Na MWANDISHI WETU| RISASI MCHANGANYIKO| MAKALA
HALOOOOO mashosti, mnajisikiaje? Mie kidogo sijaamka vizuri leo na ndiyo sijatoka kabisaa, nimepaki zangu ndani na hivi mvua zinanyesha leo, ndiyo kabisa sitoki.
Ila kwa kuwa nimeshayavulia maji nguo, sina budi kuyaoga. Leo nitawaletea mada mpya, ambayo kila mmoja itamhusu! Wengi mmekuwa mnajiuliza jinsi ya kuweza kumtambua mwanaume ambaye hasa ndiye anayekufaa katika maisha yako, maana nyie watoto wa dotcom mna mambo yenu mnatazama, wengine wakitaka wanaume wa kuwatoa out, wengine wakitaka wenye kuwapa hela, wengine wanaojua zaidi pale sita kwa sita na vitu chungu nzima.
Kuna baadhi ya vitu vya msingi mtu ukiwa katika mapenzi lazima uvipate best, asikudanganye mtu. Kwanza katika mapenzi mtu lazima ujisikie vizuri, siyo mastress. Lazima awe mtu ambaye ukijisikia umetatizika, basi awe kimbilio, ambako unaweza kwenda akakupa faraja, siyo uko na mtu ukienda ili kupata faraja, unasikia anakuambia eti, hebu niondokee, nina mambo yangu kichwani, eboo!
Mwanaume mzuri kwako ni yule ambaye unapojisikia haupo salama, basi yeye ndiyo kimbilio lako, una uhakika utapata siyo tu usalama wa maisha yako, bali pia pumziko.
Na usalama ninaouzungumzia, siyo usalama wa kuepuka kukatwa mapanga, hapana, ni ule wa kisaikolojia, unajisikia kama kufakufa hivi, kwa hiyo unataka kuwa na mtu ambaye ukienda kwake unajisikia hofu imekimbia, mtu mwenye uwezo wa kukuhakikishia usalama.
Kitu kingine mashosti, mtu wa kukufaa katika maisha yako, ni yule ambaye wakati wowote anasikiliza, kuelewa na kuwa tayari kuweka mambo sawa ili maisha ya kimapenzi yaendelee.
Maana kuna wanaume wengine mashosti, hawataki mambo yaende kinyume vile wao wanataka, waking’ang’ania jambo wameng’ang’ana! Roho inakuwa imetulia unapokuwa na mwanaume ambaye hata husiti kusema la moyoni, kama ni kukataa au kukubali kitu chochote ambacho mnaweza kukijadili kama wanandoa, wenye uhusiano, yaani mtu na mtu’we!
Katika mazungumzo, unajisikia kama hautaki kitu mnachojadili na mwenzio, unamwambia wazi kuwa hili hapana, tena bila kusita na kama unadhani hicho ni kitu poa, pia unasema bila kusita kwamba kwa hiki, ni baab kubwa. Huyu ndiye mwenza unayemhitaji, siyo eti watu mnajadili kitu, lakini unaogopa, hujui ukubali, hujui ukatae, kwa sababu unahofia sijui mwenzio atabadilikaje, Khaa!!!
Unamhitaji mtu ambaye katika uhusiano wenu, unajisikia raha, raha siyo kwa maana kwamba unaridhika kwenye yale mambo yetu, hapana, raha kwa sababu anakupa raha, unajisikia vizuri kwenye uhusiano, huna shaka kumtambulisha kwa marafiki, ndugu na jamaa, wakati wowote unajisikia vizuri unapohusishwa naye. Siyo uko na mtu, lakini wakija ndugu zako unafikiria mara mbilimbili namna ya kumtambulisha, maana hujui watamuona mhuni, hujui watamuona tapeli, ilimradi huna raha katika kuwa naye.
Comments are closed.