The House of Favourite Newspapers

Mitandao ya Kijamii Inavyoweza Kutibua Mapenzi

NI Ijumaa nyingine ninapokukaribisha mpenzi msomaji wa kona hii nzuri, mahali tunapoelekezana mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi. Leo napenda tujadiliane kuhusu mada hii kama inavyojieleza hapo juu.

Sayansi na teknolojia vinaifanya dunia iende kasi sana, mfumo wa maisha unabadilika haraka kuliko wakati mwingine wowote, dunia sasa inaunganishwa na kuwa kama kijiji kutokana na matumizi ya intaneti na mitandao ya kijamii.

Pia watu wengi wanamiliki vifaa mbalimbali vinavyowawezesha kuwa na mawasiliano ya intaneti muda wote, zikiwemo laptop na simu za kisasa (smart phones).

Hata wale watu ambao kwa kipindi kirefu walikuwa wakisikiasikia tu kuhusu mitandao ya kijamii, hivi sasa wanaweza kutumia Facebook, Instagram, Whatsapp, Twitter, Skype, Tango na mitandao mingine kibao ya kijamii. Hata hivyo, kuna usemi usemao ‘maendeleo huja na mambo leo’.

Ni jambo jema mtu kuwa na mawasiliano ya uhakika muda wote, kuelewa dunia inakwendaje, kubadilishana mawazo na ndugu, jamaa na marafiki hata wale
ambao wako mbali kabisa lakini je, ni wangapi wanajua matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii? Katika siku za hivi karibuni, mitandao ya kijamii imekuwa sawa na ‘saratani ya mapenzi ’ kwa watu waliopo kwenye uhusiano.

Ndoa nyingi zinavunjika, wachumba wanaachana, wapenzi wanagombana na baadaye kuachana kwa visa, chanzo kikiwa ni mitandao ya kijamii.

NINI CHANZO? Walioanzisha mitandao ya kijamii hawakuwa na lengo baya lakini watumiaji wengi, hasa wa nchi za ulimwengu wa tatu, ikiwemo Tanzania, wanashindwa kuelewa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na matokeo yake, inakuwa chanzo cha matatizo mengi katika jamii.

Ipo mifano mingi ya watu waliowapiga picha za utupu wenzi wao kipindi wakiwa kwenye mapenzi motomoto lakini ilipotokea wakahitilafiana kidogo, waliziposti picha hizo kwenye mitandao ya kijamii na kuwasababishia wenzao matatizo makubwa ya kisaikolojia na aibu isiyofutika.

Upo pia ushahidi wa kutosha wa watu ambao kwa kushindwa kuziheshimu ndoa au uhusiano wao wa kimapenzi, walijikuta wakiitumia mitandao ya kijamii kutongozana, kutumiana picha za ngono na mwisho wakaishia kuwasaliti wenzi wao.

Wapo pia ambao wanaiingilia (hacking) mitandao ya wenzi wao na kuanza kuposti ujumbe na picha za ajabu, ukiuliza kisa eti kwa sababu wamegombana.

Wapo pia wanaoshinda kutwa nzima kwenye mitandao ya kijamii wakiwatusi wapenzi wao wa zamani na kuposti picha za kudhalilisha. Je, haya ndiyo matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii?

MFANO HALISI

Mwanahawa wa Buguruni, alinipigia simu huku akilia akihitaji ushauri wa kitaalamu. Alinieleza kwamba alikuwa kwenye uhusiano wa muda mrefu na mwanaume mmoja ambaye walikutana chuoni wakiwa wanasoma.

“Hivi karibuni tulikorofishana naye baada ya mimi kugundua kuwa ana mwanamke mwingine, nikawa sitaki kuendelea kuwa na uhusiano naye mpaka amuache huyo mwanamke.

“Cha ajabu alianza kunitishia kwamba nikimuacha atanifanyia kitu kibaya sana, sikujali, nikaamua kushikilia msimamo wangu. Hivi karibuni nikashangaa kuona anaanza kuposti Facebook, Instagram na Twitter picha zangu kibao za utupu tulizokuwa tunapigana kipindi cha mapenzi yetu.

Nina siku ya nne leo sitoki nje, naona aibu natamani hata kujiua. Naomba msaada wako,” alihitimisha dada Mwanahawa. Kama wewe ungepewa nafasi ya kumshauri, ungemwambia nini? Nitumie ujumbe wako kwa namba za hapo juu. Tukutane wiki ijayo kwa mwendelezo wa mada hii.

Comments are closed.