The House of Favourite Newspapers

Usisahau Ubaharia Kisa Unahodha

0

HAYA tena Anti Naa mwenye maneno ya shombo nimekuja tena, sina tofauti na mnazi unaojiotea ufukweni ambao wakati wote upo tayari juujuu kuchungulia wale wanaovaa vinguo vifupi kudumbukia kwenye maji, hilo nalo neno!

Sina haja ya kukupa salamu maana mwenzio limenifika hapa! Nikisema hapa hata we unajua yaani shingoni kama siyo kwenye koromeo kabisa! Hakuna vitu vinavyokera kama kuwaiga wenzetu ati! Jitu zima linaingia hadi kazini ukiliangalia limevaa nguo safi mchunguze basi humo ndani alichovaa loo!

Chuki chukia, vimba uvimbiwe wala miye hunitishi, hunibabaishi ndiyo kwanza nasonga! Anti Naa chuma cha reli ukigusa lazima ugongwe, upo? Haya niambie mwanakwetu kutwa kuvaa boksa za kiume na wewe mwanaume kuvaa nguo za kike, inahu? Unasahau ubaharia kisa umepewa unahodha, unaona nguo za kiume zina dili unasahau na kuziacha zako!

Naongea na wewe mwanamke mwenzangu usiye na haya! Eti ooh napenda kuvaa za kiume zinanipa uhuru! Unajua uhuru wewe? Ndiyo ulivyofundwa uvae nguo za ndani za mumeo na mumeo avae za kwako? Si naongea na wewe unayenitumbulia macho kama gari linaloshuka kwenye mteremko wa tope bila breki! Haya tuseme umevaa hiyo nguo ya mkeo na kwenda nayo huko kwa wanaume wenzako, bahati mbaya ukainama wenzako wakakuona utasema umerogwa?

Wenzako waliozitengeneza walikuwa na akili zao ndiyo maana zikaandikwa hii ya kiume na hii ni ya kike, hapa paja dogo hapa kubwa, hapa mbele nakshinakshi hapa kamba tena kama kipofu wewe ukawekewa na marinda kabisa kutofautisha! Sa dume zima umejipamba nje suti ndani umevaa bikini, heee heee heeiya! Acha nicheke kwa hasira Anti Naa miye maana nikinuna siku haziendi mwenzangu!

Nikugeukie na wewe mwanamke mwenzangu, mwanamke uliyefundwa ukapitia ngazi zote tena wanakuita konkodi, ukachujwa ukachujika kweli wa kuvaa

nguo za ndani za kiume na kujisifu mtaani? Hata kama umeshauriwa maana hushindwi kujitetea ‘ohh mimi mume wangu anapenda nivae’ hee huyo mumeo kashushwa toka mbinguni! Mwanaume wa timilifu hawezi kupendezwa na hiyo tabia, upo somo?

Shoga badilika mwenzangu, tena badilika na ufundike kweli! Nasema na wewe kwa uso mpana wala sijitii ubaya! Mwana-mke uliyeka-milika huwezi kujisifu kuvaa nguo za kiume tena ume-starehe kama upo peponi, koma tena ukomae! Ngoja nikuulize kitu, hivi ukivaa hizo nguo unatembeaje huko mtaani, haya ukienda maliwatoni kule ambapo mnakutana wengi kwenye misiba na sherehe unavuaje maana jibu limenipitia kushoto mwenzenu!

Ushauri wangu wa bure ni kama maji usipokunywa basi nawa au uoge kabisa! Mwanamke jitambue, usafi siyo kupendeza tu na kuoga mwenzangu, usafi ni pamoja na nguo za ndani. Wanaume waachie zao na wao wajitambue sasa! Kwa leo niishie hapa tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Leave A Reply