The House of Favourite Newspapers

Okwi Apaa Kimya Kimya Kwenda Uganda

0


BAADA ya kiungo mshambuliaji raia wa Uganda, Emmanuel Okwi kuingia kandarasi ya miaka miwili ya kuitumikia Simba, juzi Jumatatu asubuhi aliondoka zake kimya kimya kurudi kwao Uganda huku akiwataka wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo kuwa na utulivu kwani ana mengi mapya ya kuwafanyia.

Okwi ambaye alikuwa akiitumikia SC Villa ya nchini kwao, Jumapili iliyopita alisaini mkataba huo ikiwa ni siku moja baada ya kuwasili nchini. Okwi ameondoka baada ya kumalizana na Simba ambayo imeelezwa imemlipa ‘mzigo wote keshi’ ili asaini kuichezea tena timu hiyo.

Okwi aliliambia Championi Jumatano kuwa, anaondoka kwenda kwao lakini atarudi nchini muda wowote Simba itakapoanza maandalizi yake ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara. “Sipendi kuwa mzungumzaji sana ila ninachoweza kukisema hapa ni kuwataka mashabiki wangu wote kuwa kimya maana tayari nimeshaingia mkataba wa kuitumikia Simba, hivyo kwa kushirikiana na wengine wote waliopo, wao watarajie mambo mengi mapya kutoka kwetu,” alisema Okwi.

Wakati huohuo, Okwi kupitia mtandao wa Simba, amewataka wapenzi wa timu hiyo kumuunga mkono katika kipindi chote atakachokuwa na klabu hiyo na akawahakikishia kuwa makali yake aliyokuwa nayo hapo zamani, bado yapo vilevile. “Makali yangu bado hayajaisha, yapo vilevile  kama zamani kwa hivyo Wanasimba wasiwe na wasiwasi na hilo.

“Ninaamini kabisa nitaendelea kuifunga Yanga kama ilivyokuwa kipindi kile tulipofunga 5-0. “Kwa hiyo, naamini kabisa hata msimu ujao makali hayo yatakuwepo kutokana na usajili ambao mpaka sasa Simba imeshaufanya kwani wachezaji wengi iliowasajili ni wazuri na ninaujua uwezo wao, kwa hiyo Wanasimba wajiandae kufurahi,” alisema Okwi. Mpaka kufikia jana, Okwi alikuwa ni mchezaji wa nane kutangazwa hadharani kusajiliwa na klabu hiyo msimu huu. Wengine ni John Bocco, Shomary Kapombe, Aishi Manula, Jamal Mwambeleko, Ally Mshomary, Yusuph Mlipili na Emmanuel Mseja.

(Musa Mateja na Sweetbert Lukonge | Championi)

Leave A Reply