The House of Favourite Newspapers

DC MJEMA: Wazazi Wenye Watoto Wao ‘Panya Rodi’ Kukamatwa

Sophia Mjema

Na ELVAN STAMBULI NA SIFAEL PAUL| GAZETI LA UWAZI| UWAZI LIVE NA…

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, wilaya anayoiongoza ndiyo kitovu cha nchi kwa sababu ndipo yalipo makao makuu kubwa kuliko zote nchini kimadaraka, yaani Ofisi ya Rais Ikulu lakini pia wilaya yake ndiyo yenye pilikapilika nyingi za maisha kutokana na kuwa na biashara nyingi kubwa.

Wahariri wetu hivi karibuni walifanya mahojiano naye ofisini kwake kuhusu mambo mbalimbali anayokabiliana nayo katika kazi zake za kila siku; ungana nasi:

Swali: Tulipofika hapa katika ofisi yako tumekuta watu wengi sana wakisubiri kukuona, tatizo ni nini hasa?

Jibu: Ni kweli watu wengi wanakuja kwa mkuu wa wilaya wakiamini kwamba kwa kuwa ni mwakilishi wa rais, basi watasaidiwa. Watu wanakuja na kero mbalimbali kuhusu ajira, maji, ulinzi, maisha mazuri na hakika nyingi zinakuwa hazijatatuliwa huko chini ndiyo maana mimi huwasikiliza wananchi kila Alhamisi nikiwa na wataalamu wa ardhi, barabara, maji na kadhalika. Kwa kawaida nimejipangia utaratibu, wananchi wanaanza kwenda kuonana na wataalamu wangu, ikishindikana huniona mimi.

Swali: Kuna matatizo mengi ya wananchi yanayohusu sheria hasa kuhusu ardhi, unafanyaje kutatua matatizo hayo?

Jibu: Ni kweli kuna matatizo mengi sana yakisheria, uzuri ni kwamba mimi hapa nina wanasheria wanane ambao wamejitolea kusaidia watu, nimegundua kuwa wananchi wengi hawajui sheria. Wanasheria wangu wanaenda kila kata kuonana na raia, hii imesaidia kuwafanya wajue haki zao na kutatuliwa matatizo yao.

Swali: Katika wilaya yako wananchi unaowaongoza kero zao kubwa hasa ni ipi?

Jibu: Kero kubwa wilayani kwangu ni ajira, ukosefu wa ajira kwa vijana na akina mama. Hii ni kwa sababu wilaya yangu inapokea watu wengi kila siku wanaingia wageni zaidi ya 100.

Swali: Mnatatuaje kero hiyo?

Jibu: Tunatatua kupitia mambo mbalimbali kama vile michezo na vikundi kwani wakiwa katika kundi wanachama wanaangalia fursa. Tunajaribu kuwa-keep bize (kuwashughulisha), bila kufanya hivyo vijana wanaweza kujiingiza kwenye ujambazi au matumizi ya madawa ya kulevya ambayo tunayapiga vita sana nchi nzima.Hatuna pesa lakini wadau wanaweza kuwasaidia.

Swali: Wilayani kwako kuna kero ya Wamachinga kufanya biashara barabarani, unatatuaje tatizo hilo?

Jibu: Ni kweli tuna Wamachinga wengi wanaofanya biashara barabarani. Tunachofanya sasa ni kwamba lazima tujuwe wapo wangapi ili tuwatafutie maeneo rafiki kwa biashara zao. Kwa kusaidia zaidi, tumeongea na Sumatra (Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Baharini) ili wapitishe mabasi katika maeno yao ili wapate wateja.

Swali: Ni maeneo gani mmeyatenga kwa ajili yao?

Jibu: Maeneo tuliyoyatenga ni kama vile Kigogo Fresh tunatengeneza miundombinu ya maji na umeme upatikane ili wafanye kazi zao vizuri. Msongole, Ngarangaze Chanika, tutatengeneza barabara ili mabasi yaingie kule kuwaongezea wateja.Tunawaomba Wamachinga wote wajiandikishe ili tuweze kuwahudumia na kuwapa maeneo kwa utaratibu mzuri. Tukiwapeleka katika maeneo hayo, wenyewe watatuambia kama kuna matatizo au la.

Swali: Licha ya tatizo la ajira, kero gani kubwa wilayani kwako inayowahusu wananchi?

