ya zamani kuna kitu kinaitwa bifu, yaani vita ya maneno baina ya wasanii au pande mbili za wasanii zimekuwa zikichangia sana kukuza ushindani wa muziki na kwa wale wenye akili ya haraka wamekuwa wakitumia bifu kutengeneza fedha.

Mfano hai ni bifu kati ya Diamond Platnumz dhidi ya Ali Kiba, wote wanatoa muziki mzuri lakini siyo kwamba ni bora sana kuliko kina Jux, Barnaba, Ben Pol au wengine ila kwa kuwa asili ya mashabiki wa Tanzania wanapenda kushindanisha nani ni bora ndiyo maana wao wanafatiliwa zaidi.

Fitina za hapa na pale za wanaowasimamia zinachombeza utamu na wahusika wanaingiza fedha kupitia ushindani huo, ndiyo maana hata kabla ya kutoa wimbo lazima wajipange kuhakikisha hawawaangushi mashabiki wao wanaowaunga mkono. Kuna wasanii wengi wa kawaida ambao wamewahi kutamba na kuingiza fedha nyingi kisa tu walikuwa na bifu.

Ilipotokea wamepatana kuna mambo mawili yaliyokea. Wajanja waliungana na kutengeneza kazi pamoja kisha wakaongeza umaarufu wao na baadhi waliopatana kisha wakaendelea kufanya kazi zao, umaarufu wa kazi zao ulishuka kwa kuwa hakukuwa na mtu wa kuwashindanisha.

Mifano halisi hii hapa:

NASMA KIDOGO VS KHADIJA KOPA

Nani ambaye alikuwa hajui vita hii ya nguli hao wa Muziki wa Taarab! Wote walikuwa na uwezo wa juu lakini ushindani uliotengeneza bifu kati yao ulifanya muziki wao na tasnia yao ikue. Ilikuwa kawaida kusikia Taarab ikipigwa kwenye vituo vingi vya redio, walifanya shoo nyingi huku vijembe vikiendelea kutawala kila kona.

Khadija Khopa

 

Baada ya muda wanamuziki hao walipatana, ikawa habari kubwa ambayo baada ya muda ikapotea kama upepo, licha ya kuendelea kufanya kazi kila mtu kivyake umaarufu wao ulishuka na tangu kupatana kwao taarab ikapoteza umaarufu wake, haijarejea katika ubora huo ikiwa ni zaidi ya miaka 10 imepita tangu kupatana kwao.

Nasma Hamis Kidogo

JUMA NATURE VS INSPEKTA HAROUN

Inspekta ndiye aliyeanza kutamba zaidi kuliko Nature, vita yao ikaifanya rap katuni kutoka Temeke kupata umaarufu, kila kona ikawa ni wao tu. Staili yao ya kurap ikawa maarufu na vijana wengi wakawaiga wao, ilikuwa kama ilivyo Diamond na Kiba kwa sasa. Walibeba kijiji kila mashabiki walipokuwa wakiwaona, baadaye Nature akapanda jukwaani kuomba amani, lilikuwa jambo kubwa. Bahati nzuri hawa walitumia nafasi hii kutoa wimbo pamoja, Mzee wa Busara ndiyo jina la wimbo wao ulioitikisa Tanzania.

Juma nature (kushoto) na Inspector Haroun

Baada ya hapo Nature akaendelea kutamba, muziki wa Inspekta ukawa imefikia ukingoni, hakutamba tena kama awali kwa kuwa hakukuwa na wa kumshindanisha naye.

EAST COAST TEAM VS WANAUME FAMILY

Siyo kwamba wasanii wa pande hizo hawakuwa marafiki, hapana! Walikuwa wakikutana studio na wanaishi vizuri tu lakini kimuziki wakiiaminisha jamii kuwa wao ni maadui wakubwa, wakapata mashabiki wengi, kila wimbo ukitoka wanashindanishwa. Bila shaka, hakuna familia za muziki zilizotikisa kama pande hizi mbili. Baadaye ukaribu wao ukaanza kuonekana hadharani, mashabiki wakahisi wanawazingua, wakaamua kuwapotezea na ndiyo ukawa mwanzo wa familia hizo kuparaganyika kwa kuwa hakukuwa na wakuwashindanisha bali wakaanza kushindana wao kwa wao ndani ya makundi yao.

