The House of Favourite Newspapers

Utapeli Magroup ya WhatsApp

Na MWANDISHI WETU| GAZETI LA IJUMAA| KIUJUMBE TOKA JUNGUNI

DAR ES SALAAM: Katika kutafuta namna ya kujipatia kipato kwa wakati huu ambapo njia zote za ujanjaujanja zimezibwa na serikali ya awamu ya tano, baadhi ya watu wamebuni mbinu ya kuwatapeli wananchi kupitia makundi ya mitandao ya kijamii hasa WhatsApp.

Kwa mujibu wa mmoja wa watu ambao alijikuta akiingia katika mtego huo kutokana na tamaa yake ya ngono, (jina lake linahifadhiwa) alipata rafiki katika Mtandao wa Kijamii wa Facebook ambaye baadaye alimweleza kuwa ana mtandao wa wasichana mastaa na wasio mastaa wanaojiuza na angeweza kuwapata kirahisi kwa kupewa mawasiliano yao na pia kuona picha na baadhi ya video wakiwa watupu.

Madai yaliyofikia katika dawati la gazeti hili, vijana wengi ambao ndiyo watumiaji wakubwa wa mitandao ya kijamii, wamekuwa wakitapeliwa mara kwa mara kwa kujiunga katika makundi hayo.

Inaelezwa kuwa, mchezo mzima huanzia Mitandao ya Instagram na Facebook ambapo wengi wa matapeli hao huweka picha za wanawake wakali wa Kibongo na kudanganya kuwa wanapatikana kwa njia ya picha na video wakiwa utupu katika makundi yao ya WhatsApp huku wakianika namba za simu watumiwe kiasi cha pesa waunganishwe. Wakishaweka posti hizo katika mitandao hiyo, vijana wengi hukimbilia kujiunga kwa kutumia namba zilizowekwa katika mitandao hiyo kwa kiingilio cha kiasi cha kuanzia shilingi 5,000 hadi 10,000 kwa mmoja lakini wakishajiunga katika makundi hayo hakuna kinachoendelea na hata ukiwatafuta hawapokei simu.

OFM KAZINI Katika siku za hivi karibuni ilibainika kuwa, kuna makundi mengi ya WhatsApp yanayoendesha biashara ya ukahaba. Kikosi kazi cha Operesheni Fichua Maovu (OFM) kikaingia kazini kubaini kama kweli biashara hiyo inaendelea kwa njia ya mtandao ambapo mmoja wa mapaparazi aliomba kuunganishwa na kundi linalojinadi kuwa, ukitaka kahaba wa kila aina unampata.

Kufuatia paparazi kutaka aungwe ili apate huduma, alitakiwa kutuma kiingilio cha shilingi 15, akatuma na kuomba aunganishwe na mmoja wa warembo wakali waliokuwa wamewekwa kwenye group hilo. Heh, imeliwa! Baada ya pesa kutumwa, hakukuwa na mawasilino tena na simu ikawa haipatikani.

Ijumaa linawashauri watumiaji wa mitandao hiyo, kuwa makini na watu wa aina hii kwani kila siku wamekuwa wakiongezeka katika mitandao na kujipatia pesa kwa njia rahisi. Ukishaona unaungwa au unashawishiwa kujiunga na kundi ambalo limekaa ‘kihelahela’, akili kumkichwa.

Comments are closed.