The House of Favourite Newspapers

Amigo: Mzee Yusuf Alinikabidhi Jahazi Kitambo

Baadhi ya waimbaji wa Muziki wa taarabu ‘Jahazi Modern Taarabu’

Na MWANDISHI WETU| GAZETI LA UWAZI| UWAZI SHOWBIZ

IKIWA imeshapita miezi kadhaa tangu aliyekuwa Mfalme wa Taarab na Mkurugenzi wa Kundi la Jahazi Modern, Mzee Yusuf aachane na muziki huo na kumrudia Mungu, staa aliyekabidhiwa mikoba yake, Prince Amigo ameweka wazi kuwa, tangu Mzee aondoke hajawahi kuwasaidia chochote kinachohusiana na muziki.

Ally Jay wa kwanza (Kushoto), Mishi (Mamaa wa masauti) na Amigo

Akizungumza na Global TV Online, Prince anayeliongoza Kundi la Jahazi linalotarajiwa kuangusha bonge la shoo la kutimiza miaka 10 wikiendi hii, (Februari 25) ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar alisema, Mzee Yusuf kabla hajawaacha alikuwa msaada mkubwa sana katika kutunga, kuimba na kutengeneza nyimbo lakini kwa sasa hataki kusikia vitu hivyo.

“Ukitaka kukorofishana na Mzee (Yusuf) basi we mwambie kuhusu Muziki wa Taarab, asipokukatia simu basi atakublock kabisa. Kabla hajamrudia Mungu alikuwa msaada mkubwa hilo sikatai lakini katika kutunga alikuwa akisaidiana na watunzi kutoka Zanzibar na Dar ambao ndiyo wanaendelea kutusaidia sasa.

“Kwa sasa Jahazi limerudi katika ubora wake na linatisha. Naomba niweke wazi kuwa hii ishu ya Mzee Yusuf kuachana na Taarab aliwahi kuniambia tangu zamani, mwaka 2010 tulikuwa wote Dodoma kwenye shoo akaniambia ipo siku ataachana na muziki na mimi ndiye nitachukua mikoba yake. Kwa hiyo utaona ni jinsi gani alivyokuwa akinitengeneza mapema,” alisema Amigo.

Ally Jay wa kwanza (Kushoto), Mishi (Mamaa wa masauti) na Amigo

Amigo aliyekuwa ameongozana na mpiga kinanda Ally Jay pamoja na mamaa wa masauti, Mishi aliongeza kuwa, Jahazi itatimiza rasmi miaka 10, Februari 25 hivyo mashabiki wote waje kwa wingi kushuhudia shoo ya kihistoria.

“Kwa mara ya kwanza nitaimba nyimbo tatu ambazo alikuwa akiziimba Mzee Yusuf ambazo ni Tupendane, Anajua Kupenda pamoja na Kaning’ang’ania,” alisema Amigo.

JAHAZI WOTE WA ZAMANI NDANI!

Naye Mratibu na Meneja wa Dar Live, Juma Mbizo alitia neno kuwa, usiku huo wakali wote wa muziki wa Jahazi waliokuwepo tangu kundi hilo linaanza watakuja na kuimba pamoja kama zamani.

“Tutakuwa na wakali wote waliopitia Jahazi na pia mashabiki watapata nafasi ya kujimwayamwaya kwa nyimbo kali kuanzia Mpenzi Chocolate, Nina Moyo Sio Jiwe hadi Tiba ya Mapenzi,” alisema Mbizo.

KIINGILIO BEI CHEE Burudani yote hiyo ya kishindo itakwenda kwa kiingilio kiduchu cha shilingi 8,000 tu.

Comments are closed.