The House of Favourite Newspapers

Mwanamke Kutofanikiwa Kupata Ujauzito ‘Female Sterility’

TATIZO hili humfanya mwanamke asifanikiwe kupata ujauzito kwa  wakati anaopenda au asiweze kabisa kupata ujauzito. Kutofanikiwa kupata ujauzito kwa wakati aliopanga huwatokea wanawake wengi ambapo huwa hawana tatizo lolote kiafya au katika viungo vyao vya uzazi na siku za hedhi wanapata kama kawaida.

Wanawake hawa pia hulalamika kufanya tendo la ndoa katika kipindi cha kupata mimba lakini hawapati. Wengine huwachukuwa  muda mrefu bila  hata ya kufanya uchunguzi  au matibabu yoyote na kujikuta wanafanikiwa, hawa utaona wana muda mrefu tangu waanze kutafuta mtoto wa kwanza au wa pili na wanasema  huwa hawatumii kinga yoyote kuzuia mimba.

Wengine hujikuta wanashika mimba katika umri mkubwa. Katika kundi la pili ni wale ambao hawawezi kabisa kupata ujauzito kutokana na sababu mbalimbali aidha kwa upande wao au kwa upande wa wanaume zao.

Sababu hizi zinaweza kuwa katika viungo vya uzazi au mfumo wa homoni. Sababu kwa mwanamke tunaiita ’female  factors’ na sababu kwa mwanaume zinaitwa ’male factors’. Mojawapo ya sababu za kutopata ujauzito kwa mwanamke ni kutopata hedhi, maumivu ya hedhi na kuvurugika kwa hedhi.

Nyingine ni kutopevusha mayai ambapo mwanamke hapati ute wa uzazi, kupoteza hamu na raha ya tendo la ndoa, maumivu ukeni, kutokwa na uchafu na muwasho ukeni.

Kuumwa na tumbo mara kwa mara chini ya kitovu pia ni sababu. Sababu kwa mwanaume ni kama vile kutokuwa na mbegu za uzazi, maumivu ya korodani, kutokuwa na korodani, maumivu katika njia ya mkojo, upungufu wa nguvu za kiume na kuwahi kumaliza tendo la ndoa.

CHANZO CHA TATIZO

Vyanzo vya tatizo hili vipo vikubwa vitatu,  kwanza ni tatizo litokanalo na magonjwa mbalilmbali ambapo huathiri mfumo wa uzazi wa mwanaume na mwanamke ‘pathologic’. Mfano magonjwa ya zinaa kama kisonono, kifua kikuu, kansa, utoaji wa mimba na uvimbe wa kizazi.

Pili ni matatizo katika mfumo wa homoni unaoendesha uzalishaji mbegu kwa mwanaume, nguvu za kiume na kwa mwanamke homoni huendesha mzunguko wa hedhi,  uzalishaji na upevushaji wa mayai. Tatu ni matatizo ya kisaikolojia ambayo huambatana na upungufu au ukosefu wa nguvu za kiume, kukosa raha ya tendo la ndoa kwa mwanamke na kupata maumivu wakati wa tendo. Watu wenye matatizo haya mwanaume atakwambia huwa hana kabisa hamu na wala hata uume wake huwa hausimami hasa asubuhi anapoamka  ‘morning erection. Mwanamke naye  atalalamika kupoteza hamu na raha ya tendo la ndoa huku akipoteza majimaji ya ukeni na hata akiandaliwa vipi huwa hajisikii.

Matatizo haya yote huwa yanaenda sambamba, moja huweza kuzusha jingine. Wanawake wote walio katika umri wa kuzaa wanaweza kupata tatizo hili la kutopata ujauzito endapo amepitia mojawapo ya vyanzo hivyo au sababu zinazohusiana na ugonjwa.

UCHUNGUZI

Uchunguzi wa tatizo hili hufanyika katika kliniki za magonjwa ya akina mama kwenye hospitali za mikoa ambapo vipimo mbalimbali kama vya  damu, Ultrasound na vingine ambavyo daktari ataona vinafaa vitafanyika.

TIBA NA USHAURI

Baada ya uchunguzi wa kina, daktari atapanga juu ya aina ya matibabu. Zingatia ushauri wa kitaalamu.

 

Comments are closed.