The House of Favourite Newspapers

Wanawake Wengi Hubakwa na Kushambuliwa, Kabila la Wala Watu Sehemu ya 14

0

Na ELVAN STAMBULI| GAZETI LA UWAZI| MAKALA

NAENDELEA kukuletea habari za watu wanaokula binadamu wenzao huko Papua New Guinea. Tumeeleza mambo mengi  juu ya jamii na hasa jinsi walivyokuwa  wanawala hata watumishi wa Mungu, kabla hatujaeleza kilichowapata wamisionari walioingia katika kisiwa hicho hadi kufanikisha kile walichoendea, leo tutasimulia jinsi wanawake wa nchi hiyo wanavyoishi, endelea:

Kwanza nikiri kwamba simulizi hii ya kweli kutoka kwa waandishi waliotembelea kisiwa hicho kimewaacha hoi wasomaji wa safu hii na wengine kusononeka lakini huu ndiyo ukweli wenyewe.

Wenyeji wa kisiwa hiki asilimia 40 wanaishi katika maisha ya kimaskini licha ya ukweli kwamba nchi ina utajiri mkubwa sana kama tutakavyoona baadaye.

Wanawake wengi wa kisiwa hiki wanaishi kwa kukandamizwa, wengi wamekuwa wakiteswa kutokana na mfumo dume ambao umetapakaa duniani. Wanawake ndiyo hutumika kwa kufanya kazi za kulima na kuvuna huku wanaume kazi yao kuu ni kuwinda na kuvua samaki na kulewa.

Kisiwa hiki ambacho kipo maili 100 kutoka Australia kimeelezwa na taasisi maarufu ya kuangalia haki za binadamu ya Human Rights Watch kuwa nchi hii ni moja ya sehemu hatari kwa wanawake kuishi duniani. Inakadiriwa kuwa asilimia 70 ya wanawake katika kisiwa hicho chenye watu wanaokadiriwa kufikia milioni saba, wamejikuta wakibakwa na wengine kushambuliwa na wanaume katika maisha yao ya kila siku.

Utafiti wa taasisi hiyo unaonesha kuwa zaidi ya wanawake nusu ya walioolewa hubakwa na asilimia 68 hupigwa majumbani mwao na wanaume.

Utafiti umebaini kwamba asilimia 41 ya wanaume wamewabaka wanawake ambao siyo wake zao. Wanawake wengi wanasema kwamba wanaposhambuliwa na wanaume, mamlaka au dola huwa haziwasaidii kwa lolote  hata wanapokwenda hospitali au vituo vya afya kutibiwa mbaya zaidi vyombo husika havitunzi kumbukumbu kwa unyama huo wanaofanyiwa wanawake wa nchi hiyo.

Wanawake wengi wamekuwa wakikamatwa uchawi na kufanyiwa vitendo vya kikatili tena vya kutisha kama vile kuvuliwa nguo zote na kubaki kama walivyozaliwa kisha kutembezwa mitaani huku wakipigwa na baadaye kuishia kuuawa kikatili huko vijijini.

“Mtu akiugua au mtoto akifariki dunia ghafla, husingiziwa mwanamke kwamba amemroga marehemu huyo na mara nyingi tuhuma hizo hutolewa na watu wanaomchukia mwanamke mtuhumiwa na kuishia kufariki dunia,” imeeleza ripoti hiyo.

Ipo picha moja ambayo ilisambaa duniani ikimuonesha mwanamke aliyetuhumiwa kwamba ni mchawi akifanyiwa ukatili wa kutisha (tunayo), alionekana akiwa amefungwa kamba mikononi kisha kufungwa juu ya mti na miguu ikiwa imefungwa kamba akiwa uchi wa mnyama huku usoni akiwa amefunikwa na wanakijiji wengine wakiwa wamemzunguka ni picha ya kutisha sana na ni kitendo ambacho siyo cha kistaarabu kabisa.

Mwisho wa vitendo hivyo ni kuuawa kwa mwanamke huyo ambaye inawezekana alisingiziwa tu kwamba ni mchawi. Huyo mmoja ni mfano tu lakini wanawake wanaofanyiwa ukatili huo katika nchi hiyo ni wengi sana huko vijijini. Wenyeji wa huko ukiwauliza kwa nini wanawake wanapigwa, wanasema hivyo ni vitendo vinavyokubalika kwa mujibu wa jadi za nchi hiyo na hufanywa na watu wengi wa visiwa hivyo.

Imeelezwa kwamba vitendo hivyo vimeshamiri kutokana na wanaume wa huko kutumia ulevi, kama vile kuvuta bangi, kunywa pombe za kienyeji na ukosefu wa kufanya mambo kwa ajili ya kujiletea maisha bora.

Hata wasomi waliofanya utafiti katika visiwa hivyo, wamegundua kwamba ukatili kwa wanawake ni jambo linalofanywa na watu wengi na wala hawaoni kama ni kitu kibaya na cha kikatili.

Leave A Reply