The House of Favourite Newspapers

Barua Nzito Kwa Kaka Chuz, Jiangalie Upya!

0
Muigizaji nguli na muongozaji mzuri wa filamu na thamthiliya za Kibongo Tuesday Kihangala.

Nina kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku hii ya leo, na niwashukuru pia wasomaji wangu wote ambao wamekuwa wakinipa maoni na ushauri kuhusu safu hii.

Katika barua yangu ya wiki hii, nitakuwa wa ajabu kama itapita bila kumzungumzia kaka yangu Tuesday Kihangala ambaye wengi tunamfahamu kama Chuz, muigizaji nguli na muongozaji mzuri wa filamu na thamthiliya za Kibongo ambaye awali alifanya vizuri kwenye Jumba la Dhahabu.

Chuz, wewe ni kama shamba ambalo linazalisha wasanii wazuri kwenye tasnia, umefanya hivyo kwa wengi, baadhi yao ni kama akina Winta, Kojaki, Jini Kabula na wengineo. Kwa namna ambavyo Jumba la Dhahabu lilivyoleta waigizaji mahiri, kila mmoja anakuchukulia kama tanuru la kuzalisha vipaji vipya.

Lakini taarifa zilizosambaa kwa kasi wiki iliyopita, zilizokuhusisha na udhalilishaji wa kingono kwa wasichana ambao wapo kambini kule Lushoto kwa ajili ya tamthiliya yako mpya ya Closed Chapter, siyo jambo linaloweza kupita kimyakimya.

Licha ya jambo hilo kuharibu taswira yako kama msanii mkubwa mwenye heshima mbele ya jamii kubwa inayokuzunguka, lakini pia haileti afya kwako kama ‘brand’ ambayo inahitaji wadau wa kufanya nao kazi.

Leo wanaposikia kuwa brand fulani ipo katika skendo ya udhalilishaji watoto, kwa kweli ni jambo ambalo haliwezi kukusaidia kama msanii, lakini pia kama mtu ambaye umeamua kuigeuza sanaa kuwa kazi yako inayokupatia maisha.

Wapo baadhi yao wanasema ni promo ya tamthiliya mpya na wengine wanasema madai hayo ni ya kweli. Lakini majibu ya Chuz mwenyewe wakati akizungumzia suala hili, inaonyesha kuwa anafahamu anayeeneza na sababu za kufanya hivyo anazijua, kwa maana hiyo, aliyetoa taarifa hizi ni mtu anayejua nini anafanya.

Siku zote, tuhuma hubaki tuhuma hadi pale mamlaka zinazohusika zitakapoweza kuthibitisha, lakini kwa mtu muungwana, kule kusemwa tu kwamba jambo fulani baya linafanywa naye, ni kitu tosha cha kumchafua. Chuz umechafuka.

Kitendo cha wasanii wenzako kuunda tume maalum ya kuchunguza madai hayo, inayoongozwa na Mike Sangu ni kielelezo kuwa kilichofanyika kina chembechembe ya ukweli na hili ni jambo baya kwa msanii mwenye malengo kama yako.

Kaka Chuz, hivi ni kama waswahili wanavyosema kuwa shetani alikupitia? Ni ushirikina au kiki ya Closed Chapter?

Ninajua binadamu wana udhaifu katika masuala mengi, yakiwemo ya kingono, lakini linakuwa jambo la kushangaza inapotokea kuwa mtu mmoja anadaiwa kushiriki tendo hilo na idadi kubwa ya wasichana walio pamoja.

Utawazuia vipi watu kuamini kuwa hata hiyo kambi yenyewe kupelekwa Lushoto ilikuwa ni sehemu ya mpango wako wa kuwadhalilisha watoto wa watu kingono?

Kila siku watu wanapiga kelele kuhusu kudumaa kwa tasnia ya filamu, wakidai kuwa waongozaji na wamiliki wengi wa sinema hizo, hutoa nafasi kwa watu wasio na vigezo kwa sababu tu ni ndugu zao, rafiki zao, au michepuko yao.

Kwa sababu kwa mujibu wa madai hayo, msichana aliyekataa kushiriki uchafu huo, alikataliwa kupewa nafasi ya kucheza. Kama ni hivyo, ni wazi kuwa washiriki ni wale tu waliomridhisha bwana mkubwa kingono badala ya wale waliojaaliwa vipaji vya uigizaji.

Jambo lingine baya, Closed Chapter inatoa taswira mbaya kwa washiriki wengine ambao jamii itawaona kama waigizaji wote wa kike walishiriki ngono na Chuz, kitu ambacho kwao ni fedheha.

Ni rai yangu sasa kwa Chuz kutoka hadharani na kuomba radhi kwa mashabiki, hata kama hajafanya, lakini tuhuma peke yake zinatosha kumkimbizia wafuasi wa kazi yake!

BARUA NZITO NA GABRIEL NG’OSHA | RISASI MCHANGANYIKO

Leave A Reply