The House of Favourite Newspapers

JPM Kupokea Ripoti ya Mchanga Leo

0
Rais Dk. John Pombe Magufuli.

MWANDISHI WETU, RISASI MCHANGANYIKO

DAR ES SALAAM: Rais Dk. John Pombe Magufuli, leo anatarajiwa kupokea ripoti ya kamati maalum aliyoundwa kuchunguza mchanga ulio katika makontena ya mchanga wa madini (Makinikia) yaliyopo katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais na kusainiwa na mkurugenzi wake, Gerson Msigwa, tukio hilo litafanyika ikulu jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, huku likirushwa moja kwa moja na vituo vya redio, televisheni na tovuti rasmi ya ikulu.

Taarifa hiyo imewakaribisha wananchi kutazama na kusikiliza matangazo hayo yatakayorushwa hewani kuanzia saa 3.30 asubuhi kutoka ikulu jijini Dar es Salaam. Wakati huohuo, Rais Magufuli amewahakikishia wafanyabiashara wawekezaji wa kutoka Shirikisho la Mitambo ya Viwanda la China (China National Machinery Industry Federation – CNMIF) kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itawapa ushirikiano wa kutosha katika mpango wao wa kuwekeza kwenye uzalishaji wa nishati ya umeme, viwanda na kilimo hapa nchini.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana ikulu jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa CNMIF na Mbunge wa Bunge la Wananchi wa China, Zhan Xin. Rais Magufuli alisema Tanzania imejiwekea malengo ya kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka Megawatts kati ya 1,500 na 1,800 zinazozalishwa hivi sasa hadi kufikia Megawatts 10,000 na kwamba ili kufikia malengo hayo wawekezaji wanakaribishwa kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo vilivyopo kama vile gesi, makaa ya mawe na jua.

“Kwa hiyo Zhang Xin kawaambie wawekezaji wenzako wa China waje Tanzania, nchi zetu ni ndugu na marafiki wa miaka mingi, itakuwa jambo jema wakija kuunga mkono juhudi zetu za kujenga viwanda kwa kuzalisha umeme mwingi na pia kushiriki katika miradi mingine ikiwemo ya ujenzi wa miundo mbinu ya reli na barabara,” alisema Rais Magufuli.
Katika tukio lingine, Rais Magufuli alikutana na Balozi wa Ufaransa nchini, Malika Berak ambapo viongozi hao wamezungumzia utekelezaji wa mambo mbalimbali ya ushirikiano pamoja na miradi ya maendeleo iliyotokana na makubaliano ya Mkutano wa Wafanyabiashara wa Tanzania na Ufaransa uliofanyika hivi karibuni. Viongozi wengine ambao jana walikutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli ni Kaimu Balozi wa Uturuki nchini, Yunus Belet na Kaimu Balozi wa Jamhuri ya Korea, Songwon Shin.

Leave A Reply