Na HASHIM AZIZ|CHAMPIONI IJUMAA| MAKALA
KARIBU kwenye uwanja huu mzuri mpendwa msomaji wangu, ni Ijumaa nyingine tunapokutana, ni wajibu wetu kumshukuru Mungu kwa kutufanya tuione siku hii nzuri ya leo.
Sote ni mashahidi kwamba siku hizi, tofauti na miaka ya nyuma, kunafanyika harusi za kifahari sana. Miaka ya nyuma, baada ya wawili kupendana na kukubaliana kuoana, mipango ilikuwa inafanyika, wazazi wanataarifiwa na baadaye harusi inafanyika ambapo hakukuwa na mbwembwe nyingi.
Watu mtakula pilau na soda sehemu inapofanyikia harusi halafu shughuli inakuwa imeishia hapo. Siku hizi mambo ni tofauti, wawili wakipendana, hata kabla ya siku yenyewe ya harusi unakuta tayari zimeshafanyika sherehe nyingine ndogondogo mbili au tatu.
Mara utasikia usiku wa zawadi, mara ‘kitchen party’, mara nini sijui! Bado siku ya harusi yenyewe, watu wataanzia kanisani au msikitini (kama ni ndoa za kidini) halafu jioni inahamia ukumbini, watu wanakaa mpaka usiku wa manane, wakila, kunywa hadi kusaza.
Si hayo tu, bado wakitoka hapo, maharusi wengi hupenda kwenda kula fungate kwenye hoteli za kifahari kwa kipindi kirefu! Bila shaka msomaji wangu kama nawe si mmoja kati ya waliofunga au wanaotarajia kufunga ndoa za namna hii, lazima yupo au wapo ambao umeshuhudia wakifunga ndoa za namna hii.
Hoja yangu hapa siyo kujadili kuhusu gharama zinazotumika au umashuhuri unaoonyeshwa kwenye ndoa za kifahari ambazo siku hizi zimekuwa fasheni.
Ndoa ni jambo la heri na kama unayo nafasi ya kufanya sherehe kubwa kila mmoja akafurahi, hakuna tatizo ingawa pia si dhambi kufanya mambo kwa kadiri Mungu alivyokujalia, yaani kutolazimisha kufanya mambo makubwa wakati huna uwezo nayo.
Ninachotaka tujadiliane hapa, inakuwaje watu mnatumia gharama kubwa kiasi hicho, kufanya sherehe zinazogharimu mamilioni ya fedha halafu muda mfupi tu baada ya ndoa kufungwa, migogoro mikubwa inaanza kuibuka ndani ya ndoa na mwisho wa siku, mnaachana mkiwa mmeishi pamoja kwa muda mfupi tu?
Hujawahi kuona watu waliofunga ndoa ya kukata na shoka wakiachana baada ya miaka mitatu, au miwili huku wengine wakishindwa hata kufikisha mwaka mmoja?
Hujawahi kuona watu Mapenzi & Uhusiano Harusi ya kifahari, baadaye mnaachana, nini kinasababisha? waliofunga ndoa za kifahari, maisha yao ya kimapenzi yakitawaliwa na migogoro isiyofika mwisho? Lakini hapohapo tujiulize, kwa nini wazee wetu ambao kipindi hicho hawakuwa na mbwembwe kwenye ndoa zao, wanaweza kuishi pamoja kwa wengine mpaka zaidi ya miaka hamsini hadi kifo kinapowatenganisha?
Wao walikuwa na kitu gani cha ziada ambacho vijana wa leo hawana? Msomaji wangu, unafikiri ni nini hasa kifanyike ili ndoa za vijana zitadumu kama ilivyokuwa zamani? Mimi siyo mjuaji wa kila jambo, naamini wewe pia unayo mawazo au mchango wako katika hili.
Nakukaribisha kwa moyo mkunjufu, nitumie mawazo yako, tujadiliane halafu wiki ijayo, tutaendelea na sehemu ya pili ya mada yetu. Tuma maoni yako kwa meseji za kawaida au Whatsapp kwa namba 0719 401 968
Comments are closed.