The House of Favourite Newspapers

Unayeitamani Ndoa , Mume Bora Anapaswa Kuwa Hivi 2

Na HASHIM AZIZ| GAZETI LA IJUMAA| LETS TALK ABOUT LOVE

UHALI gani msomaji wangu, ni matumaini yangu kwamba uko poa na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku. Ni Jumatatu nyingine ninapokukaribisha kwenye ukurasa huu kujadili na kuelimishana mambo mbalimbali yanayohusu uhusiano wa kimapenzi.

Wiki iliyopita tulianza kujadili mada inayojieleza hapo juu ya sifa na vigezo anavyotakiwa kuwa navyo mwanaume bora. Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitakushukuru wewe msomaji wangu uliyechangia mawazo yako kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS) kuhusu mada hii.

Leo tunaendelea na sehemu ya pili ya mada yetu. Je, mwanaume bora anapaswa kuwa na sifa gani? Vipo vigezo vingi vinavyoweza kumfanya mwanaume akawa bora. Achana na sifa za nje kama fedha, magari, nyumba au mwili mkubwa.

Sifa za ndani ndiyo zinazotoa tafsiri sahihi ya jinsi mwanaume alivyo bora. Watu wengi wanadanganyika na sifa za nje na kama nilivyoeleza wiki iliyopita, wanaume nao wanajua namna ya kuishi maisha feki ili kuwanasa kwa urahisi wanawake wanaotazama zaidi sifa za nje.

MFANO HALISI

Msomaji wangu mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake, alinitumia meseji na kunieleza jambo ambalo ningependa kukushirikisha msomaji wangu. Aliandika hivi:

Sms liandika hivi: “Ni makosa makubwa kumtathmini mwanaume kwa kutumia sifa za nje, mimi mwenyewe imenitokea. Kuna mwanaume alinitongoza, siku ya kwanza tu alikuja na gari. Akawa ananionesha kwamba anaishi maisha ya hali ya juu sana, akawa ananipa pesa nyingi, ananipeleka kwenye hoteli kubwakubwa, kila siku anabadilisha magari mpaka nikajikuta naingia kichwakichwa. Yaani alinidanganya vitu vingi sana, mpaka nyumba ya kuishi alinipeleka kwa rafiki yake, nyumba nzuri ina kila kitu ndani. Tukaenda hivyo kwa kipindi kirefu mpaka nikajikuta nimepata ujauzito wake, hapo ndiyo nilipoanza kuufahamu ukweli. Kumbe alikuwa tapeli tu, hakuwa na kazi yoyote, hakuwa na gari wala nyumba na hata pesa kumbe alikuwa anakopa. Niliumia sana kuufahamu ukweli lakini sikuwa na jinsi, tayari mimba ilishakua kubwa. Mpaka ninapozungumza haya, tayari nilishaachana naye lakini kanizalisha watoto mapacha nahangaika nao. Msomaji huyu ni miongoni mwa wanawake wengi ambao hulaghaiwa na wanaume na kujikuta wakiingia kwenye mtego hatari.

CHA KUJIFUNZA

Kama wasomaji wangu wengi walivyochangia, sifa za mwanaume bora ni nyingi. Awe ni mwanaume anayejitambua, hilo ndiyo kubwa. Lazima afahamu wajibu wake ni upi, awe na uwezo wa kuwajibika ndani ya familia, ajue namna ya kumtunza mke na watoto, awe mkweli, anayejiheshimu na kuwaheshimu wengine, mwenye busara, upendo wa dhati, mwenye huruma kwa mkewe na familia yake na kubwa zaidi awe na hofu ya Mungu.

Sifa na vigezo ni vingi lakini kama nilivyosema awali, ni makosa kudanganyika na sifa za nje. Ili kumfahamu mwanaume bora ni lazima upate kwanza muda wa kumsoma na kumuelewa ili hata unapoamua kuingia kwenye ndoa, unakuwa na uhakika na mtu unayeanzisha naye uhusiano. Tukutane wiki ijayo kwa mada  nyingine nzuri. Kwa maoni, ushauri, nicheki kwa namba za hapo juu.

 

Comments are closed.