The House of Favourite Newspapers

Kutokwa na Uchafu Ukeni ‘Leukorrhea’

Na Dk CHALE| GAZETI LA IJUMAA| AFYA

HII  siyo  hali ya kawaida mwanamke kutokwa na majimaji au uchafu ukeni au sehemu za siri.Tatizo hili hutamkwa ‘Lukorea’ na huwapata zaidi wanawake walio katika umri wa kuzaa ingawa hata wasichana wadogo na wazee pia huwatokea lakini kwa idadi ndogo. Mwanamke kuwa na tatizo hili haihusiani na mfumo wa mkojo ingawa kumekuwepo na desturi ya wanawake wanapokuwa na hali hii isiyo ya kawaida huita kimakosa Yutiai hivyo hujikuta wanapata tiba isiyo stahili.

CHANZO CHA TATIZO

Lukorea kama ilivyo siyo ugonjwa bali ni dalili ya magonjwa yaliyojificha kwa mwanamke katika viungo vyake vya uzazi ambapo ni ukeni na katika mlango wa kizazi na hata mwilini kwa ujumla kama ana magonjwa sugu ya mfumo wa mwili kifua kikuu, kisukari, kansa na upungufu wa kinga mwilini au HIV.

Vijidudu vinavyosababisha maradhi haya ni aina ya bakteria, protozoa na fangasi. Visababishi vingine ni vijidudu aina ya parasaiti ambao hujificha ukeni, kuwepo na vitu visivyo vya kawaida ukeni, matatizo ya kizazi na nyonga, matatizo katika mfumo wa homoni, kusinyaa kwa uke hasa  katika umri mkubwa, vidonda ukeni, kutokuwa msafi ukeni na kutokwa na ute mzito ukeni hasa kama unatumia baadhi ya dawa za homoni, mfano vidonge vya kuzuia mimba. Matatizo mengine yanayochangia ni tiba za mionzi mfano kwa wenye kansa ya shingo ya kizazi huweza kutokwa na majimaji ukeni pamoja na  matumizi ya vipodozi ukeni.

Pamoja na yote, magonjwa ya zinaa kutokana na vijidudu vya Trikomonia na Gono pia huchangia hali hii. Matatizo mengi ya kutokwa na uchafu mzito ukeni husababishwa na fangasi aina ya candida au monilia, bakteria wakubwa wanaohusika ni aina ya Gonococcal, Spirochetal, Staphylococcal, Streptococcal, Pneumococcal na Tuberculosis, ambapo siyo sana.

AINA ZA TATIZO KUTOKWA NA MAJIMAJI SEHEMU ZA SIRI KWA WATOTO

Watoto wachanga na watoto wadogo ambao hawajavunja ungo wanaweza kupatwa na tatizo hili la kutokwa na hali kama ya majimaji ukeni na yakamshtua mzazi au mlezi. Hali hii siyo ya kawaida  na huwa haitoki ukeni kwa ndani. Chanzo chake huwa katikati ya midomo ya uke au valvu, mara chache sana huanzia ukeni kwa ndani.

Chanzo cha tatizo hili kwa watoto ni uchafu, minyoo au wakiingiliwa na vitu visivyo vya kawaida ukeni na endapo watasuguliwa sana sehemu zao za siri wakati wa kunawishwa au kuogeshwa. Kusuguliwa huku sana kwa watoto katika sehemu zao za siri huitwa Masturbation na husababisha watoto wapate tatizo hili la kutokwa na majimaji kwa hiyo tuwe waangalifu tunapowasafisha watoto wa kike. Uchafu unaweza kusababishwa na kukaa na nepi yenye kinyesi au mkojo kwa muda mrefu bila ya kumbadilisha na kutomsafisha kwa maji baada ya kujisaidia haja kubwa.

