The House of Favourite Newspapers

Cheka, Mbelwa Wasimulia Walivyong’atana Ulingoni

0
Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka.

Na Ibrahim Mussa | Championi Jumatano | Makala

ZIMEPITA takribani siku 136 sawa na miezi minne na siku 11 tangu bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka afungiwe kucheza ngumi za kulipwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) kufuatia kitendo chake cha  kugomea kupigana na bondia Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’, Desemba 25, mwaka jana.

Siku saba kabla ya pambano hilo, Cheka alipoteza pambano la ubingwa wa WBO Asia Pasific kwa KO dhidi ya bondia raia wa India, Vijender Singh, hali ambayo inadaiwa ilisababisha mkongwe huyo katika ngumi kugomea kupanda ulingoni huku nyuma yake kukiwa na madai ya kutolipwa fedha zake hadi kupelekea kufungiwa miaka minne.

Bondia Said Mbelwa akipiga bag zito kwa ngumi nzito wakati akijiandaa na mpambano.

Mapema mwezi uliopita, kamisheni ya ngumi za kulipwa ilimfungulia bondia huyo kutoka kifungoni ambapo wikiendi iliyopita alipanda ulingoni katika pambano lisilokuwa la ubingwa dhidi ya Saidi Mbelwa ‘Moto wa Gesi’.

Katika pambano hilo lililofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, lilivunjika katika raundi ya sita na Cheka kupewa ushindi wa KO kufuatia madai ya mpinzani wake kucheza rafu za makusudi ikiwemo kumng’ata meno begani.

Championi limezungumza na aliyekuwa mwamuzi wa pambano hilo ambaye ni Katibu wa Chama cha Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST), Anthony Rutta ambapo  ameanza kwa kusema kuwa: “Kiuhalisia Mbelwa alikuwa ameachwa mbali sana kwa pointi tangu mwanzoni mwa raundi ya kwanza katika pambano lile na yeye ndiye alianza kufanya vurugu za makusudi, maana alishaanza kuchoka mapema.

Vurugu gani alianza kuzifanya

“Ukiangalia video utaona alimchomekea mwenzake mguu katika kamba kwa lengo la kupoteza stamina na hapo ndipo alipomng’ata Cheka na meno yameoneka wazi katika bega la Cheka, hawezi kukataa kwa sababu mimi ndiye nilikuwa naona kila kitu.

“Kuhusu suala la kugeuka na kumpa kisogo mpinzani wake lipo wazi maana Mbelwa ni bondia mkubwa anatambua kuwa hairuhusiwi kufanya hivyo na kama alikuwa amekwepa alitakiwa kugeuka palepale haraka lakini siyo kubaki vile ila kwa kuwa alishachoka kwani hata ile ngumi ya Cheka ilikuwa kama amemsukuma.

“Lakini Cheka nilimpa onyo na hata Mbelwa pia  nilimpa onyo na wakati Cheka anampiga ngumi pale chini ndiyo alikuwa ameshang’atwa sasa kwa hasira na ilikuwa ni mara ya tatu anarudia kufanya hivyo,  awali niliwapigia kelele kuwaonya nikashindwa, nikasusa kwa kuona bora niwaache waendelee.”

Sasa Cheka alishinda vipi kama pambano lilivunjika?

 “Nikiwa kama mwamuzi ilikuwa inaonekana wazi Cheka ameongoza karibu raundi zote na ushindi alioupata umetokana na majaji, Robert Kasiga, Said Chaku na Agapeter Mnazareti ndiyo walikuwa wanahesabu pointi.”

Msikie Mbelwa anavyosema

Championi lilimtafuta Mbelwa ambaye alianza kwa kusema: “Kwanza nilifanya mazoezi ya kutisha kwa ajili ya kumpiga Cheka na kweli nilianza kumchapa tangu raundi ya kwanza yaani karibu raundi zote nilikuwa naongoza hata video zinaonyesha hivyo, raundi ya pili nilimpasua kwenye jicho kwa ngumi kali.

