The House of Favourite Newspapers

Hivi Anayewauzia Wadada Simu Mbovu ni Nani?

0
Emmanuel Mathias, ‘Mc Pilipili’ (kushoto) akiwa na Young D.

Na MC PILPILI| GAZETI LA AMANI| KIJIWE CHA MC PILIPILI

UNAJUA nimekaa na kujiuliza maswali mengi sana kuhusu hawa dada zetu na hizi simu za mkononi. Nimejiuliza weee lakini wapi, sijapata jibu hata moja, hebu naomba na wewe unisaidie.

Hivi kwa mwanamke unayeanza naye uhusiano wa kimapenzi, kuwa na simu mbovu ndiyo fasheni? Yaani kademu umekatongoza lakini kila ukikutana nako, kana simu imefungwa rubber band (balabendi)! Mwingine hata aibu hana, eti utasikia ooh, baby unajua mi muda mwingine nakuwa sipatikani kwa sababu simu yangu mbovu.

Na ukiiangalia simu kweli mbovu haswaa, kama usipokuta kioo kina ramani ya dunia, basi ujue nyuma haina mfuniko, au muda wote ‘battery’ low, wengine ndiyo wanatembea na power bank kabisaa, muda wote simu imechomekwa na bado ina chaji asilimia nne.

Hivi nauliza, huyu anayewauzia wadada hawa tunaoanzisha nao uhusiano simu mbovu ni nani? Yaani yeye kazi yake ni kuwauzia simu mbovu tu? Au linakuwa ni dili? Basi bhana, akishakuonesha simu yake mbovu na kukupa visingizio kibao unajua kinachofuata ni nini?

Atakutafutia ‘timing’ tu, siku ukijaa kwenye kumi na nane zake, huku akikurembulia macho na kubinua midomo kimahaba, utasikia… ‘baby naomba ninunulie simu mpya, si unaona ninavyoteseka mkeo? Hapo huna ujanja, hata uwe bahili kama Mchaga au Mpare, lazima utanunua simu, tena smartphone kali kabisa! Wanawake Mungu anawaona!

 

Leave A Reply