The House of Favourite Newspapers

Roma, Naisubiri Siku Uteme Nyongo!

0
Roma Mkatoliki na mwanaye Ivan.

Na OJUKU ABRAHAM| RISASI MCHANGANYIKO| RISASI VIBES

MUZIKI ni sanaa pana inayohitaji zaidi akili iliyotulia ili kuifanya kuwa bora na isiyokufa. Ni wanamuziki wachache wamewahi kumudu kuifanya kazi yao kuwa ya muda wote kwa nyakati zote, bila kujali vizazi vinavyokuja na kupotea, vinavyochagizwa na kukua kwa teknolojia.

Robert Nesta Marley.

Katika kundi la wanamuziki wa aina hiyo, unamkuta Robert Nesta Marley, ambaye wengi tumezoea kumwita Bob Marley. Ingawa alifariki mwaka 1981, ndiye mwanamuziki wa Reggae anayefahamika kuliko wengine wote, wakiwemo wanaoimba hivi sasa!

Wakati Marijani Rajab ‘Jabali la Muziki’ akiimba kibao cha Geogina miaka mingi iliyopita, hakujua kama leo hii, vijana waliozaliwa miaka ya themanini na tisini wanacheza na kuimba kibao chake kana kwamba kimeimbwa na akina Khalid Chokoraa! Hata hivyo, sanaa ya muziki pia inatambua umahiri wa watu wanaoimba kwa masilahi ya nyakati za kizazi chao, iwe kwa ajili ya kuiburudisha jamii inayomzunguka, kufundisha, kuhadharisha na madhumuni mengine kedekede.

Katika kundi hili, kwa wanamuziki wetu wa kizazi kipya, tunao wengi wanaostahili tuzo. Wanafanya muziki wao kwa faida ya kizazi chao cha sasa, mashabiki wanapata burudani, wanapewa hadhari, wanafundishwa na wakati mwingine hata kushauriwa.

Roma Mkatoliki.

Roma Mkatoliki ni mmoja wa vijana wazuri wanaoimba Hip Hop. Nimesikiliza nyimbo zake nyingi, kuanziakibao chake cha kwanza, Tanzania. Ukimsikiliza, siyo tu unatambua kuwa ni mwenye ufahamu wa kutosha kuhusu mambo ya nchi yetu, lakini pia ni jasiri.

Anazungumza kwa niaba ya watu, matatizo yetu kama nchi, nani hasa wanatupoteza, kwa nini wengine hawaguswi, tufanye nini ili twende sawa na vitu vingine vinavyofanana na hivyo, kitu ambacho wasanii wengi wa kariba yake hawawezi kufanya. Wanaogopa kuwagusa watawala maana hawajui wataamua nini juu yao!

Roma aliimba nyimbo nyingi za ‘kukera’ watawala katika awamu ya nne, lakini hakuwahi kupewa misukosuko yoyote na sisiti kuamini kuwa hata wimbo wa Nay wa Mitego, Wapo, aliufanya kwa kujaribu kuiga ujasiri wa mwenzake katika kugusa ‘mamlaka’.

Sikumbuki Roma kuimba wimbo wenye kuonekana kama anaishambulia serikali katika awamu ya tano. Kama Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliupenda na kuruhusu upigwe katika vyombo vya habari Wimbo wa Wapo, ambao una viashiria vingi vya kuikosoa serikali, sioni ni kwa wimbo gani unaweza kuwa umeongoza Roma kutekwa na kuteswa.

Ndani ya Wapo, kuna mashairi ambayo baadhi ya watendaji wa serikali, kwa hofu yao tu, waliamua kumkamata Nay wa Mitego, wakaupiga marufuku wimbo wake kupigwa na matayarisho ya kumshtaki yakaanza, lakini kwa namna ya kushangaza, Rais Magufuli akawa tofauti nao.

Hamis Mwinjuma, ‘Mwana FA’ (Kulia) akiwa na Ay.

Hivi karibuni, Hamis Mwinjuma maarufu kama FA, alisema Rais Magufuli alimpigia simu na kumweleza kuwa yeye ni shabiki wa muziki wake na kuwa anakifagilia sana kibao chake kilichopo mtaani kwa sasa, Mwanaume Suruali! MwanaFA ni mmoja wa marapa wazuri, lakini yeye siyo mkosoaji wa watawala na wala hajishughulishi na nyimbo zenye mlengo wa siasa, ingawa ana uelewa wa hali ya juu katika mambo ya siasa kuliko wasanii wengi.

Kama Rais ameruhusu Wimbo wa Wapo upigwe redioni na tena anaupenda wimbo wa MwanaFa wa Mwanaume Suruali, Roma amefanya nini? Waliomteka hawawezi kuwa mawakala wa serikali kwa sababu hatuoni katika wimbo upi watawala wamekwazika.

Waliomteka hawakuwa na nia ya kumuua, ila kuna kitu tusichokijua walihitaji kukifahamu kutoka kwake. Kama nilivyosema mwanzo, Roma ni jasiri. Anajua kama watu hawakutosheka na alichokisema kwenye ile press conference kwa sababu yule siyo Roma wanayemjua.

Mashabiki wanasubiri Roma awaeleze ukweli kwa sababu hawaamini kama ile ni sinema ya kutafuta kiki.
Hata yeye mwenyewe anajua kama hakuwashibisha. Na bahati mbaya ni kwamba wote wanajua siku ile hakusema walichotaka kukisikia na kinachosikitisha zaidi ni kuwa hata akirejea tena na kuongopa, watajua wamedanganywa.

Itazame Video Roma Afunguka Tukio la Kutekwa..

Leave A Reply