Vitu visivyo vya kawaida ni mchanga, kama mtoto hatavalishwa chupi na nguo salama anapocheza hivyo mchanga hujipenyeza katika sehemu zao za siri. Mtoto mwenye tatizo hili wakati mwingine utaona sehemu zake za siri zimevimba na nyekundu na muda wote analia tu maumivu hasa ukimgusa na unaweza kudhani ameingiliwa au amechezewa kumbe ni uzembe wako mzazi kutokuwa msafi.

TATIZO KWA MABINTI

Hapa tunazungumzia kutokwa na majimaji au uchafu kwa mabinti ambao ni bikira, hao pia hutokewa na hali hii. Chanzo ni kama kilekile au vilevile tulivyoviona kwa watoto. Ingawa baada ya kuvunja ungo hupatwa na hali ya kutokwa na majimaji yasiyo na maambukizi mara kwa mara au kila siku na kujihisi wanalowa.

Hali hii hutokana na mfumo wao wa uzazi sehemu za ukeni ambapo hufanya sana kazi katika kipindi hiki cha mpito cha balehe. Kwa hiyo kama hakuna muwasho, harufu mbaya wala maumivu, huwa tunasema ni hali ya kawaida.

UCHAFU WA KAWAIDA

Ipo pia hali ya kawaida inayomtokea mwanamke tunaita Physiological Leukorrhea . Hapa hali ya kutokwa na uchafu ukeni hutofautiana kiwango kati ya mwanamke na mwanamke. Wakati mwingine uchafu huwa mwingi hadi unatisha lakini kitu cha msingi tunaangalia kama hakuna harufu mbaya wala muwasho hivyo mwanamke anaweza kuishi hivyohivyo.

Wakati mwingine hali hii ikitokea  kwa wingi katikati ya mzunguko wake wa hedhi ni dalili ya upevushaji wa mayai. Hali ya kawaida pia inaweza kuwa ni ute wa uzazi ambao umegawanyika katika makundi matatu. Kwanza ni ute mwepesi, pili ni ute wa kuvutika na tatu ni ute mzito.

LEUKORRHEA IN SEXUAL MATURITY

Mwanamke aliye katika kundi hili ni yule ambaye tayari yupo katika mahusiano ya kimapenzi na kulalamika kutokwa na uchafu ukeni ambao una harufu mbaya kama shombo la samaki, rangi ya njano na muwasho. Uchafu huu unaweza kuwa kama maziwa ya mgando au usaha. Hali ya muwasho mkali husababisha maumivu ukeni, maumivu wakati wa kujamiiana na maumivu chini ya tumbo. Uchafu unaweza kuongezeka kila siku na kukukosesha raha.

Hali hii inaweza kusababishwa na maambukizi, kisonono au fangasi, kulika na kuharibika kwa mlango wa kizazi, kuongezeka kwa ute mzito ukeni, maambukizi ya kizazi baada ya kujifungua na saratani ya shingo ya kizazi pia ni sababu.

Uvimbe ndani ya kizazi, kuharibika kwa mimba vyote hivi huchangia mwanamke kutokwa na uchafu wa aina hii ambao huambatana na maumivu upande wa chini wa tumbo.

TATIZO KWA WANAWAKE WAZEE

Wanawake wazee hutokwa na majimaji mepesi ukeni au damu na wakati mwingine huwa na harufu mbaya sana hata akikaa sehemu utahisi anatoa harufu. Hii ni dalili kwamba kuna nyamanyama katika sehemu zake za siri zinaoza, na hii ni dalili kubwa ya saratani ya uke au ya shingo ya kizazi. Kama atatokwa na ute mzito, basi ni dalili ya maambukizi hasa Trikomonia.

UCHUNGUZI NA TIBA

Tatizo hili hufanyiwa uchunguzi kwa madaktari wa magonjwa ya akina mama kwenye hospitali za mikoa. Vipimo mbalimbali kama vya kuangalia mlango na shingo ya kizazi, vipimo vya Ultrasound, vipimo vya damu na vingine ambavyo daktari ataona vinafaa vitafanyika, wahi hospitali kwa uchunguzi na tiba.

Comments are closed.