The House of Favourite Newspapers

Maumivu Chini ya Kitovu kwa Wanawake na Wanaume

MAUMIVU chini ya kitovu kwa wanawake na wanaume kitaalamu huitwa lower abdominal pain ni tatizo ambalo huwakumba watu wengi lakini kwa bahati mbaya wengi hulichukulia kuwa ni jambo la kawaida kitu ambacho baadaye husababisha wagonjwa kuingia kwenye matatizo makubwa ya kiafya hasa kwenye mfumo wa uzazi na mfumo wa chakula.

Maumivu chini ya kitovu yapo yale ya chini yake, katikati, kushoto na kulia. Kwa wanawake maumivu ya kushoto na kulia yapo ya aina mbili. Kuna yale ambayo yanakuwa upande mmoja lakini husambaa kwa urefu wa sentimita mpaka nne na inaweza ikawa upande mmoja au pande zote mbili lakini yapo mengine chini ya kitovu ambayo yanaweza yakawa upande mmoja au pande zote mbili bila kusambaa kwa marefu.

Kuna maumivu mengine chini ya kitovu huwapata wanawake wakati tu wanaposhiriki tendo la ndoa kwa ndani ya uke au chini ya kitovu. Pia yapo ambayo huwapata wanawake wakati wameinama, wakati wa kunyanyua vitu vizito, wakati wa kucheka au kuimba na wakati mwingine wakiwa wamelala kifudifudi.

Maumivu chini ya kitovu yanaashiria matatizo  kwa wanawake kama vile mirija ya uzazi kujaa maji mazito na machafu ambayo huzuia yai kutembea kwenye mirija ya uzazi.

Mwanamke ambaye amewahi kuambiwa na daktari kwamba anatakiwa asafishwe kizazi chake/mirija ya uzazi na wakati huo huo anasikia maumivu chini ya kitovu kushoto na kulia au upande mmoja kuna uwezekano akawa na tatizo la mirija ya uzazi kuziba kutokana na kujaa maji machafu. Lakini pia maumivu hayo yanaashiria kutokukomaa kwa mayai ya uzazi. Hii husababisha vifuko vya mayai ya uzazi kuvimba ovaritis na kumletea mwanamke maumivu chini ya kitovu mithili ya kichomi.

Mwanamke ambaye ana maumivu chini ya kitovu na wakati huo huo ana matatizo ya hedhi kukoma au kutokuwa na mpangilio maalum kuna uwezekano mkubwa akawa na tatizo la vifuko vyake vya mayai ya uzazi kutokomaza mayai na hivyo mayai kutotoka kwenye vifuko hivyo na kusababisha kuvimba na hatimaye kumsababishia mwanamke maumivu makali au kitu kama kichomi.

Pia humsababishia kuvimba kwa kuta za mji wa mimba na kuta za mirija ya uzazi yaani Pelvic Inflamatory Disease (PID). Mwanamke anayesikia maumivu chini ya kitovu katikati na pembeni lakini pia akawa anatokwa na uchafu mzito mithili ya maziwa mtindi kuna uwezekano akawa na PID hasa kama amewahi kukumbwa na tatizo la kuharibika kwa mimba kabla haijafikisha miezi mitano.

Ieleweke kuwa maumivu chini ya kitovu yanayohusisha afya mbovu ya kibofu cha mkojo huambatana na mgonjwa kutoa haja ndogo kidogo sana ila mara kwa mara. Maumivu chini ya kitovu kwa wanaume huashiria pia tatizo la tezi dume liitwalo prostatitis yaani kuvimba kwa tezi dume.

Maumivu haya hujikita kwenye shina la uume na huashiria tatizo hili  hasa kama mwanaume anakwenda haja ndogo mara kwa mara nyakati za usiku na umri ukiwa unaelekea miaka 50 au zaidi. Dalili nyingine ambatano ni kutoa haja ndogo ambayo ina kasi ndogo sana tofauti na kawaida, ikiambatana na maumivu ya kiuno na mgongo, kuvimba kwa korodani, haja ndogo inayoambatana na usaha na damu, maumivu ya uume wakati wa kufika kileleni na  damu katika maji ya uzazi semen.

Kwa wanaume, maumivu haya ya chini ya kitovu huashiria pia tatizo ambalo kitaalamu hujulikana kwa jina la hernia ambapo waswahili tunaita ngiri. Mwanaume anaposikia maumivu haya ya chini ya kitovu ikiambatana na maumivu ya korodani, korodani moja kupungua na nyingine kukua zaidi au zote mbili kukua au kupotea ni dalili ya ugonjwa huu ambao huharibu ubora wa uzalishwaji wa mbegu za kiume ambazo zaweza kuzalishwa chache au ambazo hazina kasi ya kutosha kusafiri kwenye via vya uzazi vya mwanamke na hivyo mwanaume kupoteza uwezo wake wa kutungisha mimba.

Maumivu chini ya kitovu kwa wanaume kama ilivyo kwa wanawake huashiria tatizo la maambukizi katika mfumo wa haja ndogo yaani Urinary Track Infection (UTI) ambapo dalili zake ni kama zile za mwanamke hapo juu.

HITIMISHO.

Vipimo na tiba vyahitajika mapema bila kuchelewa ili kuepuka madhara makubwa katika mfumo wa uzazi, mkojo na hata wa chakula

Comments are closed.