“Sasa alivyoona amepasuka ndiyo alianza kunipiga ngumi nyuma ya kisogo katika raundi ya tatu, mwamuzi akaacha, hakuchukua hatua zozote, kulikuwa na viwiko na kufinya, mimi kama bondia mkubwa ambaye nimeshacheza mechi nyingi nje ya nchi kwa hali ilivyokuwa inaenda nikajua tu kuwa kuna maamuzi yamepangwa tayari yaani mshindi walikuwa naye kabla ya pambano kuisha.

“Hata kama pambano lingekuwa limeisha katika raundi zote kumi kwa lazima wangempa ushindi ukiangalia amewalipia waamuzi chakula na sehemu ya kulala kwa sababu yeye ndiye aliyeandaa pambano, sasa wanaanzaje kumnyima ushindi?

“Ukiangalia vizuri rafu zote amecheza yeye, nipo chini kengele imeshapigwa lakini bado alikuwa akinishambulia na hakuna sheria inayosema hivyo kuwa mpinzani wako akianguka chini unaruhusiwa kuendelea kupigana naye, hapo ndipo pambano likavunjika.

“Tena hadi mdogo wake, Cosmas Cheka aliingia ulingoni kuja kunishambulia nyuma ya mgongo, polisi walimuona wakampiga sana na kwenda kumuweka mahabusu.”

Vipi kuhusu meno?

“Yale siyo meno kama utaangalia vizuri, nilikuwa chini yeye alikuwa juu akawa ananipiga tena ‘gumsheet’ yake ilikuwa sehemu moja ipo wazi imeachwa na ndiyo akaning’ata mpaka nikawa nalalamika kwa kupiga kelele sasa hilo kovu analosema nimemng’ata hilo ni punye asitake kudanganya watu.

“Kiukweli licha ya Cheka kuning’ata nilikuwa nataka kumrudishia ila bahati yake ‘gumsheet’ yangu ilikuwa ni mpya hivyo hakuweza kuchomoka haraka lakini huwa sipendi kuonewa maana na mimi nilitaka kumtia meno ili aone maumivu yake.”

Cheka naye huyu hapa
Championi lilipomtafuta Cheka, alianza kwa kusema: “Nashukuru Mungu kwa kuweza kushinda pambano langu kihalali kwa sababu ni bondia mkubwa.

“Kuhusu fujo nadhani hii itakuwa ni mechi yangu ya kwanza kabisa tena baada ya chama kutangaza mshindi kutokana na kuona hakukuwa na tatizo lolote upande wangu kwa sababu Mbelwa alining’ata na mimi nikamng’ata kwa kumrudishia.

“Raundi zote nimempiga ila katika raundi ya nne  ndiyo alianza kufanya vurugu zake baada ya kumpiga ngumi kali sana kichwani, sasa kama anasema nimepiga kisogoni, yeye alirusha ngumi nikamkwepa na akapita moja kwa moja ndiyo ikanitoka hiyo ngumi.

“Kiukweli pale nilichofanya ni kama kuteleza kwa kumkwepa ambapo nilimzunguka akapita na kuanguka mwenyewe na hiyo siyo kwake tu hata Mada Maugo, Rashid Matumla walishawahi kuteleza kutokana na kuwazunguka, Japhet Kaseba ndiyo mara nyingi sana, uzuri wake amekiri kwamba alifanya kosa kugeuka na ameomba radhi kwa kuwa anajua bondia hatakiwi kufanya vile.

Ilikuaje ulianza kumpiga wakati yupo chini?

“Unajua pale kwanza vurugu ndiyo zilianza kutokea halafu pia ifahamike kwamba mimi ni binadamu naweza kukosea, siyo muhuni kwenye ngumi na sijawahi kucheza ngumi za kihuni na kama nilimpiga ngumi vile ilikuwa ni kwa sababu ya damu imeshacheka ndani ya ringi na haikuwa dhamira yangu.

