The House of Favourite Newspapers

Huku Vanessa Mdee, Jux Wakidaiwa Kumwagana, Mbunge wa CCM Afungukia Uhusiano Wake na Vanessa Mdee

0
Vanessa Mdee.

DAR ES SALAAM: Baada ya uvumi wa muda mrefu unaomhusisha Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Elibariki Kingu na msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya, Vanessa Mdee, hatimaye jipu limepasuka pwaa, kufuatia kiongozi huyo kufungukia ishu hiyo.

MCHEZO MZIMA ULIVYOANZA

Kwa mujibu wa chanzo chetu makini, Vanessa na Kingu wamekuwa wakionekana mara kwa mara katika Hoteli ya Seashers, iliyopo ndani ya majengo ya Millennium Towers, Kijitonyama jijini Dar es Salaam. Katika kukutana huko, inadaiwa kuwa wakati mwingine Vanessa huwa ameongozana na mpenzi wake wa muda mrefu, ambaye hata hivyo inadaiwa hivi sasa hawako sawa, Juma Jux.

Juma Jux.

NINI KILICHOWASHTUA WADAU

Kwa mujibu wa chanzo chetu ambacho kina ukaribu na baadhi ya wadau wa hoteli hiyo ya kishua, kilisema jambo lililowapa mashaka juu ya wawili hao ambao wakiwa hapo huitana dada na kaka, ni vile wakati mwingine walikutana wao peke yao pasipo uwepo wa Jux.

“Ni kweli wakiwa hapa watu wanatambua kuwa ni kaka na dada na mara zote walikuwa wakija pamoja na Jux, lakini ajabu ni kwamba nyakati zingine walikuwa wanakuja Vanessa na mheshimiwa mbunge peke yao na wanaongea hadi wanaondoka bila Jux kutokea, sasa hili likawa linawapa wasiwasi,” kilisema chanzo chetu, kikimnukuu mmoja wa wadau wa hoteli hiyo.

WAHUDUMU WABANWA, WAZUNGUMZA

Risasi Mchanganyiko lilifika katika viunga vya hoteli hiyo na kuvinjari kwa muda, likitaka kupata ukweli juu ya kuonekana katika hoteli hiyo kwa mbunge huyo kijana akiwa ameongozana na mwanamuziki huyo nyota, ambaye hivi sasa anang’ara kimataifa. Mmoja wa wahudumu hao, alikiri kuonekana kwa mbunge huyo, akidai ni mteja wao ambaye hufika hapo mara kwa mara.

“Huyu (baada ya kuonyeshwa picha katika simu) ninamfahamu, huwa anakuja hapa mara kwa mara, ni mtu wetu. Na hata Vanessa na Jux pia wanafika hapa, unajua wale ni watu maarufu na hapa ni sehemu ya mastaa, sina uhakika kama nimewahi kuwaona wote wamekaa meza moja (Jux, Vanessa na Kingu), ila wote hufika,” alisema mhudumu huyo huku akikataa kutaja jina lake.

MBUNGE KINGU APATIKANA, AFUNGUKA

Baada ya kujiridhisha juu ya kuonekana eneo hilo mara kadhaa akiwa pamoja na kampani ya akina Vanessa, Mbunge Kingu alipatikana na akaifungukia ishu hiyo kama ifuatavyo;

“Siyo kweli kwamba nina uhusiano wowote na Vanessa zaidi ya kuwa dada yangu wa hiyari, ni kweli pia kwamba mara kadhaa huwa tunakuwa pamoja pale hotelini, lakini yeye huwa yupo na mtu wake Jux na hata Jux anajua kuwa yule ni dada yangu.

Vanessa na Jux.

“Hawa wanaosambaza haya maneno wana nia ya kunichafua tu, kwa sababu hakuna ukweli wowote kwenye hili jambo,” alisema Kingu.

VANESSA, JUX WASAKWA

Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Vanessa ili azungumzie suala hilo, lakini watu wake wa karibu walisema yupo nje ya nchi kikazi, hivyo kulazimika kutumia Mtandao wa WhatsApp, ambao hata hivyo, ujumbe aliotumiwa kuhusu jambo hilo haukujibiwa, licha ya kuonekana kuwa umefunguliwa na kusomwa.

Aidha, Jux ambaye ndiye mtu anayetambuliwa kama mpenzi wa Vee Money kwa sasa, naye simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

 

 

Leave A Reply