Elimu ya Kumpata Mwenza Sahihi wa Milele- 2

 

NI matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa, bila shaka kwa wewe ndugu yangu Mkristo, ulisherehekea vyema Sikukuu ya Pasaka. Nakukaribisha tuendelee na sehemu ya pili ya mada tuliyoanza kuijadili wiki iliyopita.

Tulianza kujadili kwamba kama unataka kuingia kwenye uhusiano ambao baadaye utazaa ndoa na familia bora, lazima uwe makini na mtu unayeanzisha naye uhusiano. Siku hizi wengi wapo kwa ajili ya kukidhi tamaa zao za ngono kuliko mapenzi ya dhati. Nikakudokeza kwamba, uhusiano mzuri ambao unaweza kuja kuishia kwenye ndoa na familia bora, lazima uanzie kwenye urafiki.

Ipo wazi kwamba hakuna urafiki wa kawaida kati ya mwanaume na mwanamke, ni sawa lakini narudia kukusisitiza, uhusiano imara lazima uanzie kwenye urafiki. Maana yangu ni ipi? Mnapoanzia kwenye urafiki wa kawaida, ni rahisi mtu kuonesha tabia zake halisi.

Marafiki huzungumza mambo mengi sana, hata yale ya kijinga! Marafiki husimuliana mambo mengi sana yanayohusu maisha yao ya baadaye au yaliyopita. Tofauti yake, wapenzi hawapati muda wa kutosha wa kujadili kwa upana mambo mbalimbali yanayowahusu, tayari kunakuwa na mipaka ambayo huwezi kuivuka kwa urahisi.

Kama anakupenda kwa dhati, hata kama hajakutamkia, ni rahisi kujua kwa zile ishara na matendo anayokufanyia mkiwa marafiki wa kawaida na jambo ambalo wengi hawalijui, hisia zinazoanza kuchipuka mkiwa tayari mnafahamiana, zina nafasi kubwa ya kuwavusha kutoka hatua ya urafiki wa kawaida, uchumba na hatimaye ndoa.

Utakapokuwa na uhakika kwamba ni kweli anakupenda, hapo ndipo unapokuja ule usemi maarufu wa vijana wa ‘kukaba mpaka penalti.’ Ukishajua anakupenda, na wewe unampenda, unapaswa kuhakikisha hakuna mtu anayekuja kuingilia uhusiano wenu na kuwavurugia.

Umeshawahi kusikia mtu analalamika kwamba mchumba wake alimsaliti kwa kutoka na rafiki yake na mpaka leo wameoana na huyo rafiki? Kuwa makini, ukishajua anakupenda, muda mwingi fikiria namna ya kumfanya aendelee kukupenda daima, epuka maudhi, epuka vikwazo au masharti yasiyo na kichwa wala miguu, onesha uaminifu kwa asilimia 100, onesha kumjali na kumfanyia yale yote ambayo unapaswa kuyafanya kwa mtu unayempenda!

Utashangaa baada ya muda fulani kupita, yeye au wewe, au nyote kwa pamoja mnaanza kuitamani ndoa, kwa pamoja mnapanga malengo yenu na kumtanguliza Mungu, mwisho wa siku mnakuwa mume na mke halali. Zinabaki tu kumbukumbu tamu za namna mlivyoanzisha safari yenu ya mapenzi! Kuna baadhi ya watu ambao kwa kujua au kutokujua, aina ya maisha wanayoishi, yanawafanya hata wale watu wenye nia njema nao, kuwaogopa na mwisho wanapishana na bahati.

Mtu anaweza kupata rafiki mwenye malengo ya kuja kuwa mume au mke, lakini kwa sababu ameshaji-tune akilini maisha ya ujana yanavyotakiwa kuwa, anachoangalia yeye, kama ni mwanamke, ni kupata mwanaume ambaye atakuwa na uwezo wa kumpa shilingi elfu kumi, ishirini au hamsini kila wanapokutana, tena wanakutania nyumba za kulala wageni! Unategemea atakuja kuwa mumeo huyo?

Ni fasheni siku hizi kwamba leo mnakutana asubuhi, jioni mmeshavunja amri ya sita, au leo mmejuana siku mbili tatu tayari mmeshaanguka dhambini! Humjui alikotoka, hujui aliyekuwa naye na ikitokea bahati mbaya amekuja na maradhi yake, basi anakuwa ameshakuambukiza.

Usiwe limbukeni wa mapenzi, ufundishe moyo wako kuwa na subira ili hata ukiamua kuingia kwenye uhusiano, unakuwa na uhakika na unachokifanya.

Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Kwa maoni, ushauri, nicheki kwa namba ya hapo juu, tuma meseji ya kawaida au nicheki WhatsApp.

 


Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment