The House of Favourite Newspapers

Roho Nzuri ya Mumeo Isikupe Wivu

0

Na MWANDISHI WETU| RISASI MCHANGANYIKO| MAKALA

HALO haloooo mashosti, leo nina booonge la umbeya ninawaletea, si unajua tena nimetoka kwenye sikukuu, hata kama hainihusu.

Ndiyo, mie Muisilamu, lakini Wakristo ndugu zangu, sasa hivi hapa tangu Ijumaa Kuu, sipo nyumbani, nilikuwa zangu Mbagalaaaaaa nafyonza vitu vitamu! Nikiwa huko sasa, wenyeji wangu si wakawatonya majirani kwamba mimi ndo Anti Nasra, basi kila siku mimi mtu wa kuwekwa kati, wengine wanataka umbeya, wengine wanaleta umbeya, ilimradi kijiwe kikawa hakijai wala hakipungui.

Nimepata ubuyu mwingi kiasi kwamba ninaweza kuwaletea mwaka wote huu ukaisha, lakini kama mnavyojua, hatuwezi kuzungumza mada kutoka Mbagala pekee, kwa sababu tuna umbeya kutoka kila kona, hasa ninapokuwa pale barazani kwangu, wanakuja hadi Wangazija, wale ndugu zetu wa visiwa vya mbali bahari ya Hindi.

Basi kaja bi mkubwa mmoja kunilalamikia, eti ooh, mumewe ana roho nzuri kiasi kwamba yamtia wasiwasi, anadai hawezi kumpita jirani njiani akaacha kumsalimia, kumwulizia kuhusu familia na vitu vingine na ni mwepesi kutoa msaada pale anapoweza, kiasi kwamba inamtisha, kwa sababu michepuko inaweza kutumia nafasi hiyo kumpora mumewe, au hata yeye kutumia fursa ya kusaidia majirani kufanya ufuska!

Nikashangaa sana, ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kumsikia mtu akitishwa na roho nzuri ya mumewe, maana mimi naonaga watu wanalalamikia tabia za waume zao kutokuwa na roho nzuri, au kutopenda kujiweka karibu na jamii inayomzunguka!

Lakini mwishoni nikamuelewa yule bibie, kwamba hana matatizo na mumewe, ila ana wasiwasi na wanawake wenzie, wanaweza kutumia kanafasi ka roho nzuri ya mumewe, wakamwekea mitego, si unajua tena sisi tulivyo jamani, tuna mitego mingi tukiamua kuitega mwanaume rijali hachomoi! Lakini niwaambie mashosti, kwanza nilimtoa wasiwasi kabisa yule mama, kwamba hana sababu ya kumtilia mashaka mumewe, kwa sababu roho nzuri au mbaya huzaliwa, hazitengenezwi.

Kama mtu amezaliwa na roho nzuri, ya kuwajali wenzake, ya kuwasaidia wenzake na hata kuwasikiliza, ni tofauti kabisa na mwanaume mkware.

Roho yake nzuri kamwe hawezi kumtumia kwa ajili ya ukware, maana tayari kuna watu wenyewe wamezaliwa na tabia hiyo.

Na hapa nataka niwaambie nyie wanangu, sisi tuliofanya umalaya zamani ndiyo tunajua, maana kipindi kile ukisikia mtu huyu ni mchungaji, basi ni mchungaji kwelikweli, huwezi kusikia eti kamrubuni muumini kafanya naye ujinga, kwa hiyo tunajua tofauti ya mtu mwema na muovu.

Usihofu kama mumeo ana tabia njema. Ninaposema tebia njema wewe mwenyewe unajua, maana isije ikawa ni mhuni, ukasema ni njema, hapana, hawa watu ni tofauti.

Kama mzee anapenda na kuwajali majirani, wake kwa waume huna haja ya kuwa na hofu kwa sababu hilo ni jambo jema. Katika vitu ambavyo binadamu tumependelewa ni kupewa umbeya bure.

Kama mumeo ni mchepukaji, huna hata haja ya kuhofia wema wake, kwa sababu utaletewa tu, tena kwa kebehi. Lakini ukiona mtu amekuwa mwema na hadi leo hujaletewa chochote, ujue hana madhara.

Ni jambo la heri kuwa na mume mpenda haki, kujali na heshima kwa majirani, kuliko uambiwe mumeo ana roho mbaya, katili utajisikiaje?

 

Leave A Reply