The House of Favourite Newspapers

Sakata la Matrilioni Ya Fedha Mchanga wa Dhahabu Akipona Mtu Akatambike

0

STORI: MWANDISHI WETU | UWAZI | HABARI

DAR ES SALAAM: Wakati nchi nzima ikiwa bado imelivalia njuga sakata la utoroshwaji wa madini kupitia usafirishaji wa mchanga wa madini, unaofanywa na kampuni za kigeni za uchimbaji madini, mikakati ya vyombo vya ulinzi na usalama juu ya watu waliohusika na dili hizo inaonyesha kuwa akipona mtu, basi aende akatambike, Uwazi linakupasha.

Rais Dk. John Magufuli.

Akizungumza wakati wa kukabidhiwa taarifa ya uchunguzi uliofanywa na kamati aliyoiteua ya kuchunguza mchakato mzima wa usafirishwaji wa mchanga wa dhahabu nje ya nchi wiki iliyopita, Rais Dk. John Magufuli aliwataka wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwachunguza na kuwachukulia hatua za kisheria mara moja watu wote wanaojihusisha na suala hilo, wakiwemo maofisa wa ngazi za juu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini, TMAA.

Profesa Muhongo.

Kwa mujibu wa chanzo kutoka ndani ya Taasisi ya Kuchunguza na Kupambana na Rushwa (Takukuru), watu wote wazito waliowahi kushika nafasi nyeti katika Wizara ya Nishati na Madini, wakiwemo mawaziri, manaibu wao, makatibu wakuu na vigogo kutoka TMAA na makamishna wa madini waliojihusisha na usafirishaji wa mchanga nje ya nchi, watalazimika kufika mbele ya chombo hicho ili kuhojiwa juu ya mchakato huo, ambao unadaiwa kufanywa kwa muda mrefu tangu kuanza kwa ‘biashara’ hiyo, mwaka 1998.

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, George Simba chawene.

“Hakuna mtu atakayepona kwenye hii ishu, na uzuri wa hili jambo ni kwamba inafahamika ni kiasi gani cha mchanga kimeshasafirishwa kwenda nje, akina nani walihusika kuikagua, kiasi gani cha madini kilitajwa kuwemo, akina nani walikuwepo pale bandarini kuruhusu makontena hayo 277 kupita bila kuangaliwa na vitu vingine chungu nzima, ni suala la muda tu,” alisema mtoa habari wetu na kuongeza;

“Inavyoonekana, mchezo huu ulikuwa unachezwa kwa kushirikisha kada zote, hawa watumishi wa TMAA walikuwa wanachukua vipimo hivyo vya mchanga kwa kutumia maabara zao na zile za Mkemia Mkuu, haiwezekani kwamba watu wadogo tu ndiyo waliokuwa wanajua, hata baadhi ya maofisa wa polisi nao ni miongoni mwa watakaohojiwa, kwa sababu kuna baadhi ya nyakati watu hawa walipaswa kutimiza wajibu wao.”

Mkurugenzi wa Mashtaka na Makosa ya Jinai nchini, CP Robert Boaz.

MAWAZIRI WALIOHUDUMU WIZARA HIYO

Baadhi ya mawaziri ambao wamekuwepo katika wizara hiyo tangu mwaka 1998 ni pamoja na Daniel Yona, aliyehudumu katika uongozi wa serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi na William Ngeleja wakati wa Jakaya Kikwete, Profesa Sospeter Muhongo na George Simbachawene waliohudumu kwa Kikwete.

Aidha, wapo pia makatibu wakuu kadhaa waliopita katika wizara hiyo, lakini wanaofahamika zaidi ni David Jairo na Eliakim Maswi ambao walitikisa zaidi kutokana na skendo mbili zilizotikisa Bunge. Pia mwingine ambaye naye anatazamiwa kuwepo katika ishu hiyo, ni Dalali Kafumu, Mbunge wa Igunga (CCM) ambaye amewahi kuwa kamishna wa madini kwa miaka mingi.

POLISI WANASEMAJE?

Uwazi lilimtafuta Mkurugenzi wa Mashtaka na Makosa ya Jinai nchini, CP Robert Boaz ambaye alipoulizwa kuhusu ishu hiyo, alitema sumu kwa ku sema: “Kazi ya uchunguzi inaendelea vizuri, tutahakikisha kila mmoja aliyewahi kuhudumu katika sekta hiyo anahojiwa.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, ACP Advera Bulimba.

“Kuhusu nani amekamatwa ni masuala ya kiupelelezi siwezi kuyaweka wazi kwa sasa ila kazi imeanza na inaendelea vizuri. Mtu yeyote aliyewahi kufanya kazi katika sekta ya madini, hasa kama inahusiana moja kwa moja na usafirishaji wa mchanga wa madini, basi ni lazima ahojiwe,” alisema Boaz.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, ACP Advera Bulimba naye amethibitisha kuwa wameshaanza kutekeleza kazi waliyopewa na Rais Magufuli: “Kwa sasa tunaendelea kutekeleza maelekezo ya rais,” alisema Bulimba.

Wakati hayo yakiendelea, taarifa kutoka ndani ya Wizara ya Nishati na Madini, zinadai Mtendaji Mkuu wa TMAA, Dominic Rwekaza ameitwa Takukuru tangu Alhamisi iliyopita na kwamba alihojiwa kuhusiana na ishu hiyo.

Viongozi wengine waliowahi kuhudumu TMAA ni Andrew Makangala, Elikana Petro, Emmanuel Sumay, Jumanne Mohammed, Shamika Gilay, Thadei Sijaona, Venance Bahati na Mvumilwa Mwarabu. Haijajulikana kama nao wataitwa na itakuwa lini.

BOSI TAKUKURU APIGILIA MSUMARI

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Valentino Mlowola, hakuweza kupatikana mara moja kuthibitisha kuhojiwa kwa bosi huyo lakini afisa mmoja wa TMAA alithibitisha.

Hata hivyo, akizungumza na wana habari wiki iliyopita Mlowola alipigilia msumari kwani alisema agizo la Rais Magufuli la kuchunguzwa kwa vigogo wote wa wakala wa ukaguzi wa madini, litafanyiwa kazi kwa haraka pasipo kumuacha mtu yeyote anayepaswa kuhojiwa.

“Kosa la jinai halina muda wala ukomo, wale ambao walikuwepo wizarani kitengo cha madini na kwa sasa hawapo nao tutawafuatilia popote walipo,” alisema, Mlowola.

Leave A Reply