The House of Favourite Newspapers

Elimu ya Kumpata Mwenza Sahihi wa Milele!

0

Na HASHIM AZIZ| GAZETI LA IJUMAA| LETS TALK ABOUT LOVE

UHALI gani msomaji wangu, ni matumaini yangu kwamba unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku, kwa wale ndugu zangu Wakristo, leo ni siku muhimu kwa sababu ni Ijumaa ya Pasaka, nawatakia kila la heri na maandalizi mazuri ya Jumapili ya Pasaka.

Kwa wiki mbili zilizopita, tulikuwa tukijadiliana kuhusu mada ya kwa nini uuvumilie uchumba wa kuumizwa kila siku? Nilikuahidi kwamba wiki hii nitakujuza mambo muhimu ambayo kama unataka usiwe miongoni mwa watu ambao wanaishia kwenye uchumba na baadaye kuumizwa kila siku.

Mapenzi ni sanaa kama zilivyo sanaa nyingine, wazee wetu wa zamani wana usemi wao kwamba sanaa ya mapenzi ni sawa na sanaa ya kupiga gitaa. Sote tunalijua gitaa lakini kama hujawahi kujifunza kulitumia, leo ukipewa, kamwe huwezi kutoa muziki mzuri, utaishia kugusagusa nyuzi tu.

Lakini mtu ambaye amejifunza na anajua namna ya kulitumia gitaa, ataweza kupiga muziki mzuri utakaomburudisha kila atakayeusikia. Mapenzi nayo ni hivyohivyo, tukianza kuulizana mmojammoja, ‘umejifunzia wapi mapenzi?’ bila shaka majibu yatakuwa ya ajabuajabu sana.

Simaanishi umejifunzia wapi mapenzi kwa maana ya tendo la ndoa, la hasha! Namaanisha sanaa nzima ya mapenzi kwa sababu tendo ni sehemu tu ya mapenzi lakini kuna mambo mengine mengi ambayo kwa pamoja ukiyaunganisha ndiyo unapata tafsiri sahihi ya mapenzi.

Ukweli mchungu ni kwamba watu wengi hawana uelewa na ujuzi wa kutosha kuhusu mapenzi, wanabahatisha tu na kibaya zaidi, hawapo tayari kujifunza na hata wale ambao wapo tayari kujifunza, hakuna sehemu elimu hii inaweza kupatikana kwa urahisi.

Tofauti na wenzetu wa nchi za Magharibi ambao elimu za uhusiano na mapenzi hutolewa kwa vijana tangu wakiwa wadogo, kwa jamii za watu weusi suala hili ni nadra sana au ni kitu ambacho hakiwezekani.

Kwa mantiki hiyo, ndiyo maana wengi wetu wanaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi wakiwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu mapenzi, matokeo yake wanaishia kuumizwa na kulia kila kukicha. Unaweza kuwa umejitunza sana lakini hilo pekee halitoshi kukupa tiketi ya moja kwa moja ya kuingia kwenye ndoa, lazima ujifunze na hicho ndicho ninachokifanya hapa.

Jambo ambalo watu wengi hawalijui, mwanamke au mwanaume unayepaswa kuingia naye kwenye ndoa, ni lazima uwe na uhakika kwamba kweli anakupenda.

Hata hivyo, ni nadra sana kumpenda mtu halafu naye akawa anakupenda kwa kiwango kilekile. Utaweza kugundua hilo ikiwa tu utajipa muda na kuhakikisha ‘unakaba mpaka penalti’ kwa huyo mwenzi wako, ili uweze kuujua ukweli wa maisha yake na wakati huohuo, ukijifunza nini anachokipenda, tabia zake zikoje.

Wanaume wengi au wanawake wengi, huwa ni wepesi kuigiza maisha yasiyo halisi wanapoanza uhusiano na wewe lakini unapoamua kukaba mpaka penalti, unamnyima nafasi ya kuishi maisha ya kuigiza na badala yake, ataonesha maisha yake halisi na hapo ndipo unapoweza kuamua kama anakufaa au la.

Kwa taarifa yako, mapenzi imara ni yale ambayo huanzia kwenye urafiki wa kawaida, unaweza kuwa umependa au yeye anakupenda lakini badala ya kukimbilia kwenye tendo, ni vizuri mkaanza na urafiki wa karibu kwanza na hapo ndipo unapoweza kugundua kwamba anakupenda kwa dhati au anakutamani.

Tukutane wiki ijayo kwa mwendelezo wa mada hii nzuri.

Leave A Reply