Harmonize Sikio Halizidi Kichwa, Chunga Sana
Na ERIC EVARIST| RISASI MCHANGANYIKO| BARUA NZITO
MOJA kati ya jambo ambalo linawashinda watu wengi ni kubaki na nidhamu pindi wanapopata mafanikio. Wengi wamejikuta wakiwa wajeuri. Watoa lugha chafu, wagomvi, walevi na tabia nyingine nyingi mbaya baada tu ya kufanikiwa.
Nimeguswa leo kukuandikia barua, Harmonize unayewakilisha Kruu la Wasafi Baby (WCB) lililo chini ya uongozi mzima wa bosi wenu Diamond Platnumz. Harmonize ndugu yangu, dhumuni la kukuandikia barua hii ni kutaka kukuambia kwamba, tazama mwenendo wako kwani umri wako bado mdogo, nidhamu inahitajika zaidi ili uweze kufika mbali.
Kaka yako Diamond ambaye wewe unamhusudu kama taa ya mafanikio yako, alijitahidi sana kutanguliza nidhamu alipokuwa kwenye nafasi kama uliyonayo. Hakuanza kuonesha cheche zake akiwa angali bado anahitaji msaada. Wewe naona umeanza mapema.
Kitendo chako cha kukataa kukutana na msanii mwenzako Harmorapa, ulichokifanya wiki iliyopita pale East Africa TV hakikuwa cha kiungwana. Umeonesha dharau ya hali ya juu. Waandaaji wa kipindi walishakupanga kwenye ratiba, waliamini utakuwepo lakini kwa masikitiko makubwa, ukaona tu uondoke eti baada ya kusikia Harmorapa amefika eneo hilo.
Kinachokufanya umuone Harmorapa kama vile si binadamu ni nini hasa? Unakosa hata tu ubinadamu wa kawaida na kuona yule naye ameumbwa na Mungu? Kwani ungeenda nini kingetokea? Yule si ni Mtanzania kama wewe? Si anaanza muziki kama wewe ulivyoanza, kiburi cha kumdharau kinatoka wapi? Diamond ndivyo alivyokufundisha hivyo?
Hata kama amekufundisha hivyo, unapaswa kujiongeza maana mwenzako tayari ameshafika levo nyingine, wewe bado una safari ndefu sana ya kuelekea kwenye kilele cha mafanikio. Usivimbe, huna sababu ya kuvimba maana jina lenyewe ndiyo kwanza linachipukia, dunia duara na wa mwisho anaweza kuwa wa kwanza.
Katika kipindi hikihiki ambacho wewe unaonesha dalili za kuchomoza, unaweza kupitwa na Harmorapa na ukajikuta unajuta. Hivi ujasiri wa kumnyooshea kidole chenye ishara ya tusi, meneja wa Harmorapa umeutoa wapi? Unajiona upo kwenye uongozi mkubwa kiasi cha kuona uongozi mwingine wowote Bongo hauna maana? Jiheshimu, huyuhuyu meneja wa Harmorapa uliyemtusi, anaweza kukustiri kesho na kesho kutwa.
Anaweza kukustiri maana hakuna anayeijua kesho. Fumba na kufumbua umetemwa hapo WCB, huwezi kuomba msaada kwa meneja wa Harmorapa? Shauri yako, haya ni maisha tu. Nakushauri, katika dunia ya sasa hakuna sababu ya kumchukia mtu.
Kuna leo na kesho, wewe bado kijana mdogo hupaswi kuongeza idadi ya maadui. Umewaonesha dharau East Africa TV, wanaweza kukuweka kando katika suala zima la kutangaza muziki wako, unafikiri umevimba kichwa sana kiasi cha kutohitaji msaada wao? Badilika kijana.
Kama unataka kwenda vizuri, nenda kawaombe radhi East Africa, muombe radhi meneja wa Harmorapa na nina hakika wanaweza kukuelewa ukaanza upya. Ukijifanya ‘bandidu’, endelea na siku yakikuta ndipo utatia akili. Mimi nikutakie kila la kheri katika safari yako ya kimuziki, nikusihi tena acha jeuri, badilika! Mimi ni kaka yako; Erick Evarist
Comments are closed.