BANZA STONE VS ALI CHOKI VS MUUMINI MWINJUMA

Hawa waliifanya dansi kupata mashabiki wengi, walihamisha fikra za Watanzania kutopenda muziki wa dansi wenye miondoko ya Kicongo na badala yake wakawa na fleva zao flani hivi tofauti. Walikuwa wakipigana vijembe kila kukicha kuanzia kwenye nyimbo hadi katika maisha ya kawaida. Ikawa ni utamu tu kusikia kila upande umetoa nyimbo gani na una uzuri kiasi gani, wao ndiyo waliokuwa wameiteka dansi ya kisasa na kufanya muziki wa Bongo Fleva kuwa na wakati mgumu, lakini walivyopatana tu dansi ikapotea na hadi leo muziki huo unapumulia mashine.

ZAY B VS SISTER P ‘Zay to the B mwanadada gaidi….’

Zay B

Daaa ilikuwa furaha ya ajabu ukimsikia akirap, upande wa pili unasikia ‘anakuja anakuja Sister P…’ ushindani wao ulikuwa mkali kiasi kwamba kuna wakati ilibidi kituo kimoja cha runinga kirushe kipindi ‘live’ kwa ajili ya kuwapatanisha wasanii hao. Nakumbuka tukio hilo nililishuhudia nikiwa nasoma sekondari, kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliokuwa wakifuatilia tukio hilo na hata wiki hiyo ikawa habari kubwa magazetini na kwenye redio. Nyimbo zao zilikuwa na vijembe na ziliifanya Bongo Fleva ikachangamka.

Sister P

Walipopatana tu, watu wakaanza kuona kama wote hawana jipya, kila walivyotoa nyimbo hazikutamba, mwishowe wakapotea kwa wakati mmoja.
FID Q VS JOH MAKINI

Mifano ya juu ipo mingi lakini kwa nafasi hiyo inatosha kumaanisha kile ninachokizungumzia. Kwa miaka mingi tetesi kuwa John na Fid Q wana bifu na kuwa hata kwenye nyimbo zao wamekuwa wakipigana vijembe zimekuwepo kiasi kwamba mifano ipo mingi ya mashabiki kuchukua mashairi yao na kuyalinganisha. Wenyewe hawakuwahi kujitokeza kuzungumzia kinachoendelea, hilo liliongeza ushindani, kutoka kwenye mashairi sasa vita ikahamishiwa hadi kwenye video kali, hilo lilikuja baada ya Joh kutoa video zinazoonekana kuwa kali zaidi ya zile alizokuwa akitoa Fid, baada ya muda Fid naye akaanza kutoa video kali basi utamu ukazidi kunoga.

Joh Makini

Miezi ya hivi karibuni wawili hao wakaanza kuonekana kuwa karibu katika baadhi ya matukio, wiki jana Fid akajitokeza live na kumpongeza Joh kwa kutoa video nzuri na kuwataka watu waitazame, hiyo ikawa habari kubwa, nikajua kitakachofuata hapo labda ni kolabo. Binafsi niliitazama bifu yao ambayo hata kama haikuwepo kuwa biashara nzuri kwao, ila kitendo cha Fid kikipita kisha maisha yakaendelea naamini yaliyotokea kwa wasanii wa juu yatajirudia, simaanishi nataka wasanii wawe na bifu lakini zikitumika vizuri kama ilivyo kwa Diamond na Kiba zinachangamsha ‘game’, tofauti na hapo muziki wao utapoa na idadi ya wafuatiliaji itapungua.

Comments are closed.