The House of Favourite Newspapers

Muache Achague Mwenye Kumpa Raha!

Na GABRIEL NG`OSHA| IJUMAA WIKIENDA| MAKALA

NI Jumatatu nyingine yenye kila neema machoni pa Mungu, zipo changamoto za hapa na pale zinazokukabili msomaji wangu wa XXLove, lakini nikutie moyo tu kuwa kamwe usithubutu kukata tamaa, hayo ndiyo maisha.

Amini tu! Bila shaka kila mzazi anapenda au anatamani mwanaye aangukie mikononi mwa mpenzi mwenye sifa anazotaka yeye. Kwa mfano, anatamani mwanaye kipenzi awe wa kike au wa kiume apate mpenzi mwenye elimu, fedha, mali na kadhalika.

Kama ni suala la kutoa mapendekezo kwa mwanao siyo jambo baya lakini ni lazima ujue kuwa hata mwanao naye ana chaguo lake. Hivyo ni vyema yeye ndiye ukampa nafasi ya kumchagua mtu wa kumpa raha katika maisha yake.

Katika makala haya ngoja nijikite zaidi kwa wazazi wenzangu, maana hata mimi nina mtoto anayeweza kuoa au kuolewa muda ukiwadia.

Wazazi wamekuwa na tabia ya kulazimisha kijana au binti yao aoe au aolewe na f’lani kwa sababu ya kitu f’lani. Hii si sawa, huko ni kumnyima mtoto haki yake ya msingi, labda kama ameridhia au kaomba mzazi umsaidie kumtafutia, jambo ambalo nalo pia si sahihi.

Lakini si kwa matakwa yako au kumlazimisha, hii ni hatari sana hasa kwa karne hii ya sayansi na teknolojia. Kama kweli raha jipe mwenyewe, basi muache mwanao amchague mwenyewe wa kumpa raha na siyo kumchagulia.

Maana ukimchagulia, akienda huko yakamshinda, lazima ujue lawama zote atazielekeza kwako. Kila akikorofishana na mwenza wake, ataanza kulia na kulaumu kama kuwa isingekuwa wewe kumchagulia mwanamke au mwanaume wa kumuoa, basi asingekuwa anapata mateso kama anayopata katika kipindi husika atakachokuwanacho.

Kusema kweli, suala hili la kuchaguliwa mwanaume au mwanamke wa kuoa linazitesa ndoa nyingi kwa sasa, linawatesa watoto wetu kama ulikuwa hujui kadiri zinavyozidi kusonga mbele, suala la harusi au ndoa linaonekana kupungua siku baada ya siku, vijana wa kike na wa kiume ni mara chache sana kufikia hatua ya kuoana kama zamani zaidi ya kufanya uasherati.

Hivi kama mwanao amerukaruka huku na kule, kijiji kizima anajulikana kwa mawenge yake, leo amepata mchumba wa kumuoa au kuolea naye, una sababu zipi za kumkataa mchumba wake na kutaka aolewe au amuoe unayemtaka wewe? Ingawa unaweza ukachaguliwa na ukabahatika kumpata mwenza mwenye upendo na mapenzi ya dhati, lakini katika kipindi tulichonacho ni heri kila mtu akabeba msalaba wake.

Labda kama mwanao atapenda kukushirikisha katika hatua ya kumpata anayemtaka kwa ajili ya kumpa raha. Mpenzimsomaji, kwa ushauri na maoni, tembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Ijumaa Wikienda, Insta:@mimi_ na_uhusiano au jiunge na Group la M&U la WhatsApp +255 679 979 785

Comments are closed.