Jibu: Kero nyingine kubwa ni migogoro ya mashamba ambayo sasa imegeuka na kuwa viwanja. Wavamizi wa viwanja wamekuwa wengi, wavamizi wanajipimia au kujigawia maeneo, sasa tumeamua kupima viwanja kama vile kule Chanika, Msongole, Pugu, Kitonga, tutatumia Mipango Mji ya Mwaka 2017. Maeneo yameanza kupimwa. Tumefanya hivyo kwa sababu kesi ni nyingi na baadhi ni za kutunga, wananchi wanakosa haki zao. Kuna vikundi vinafanya uhalifu kutokana na maeneo kutopimwa. Maeneo yaliyokithiri kwa uvamizi ni maeneo ya Pugu watu wanavamiwa sana maeneo yao na matapeli. Nilielekeza watu waorodheshwe na kama kuna mtu kavamia eneo la mtu ikithibitika, tutawapeleka mahakamani. Kuna madai kuwa kuna viongozi wanashirikiana kufanya maovu, wanauza ardhi ambayo wananchi walilipwa fidia, tutawachunguza, tukiwabaini sheria itachukua mkondo wake.

Swali: Kulikuwa na habari kwamba kuna watu walitimuliwa katika Msitu wa Kisarawe, hilo unalizungumziaje?

Jibu: Ni kweli kwenye Msitu wa Kisarawe wananchi walivamia, ni eneo la hifadhi la Nyeburu. Tumeshawaelekeza maofisa wa Wizara ya Maliasili ili washughulikie tatizo hilo nasi tunasubiri majibu.

Swali: Unazungumziaje vijana ambao wamekuwa wakijiingiza kwenye uhalifu wakiwa na umri mdogo kama hawa wa panya rodi? Jibu: Kusema kweli inasikitisha sana. Wazazi wengine hawajui kwamba watoto wao wameingia kwenye makundi haya hatari. Baadhi ya wazazi hawajui watoto wakitoka majumbani mwao asubuhi wanakwenda kufanya kazi gani. Inasikitisha kuona mtoto wa miaka 12 hadi 15 anajiingiza katika uhalifu.

Vijana wanataka utajiri wa haraka haraka bila kufanya kazi halali. Hawataki kufanya kazi na badala yake wanajihusisha na kucheza kamari za simu. Wakati umefika wa kuondoa viashiria vyote vya uhalifu. Watu wanakaa baa na kucheza pool mchana wakati wa kazi, wanacheza vigodoro, wanafunzi badala ya kwenda shule wanakwenda bichi, tutawakamata, hii ni hatari, tupige vita wote.

Swali: Unadhani tufanye nini kuondoa haya mambo hatari?

Jibu: Ni lazima turejeshe uzalendo, vijana tuwaingize kwenye ulinzi shirikishi, wapate mafunzo ya mgambo na ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Televisheni zetu ziweke picha (sinema) zenye maadili. Kwa mfano China, hakuna tv za nje, zipo za kwao za kujenga jamii. Sisemi kwamba tupige marufuku tv za nje la hasha, isipokuwa kuna haja ya kuangalia sinema zinazooneshwa ziwe na maadili ya kwetu. Utakuta tv inaonesha picha za watu kuchinjana! Huo siyo utamaduni wetu na unajenga ukatili na ujambazi kwa vijana wanaoangalia. Ndiyo maana wanaibuka mapanya rodi. Tukiacha haya makundi ya panya rodi yakikomaa tutashindwa kutawala, hivyo ni jukumu letu wananchi wote kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha makundi hayo yanatokomezwa. Naamini hawa watoto wanaokuwa panya rodi wanalishwa kitu. Wote tuwarejeshe kwenye mstari ili tufaidi matunda ya nchi yetu. Wito wangu kwa wazazi, angalieni sana watoto wenu, haiwezekani mtoto atoke nyumbani asubuhi arudi usiku mzazi usijue alikuwa wapi na alikuwa akifanya nini!

Swali: Unafikiri utoro huo wa watoto unasababisha wengine kutofanya vizuri darasani?

Jibu: Kweli kuna watoto, wanatoroka shuleni na kufeli mitihani na wazazi wakiambiwa hawasemi chochote yaani hawashirikiani na walimu, mzazi kama huyo inafaa akamatwe kwa sababu anasabotage (anahujumu) nguvu kazi ya serikali katika elimu, mwisho mtoto anakuwa panya rodi.

Swali: Vipi kuhusu ukusanyaji wa mapato katika wilaya yako, unakwenda vizuri?

Jibu: Unakwenda vizuri japokuwa hivi sasa kodi za majengo zipo chini ya TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania). Lengo ni kukusanya shilingi bilioni 85 kwa mwaka. Changamoto ni nyingi na tunataka wafanyabiasha, kwa mfano wa samaki na urembo wawe nao wakilipa ushuru wa serikali, kuna biashara za siri nyingi zenye fedha nyingi zinafanyika kama vile nyumba, samaki urembo na kadhalika, wataalamu wangu wako mitaani kuangalia biashara hizo, si kwa nia ya kuonea mtu. Wito wangu ni kwamba watu walipe kodi ili tuhudumie jamii tumsaidie Rais Dk John Magufuli na tuungane na serikali yake katika kujenga nchi yetu.

Mwandishi: Asante sana kwa muda wako.

Jibu: Karibuni tena.

Comments are closed.