The House of Favourite Newspapers

Hiki Ndicho Kinachowatisha Wanaume

HALOHALO mashostito kokote mlipo, asalam aleykum. Mnaendeleaje na kazi za kila siku jamani, maana maisha yameshakuwa magumu, kila mtu analia ooh Magufuli kabana, Magufuli kabana, sasa sijui kabana wapi! Hivi sasa hata wanaume nao wameweka kisingizio, ukimuomba hela, anakuambia eti Magu kabana, kabana kwani wewe una kazi yako na mshahara ni uleule amebana nini, hulipwi mshahara kwani? Basi mwaya, tuachane na hayo, turudi kwenye mada yetu niliyowaandalia leo, maana wanasema kata mti, panda mti, ndiyo mwendo wa kisasa.

Juzi kama kawa, nilikuwa barazani kwangu nimejituliza na wadada wengi wamenizunguka, kungwi namwaga somo. Sasa katika hali ambayo sikuitarajia, mama Snura, akachomboze kuwa bintiye shoga’ke mmoja, karudishwa kutoka kwa mumewe, mwezi mmoja tu tangu aanze kuishi naye kinyumba. Maana ukweli hajaolewa, lakini wameamua kuanza kuishi kama mume na mke na wazazi wa pande zote wameridhia.

Sasa shoga huyo kakaa mwezi mmoja tu, karudishwa. Nini kisa? Mwanaume amekwenda kwa wazazi wa mkewe kulalamika, kuwa eti mwanamke amebadilika sana siku hizi, amekuwa ndiye kichwa cha familia, kila jambo aelekeze yeye, anachotaka yeye ndicho kifanywe na asichotaka kisitokee.

Mwanaume kasema siwezi, mimi ndiyo mwanaume, ninachoamua mimi ndicho kiwe hivyo, tangu lini mwanamke ampangie? Kisa ndiyo hicho shosti! Sasa aliponiambia vile ndiyo nikajua kumbe haya mambo bado yanaendelea, maana sisi tuliopitia kwa makungwi tunajua nini cha kufanya ukishawekwa ndani na mwanaume.

Iko hivi, wanawake wengi wakiwa katika uhusiano wa kimapenzi na wanaume, huficha tabia zao za asili, kama wana roho mbaya, watajifanya ni wakarimu, kama ni wakali watajionyesha kuwa wao ni wapole, yaani kifupi ni kwamba hawaonyeshi rangi yao halisi wakati wa urafiki au uchumba, kwa sababu gani unajua? Kwa sababu wanataka wanaume wawaone wanafaa, wife material!

Tatizo linakuja pale wanapofanikiwa kuwekwa ndani, ndipo napo tabia inabadilika mara moja. Kwa kuwa wamo ndani, watataka sasa kuwa wao ndiyo wao, ratiba za maisha ya kila siku wanapanga wao, muda wa mume kurudi nyumbani wanapanga wao, siku za wenyewe kwenda saluni wanapanga wao na vitu vingine chungu nzima. Kwanza niwaambie, hakuna mwanaume anayependa kupangiwa muda wa kurudi nyumbani na mkewe.

Wee muache ajipangie mwenyewe, utamuona saa kumi na mbili kafika, au saa moja, au hata mbili. Ukishaanza kutaka muda unataka wewe, ndiyo unamchochea kuchelewa ati. Kitu cha msingi nilitaka kuwafahamisha akina dada wachanga katika uhusiano wao ni kuwa vile wanavyoishi hivi sasa wakiwa na wapenzi wao, basi tabia hizo ziendelee baada ya kuwekwa ndani.

Usije kumshangaza mwenza wako akaanza kujiuliza, mbona zamani hakuwa hivi? Utamfanya ajue kumbe tabia zako zote za zamani zilikuwa ni feki.

Comments are closed.