The House of Favourite Newspapers

Kama Unawapenda Wanao, Kwa Nini Walelewe na Hausigeli kwa Asili 100%?

0

KAMA wewe ni mfuatiliaji wa makala zangu, utakumbuka niliwahi kuandik sifa za binti anayefaa kuwa dada wako wa kazi nyuumbani kwako. Nilifanya vile kwa kuwa nilijua wengi tunawahitaji sana watu hao kutokana na kubanwa na majukumu yetu ya kila siku.

Lakini niliahidi kuwa, kuna siku nitaeleza hatari ya kuwategemea hawa dada wa kazi kutulelea watoto wetu kwa asilimia 100 na siku yenyewe ni leo. Mpenzi msomaji wangu, hakuna asiyejua kwamba, raha ya ndoa ni kupata watoto. Ndiyo maana wengi wanapoanza maisha ya ndoa akili zao huzielekeza kwenye kupata mtoto.

Kwa nini? Kwa sababu hiyo ndiyo heshima ya ndoa. Angalia wanavyohaha wale ambao wako katika ndoa lakini hawajafanikiwa kupata watoto. Wapo wanaodiriki hata kufanya mambo ya kishirikina ilimradi tu nao waitwe mama fulani ama baba fulani.

Cha kushangaza sasa wakati wengine wanahaha kutafuta watoto eti wapo ambao wanawapata na kuwatelekeza, kitu ambacho ni cha kinyama na kinalaaniwa. Yaani upate mtoto kisha umtupe, kisa eti hali ngumu ya maisha au wengine wanasema watawaondolea ujana wao.

Huo ni ujinga. Mimi nadhani kwa wale ambao hawajabahatika kupata mtoto ni vyema wakawa na subira huku wakiamini ipo siku Mungu atawajaalia. Wasifi kie hatua ya kukufuru, kufanya hivyo wanaweza kukaa milele wasipate mtoto.

Kimsingi wanandoa wanapopata mtoto furaha huongezeka ndani ya ndoa. Hii inatokana
na ukweli kwamba baadhi tunakuwa na wasiwasi kwamba tunao uwezo wa kuzaa ama laa, hivyo tunapopata mtoto tunathibitisha ukamilifu wetu. Lakini wazazi wanapopata mtoto wanakuwa na jukumu moja la msingi sana ambao ni la kutoa malezi sahihi kwa mtoto wao.

Huo ndiyo wakati muafaka wa kuondoa tofauti zao kama zilikuwepo na kuhakikisha kunakuwepo na mazingira ya amani ndani ya nyumba hivyo kuweza kumpa mtoto matumaini ya kuishi vizuri. Mara nyingi wanandoa wanapopata mtoto kama wakiwa na uwezo hulazimika kutafuta msaidizi wa kazi za ndani ‘hausigeli’.

Wengi wetu tunakosea kwa kuwaachia majukumu yote wafanyakazi hawa wa ndani ikiwa ni pamoja na kumlea mtoto katika mazingira ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kumfanya akakosa malezi sahihi. Sawa kuna muda hausigeli anatakiwa kubaki na mtoto wakati wazazi wakiwa kazini, lakini ni vyema kwa wazazi hasa wale wanaofanya kazi wakahakikisha wanakuwa wafuatiliaji wa karibu sana wa malezi anayopata mtoto wao. Nasema hivyo kwa sababu siyo kila mtu anaweza kutoa malezi sahihi kwa mtoto.

Hausigeli kweli anaweza kumlea mtoto lakini ni wachache wanaotoa malezi sahihi. Kwa maana hiyo basi kwa wazazi wanaofanya kazi ni vizuri muda mwingi wanapokuwa nyumbani wakajitahidi kuwa karibu na mtoto wao na kumpa yale wazungu wanayoyaita ‘Professional baby care’ yaani malezi ya kitaalam.

Kimsingi wazazi wanatakiwa kuwa karibu sana na mtoto wao kwani wao ndiyo wenye uchungu naye na ndiyo wanaofahamu wanataka mtoto wao akue katika mazingira gani. Anachojua hausigeli ni kumlisha, kumuogesha na kumbembeleza pale anapolia.

Hausigeli hawezi kumsoma mtoto ana kipaji gani, baadhi yao ni wagumu hata kutambua kama mtoto anaumwa. Matokeo yake mtoto anashambuliwa na ugonjwa kwa muda mrefu bila kupata matibabu na hatimaye kupoteza uhai. Hii ndiyo hatari ya kumtegemea hausigeli katika malezi ya mtoto.

Mbaya zaidi ni kwamba, wazazi wengi wanawaamini sana wafanyakazi wao wa ndani kiasi kwamba hata pale wanapokuwa nyumbani hawajishughulishi kabisa na mtoto wao. Hiyo ni hatari pia, wasipoangalia wanaweza kumkuta mtoto anakuwa na tabia za ajabu bila wao kutarajia.

Mimi nadhani hausigeli awe ni kwa ajili ya kuwaongezea muda wazazi kuwa karibu na mtoto/ watoto wao.

Leave A Reply