Mshambuliaji Mesut Ozil ameendelea kuweka hai matumaini ya Arsenal kumaliza Ligi Kuu ya England ikiwa katika nafasi ne za juu baada ya kufunga bao la ushindi katika mchezo wa timu yake dhidi ya Middlesbrough.
Arsenal imepata ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo huo wa ligi hiyo maarufu kwa jina la Premier League, uliopigwa jana usiku.
Mjerumani huyo alifunga bao katika dakika ya 71 baada ya Alexis Sanchez kutangulia kufunga bao la kwanza kwa timu yake katika dakika ya 42.
Licha ya Arsenal kutangulia kufunga bao, wapinzani wao walisawazisha katika dakika ya 50 kupitia kwa Álvaro Negredo.
Kutokana na ushindi huo Arsenal sasa ipo nafasi ya sita ikiwa ni nyuma kwa pointi saba dhidi ya timu inayoshika nafasi ya nne, Manchester City lakini City ikiwa imecheza mchezo mmoja zaidi.