“Nawaomba mashabiki wangu wanisamehe.”

MSN mabao 100 msimu wa tatu

Barcelona, Hispania

MASTAA watatu wa klabu ya Barcelona ya Hispania wanaojulikana kwa jina la MSN, wamefanikiwa kufikisha mabao 100 tena.

Barcelona kwa sasa inawania ubingwa wa ligi kuu ya nchi hiyo, La Liga na wachezaji hao ndiyo wameonekana kuwa hatari sana kwa siku za hivi karibuni.

Hwakupata nafasi ya kucheza pamoja muda mwingi msimu huu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara, lakini kwa umoja wao wamebebana na kuweka rekodi ya kufunga mabao 100 kwenye misimu mitatu mfululizo.

Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar ndiyo wachezaji bora wa timu hiyo kwa sasa na duniani kote kutokana na kiwango chao.

Uwanjani wamekuwa watu hatari sana wakionyesha kiwango kizuri, lakini zaidi uwezo wao wa kupachika mabao ndiyo umekuwa ukiwabeba.

Baada ya mastaa hao kufunga mabao manne kwenye mchezo wa ligi wikiendi iliyopita dhidi ya Villareal sasa wamefikisha mabao 101 wakiwa ndiyo bora zaidi duniani na hakuna wanaoweza kuwafikia msimu huu.

Barcelona ndiyo timu iliyofunga mabao mengi zaidi msimu huu hadi sasa katika ligi zote tano kubwa barani Ulaya wakati wenyewe wakiwa wamefunga mabao 108 hadi sasa, wanafuatiwa na Monaco  ambao wao ni vinara Ligi Kuu Ufaransa ambao wamefunga mabao 98 tofauti ya  mabao 10.

Wachezaji hao watatu wameshafunga asilimia 63 ya mabao yote ya timu hiyo msimu huu.

Messi ndiye kinara kwa sasa akiwa amefunga mabao 51, Suarez amefunga 34 huku Neymar akifunga 16.

Kiwango hiki ni kikubwa zaidi ya kile ambacho wamefunga wapinzani wao wakubwa Real Madrid ambao kombinesheni yao inajulikana kwa jina la BBC ikiwa na Gareth Bale, Karim Benzema na Cristiano Ronaldo, ambao kwa ujumla wao wamefanikiwa kufunga mabao 61 ni nyuma mabao zaidi ya 40 kwa MSN lakini timu kwa ujumla ikiwa imefunga mabao 96 ambayo ni nyuma kwa mabao 12.

MSN ndiyo Barcelona, inaonekana dhahiri kuwa bila watu hawa basi timu hiyo inaweza kushindwa kufurukuta.

Uwepo wa wachezaji hao fiti kwa misimu yote umeweza kuwafanya vijana hao wanaotaka ubingwa wa La Liga msimu huu kutembea kifua mbele.

Iliaminika kuwa wangeweza kufanya mambo makubwa na kufunga mabao mengi kuliko hayo lakini majeraha ya Neymar msimu huu yaliwazuia kuweza kuwika vizuri.

Neymar amefunga mabao machache kwa kuwa amekuwa na msimu mbaya wa kupata majeraha ya mara kwa mara na kukumbwa na jinamizi la kadi nyekundu.

Kiwango cha juu sana cha mabao ambayo wamefunga kwa msimu mmoja ni 131 waliyopachika msimu uliopita wakati msimu wa 2014-15 walifanikiwa kufunga mabao 122.

Hofu kubwa kwao ni kwamba kila msimu wamekuwa wakishuka chini, kuanzia 131 wakafuata 122 na sasa wapo 101 na picha halisi inaonyesha kuwa hawataweza kufikia rekodi zao hizo za nyuma, lakini litakuwa kosa kubwa kama wataacha kuheshimiwa.

 

 

Leave A Reply