Heh! Kumbe kuna Harmonize!

Harmonize.

Na BONIPHACE NGUMIJE| GAZETI LA AMANI| HABARI

NI nadra sana kwa sasa kama utatembelea kwenye mitandao ya kijamii usikutane na jina la Harmorapa akizungumziwa kwa ishu yoyote ile, iwe kwa kupondwa, kusifiwa na hata kusanifiwa, yeye kila kitu ni sawa tu ilimradi atimize ndoto zake. Harmorapa ambaye hana hata mwaka mmoja kwenye gemu la muziki, asiye na hit songs hata mbili tu kwenye tasnia hiyo, lakini ni mmoja wa wasanii ambao wanazungumziwa zaidi kwenye mitandao kuliko hata Darassa mwenye zaidi ya miaka kumi kwenye gemu, Fid Q au Joh Makini. Kila kona ni Harmorapa.

Harmonize.

Upepo alionao si wa mchezomchezo, hakuna anayemzungumzia Harmonize tena pamoja na kumpa umaarufu kijana huyu wa Kimakua kutoka Masasi, Mtwara kutokana na kufanana kwao, ingawa Harmonize hakubaliani na hilo! Inawezekana Harmonize anaamini kama alivyosema Dancer wa Diamond Platnumz, Moses Iyobo kuwa Harmorapa hafanani naye bali anafanana na nyani huku chuki dhidi yake akiionesha waziwazi.

Hamorapa.

Kuhusu Harmonize kwa sasa hadi ukutane na habari zake ndiyo unashtuka; “Heh! Kumbe kuna Harmonize!” Kila mtu anamzungumzia Harmorapa tu.

Harmorapa ambaye kimuziki bado anajikongoja kutokana na uwezo wake lakini inaonekana uongozi wake ni mzuri katika suala zima la kumtengezea kiki. Kimchezomchezo anazidi kutengeneza vichwa vya habari kila kukicha bila kujali ametengeneza kwa kudhihakiwa, kulia, kupiga magoti, kutukanwa na mambo mengine mengi lakini mwisho wa siku ni yeye kufahamika.

Kwa mambo yanavyoenda si ajabu kusikia Harmonize amesahaulika kabisa kama Harmorapa ataendelea kukua kama ilivyo sasa. Ni ukweli kuwa wakati ‘dogo’ huyo alipoanza kuchomoza na kupata kiki kwenye midia mbalimbali, baadhi ya watu walikuwa wanamuhesabia siku za kupotea, wengine wakampa wiki kadhaa, wengine miezi lakini upepo umekuwa tofauti na mitazamo ya wengi na sasa Harmorapa anazidi kupaa tu.

Nyota ya kinda huyo inaonekana kung’ara kila kukicha, hivi karibuni ‘alimeki headline’  kwenye mitandao na vyombo vingine vya habari kufuatia kitendo chake cha kutimua mbio baada ya kuona ‘mdomo wa bata’ (bastola) aliyotolewa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye.

Baada ya Harmorapa kutimua vumbi kwenye sakata la Nape, vibonzo, magazeti na video mbalimbali zilisambaa mitandaoni jambo lililosababisha kinda huyo kupewa Ubalozi wa Kinywaji cha Swala huku akipata mashavu ya shoo kadhaa ikiwemo ya kukata na shoka ya Dar Live kwenye Usiku wa Pasaka. Katika nukuu zake, Fid Q aliwahi kusema kuwa mafanikio hufuata kile unachofanya. Hilo linajidhihirisha kwa Harmorapa, mafanikio yake yanatokana na juhudi zake pamoja na kujitoa ufahamu katika kila jambo ambalo haijalishi litaacha gumzo kwa kupondwa au kusifiwa na watu.

Mbali na kutafuta mafanikio kwa njia yake ya vituko, kimuziki pia rapa huyo anaonesha mabadiliko na kukua, hasa kwenye kibao chake cha Kiboko ya Mabishoo alichomshirikisha Juma Nature. Wimbo huo umepiga hatua kubwa kwa kuanza kuchezwa kwenye kituo kikubwa cha Runinga cha MTV Base.

Ushauri kwa Harmonize ni vyema akawekeza nguvu nyingi kwenye kazi zake, hana sababu ya kuonyesha chuki kwa Harmorapa kwa sababu hawezi kuzuia mafanikio yake! Hivi tatizo liko wapi Harmorapa kufanana na Harmonize? Mbona kuna vijana wengi wameibuka na kudai wanafanana na bosi wake, Diamond Platnumz?

Kwani Harmonize ni mtu wa kwanza kufananishwa na mtu? Ni wakati wa kufanya kazi, Harmonize asipoangalia atazidi kupotea na kushindwa kuelewa ni wapi alipoteleza, huku akimshuhudia huyo ‘nyani’ akizidi kupanda kwenye matawi ya juu ya mti wa mafanikio.

 

Toa comment