The House of Favourite Newspapers

Hakuna aliyekamilika, Cha Muhimu ni Kuvumiliana

0

UHALI gani msomaji wangu! Ni matumaini yangu kuwa uko poa kabisa. Ni ijumaa nyingine nzuri ninayokualika kwenye uwanja huu, kwa wewe ambaye mambo yako hayaendi sawa, nakuombea kwa Mungu akufanyie wepesi. Mada yetu ya leo ni kama inavyojieleza, wapo baadhi ya watu ambao wao kamwe hawakosei, kila tatizo linapotokea basi wanawasukumia mizigo wenzi wao, wanaamini wao ni wakamilifu ila wenzi wao ndiyo wana matatizo.

 

Ipo wazi kwamba uhusiano wa kimapenzi ni jambo ambalo linatakiwa kuwa la furaha, wewe na mwenzi wako muishi kwa upendo na amani, hata kama kunatokea misuguano, basi inakuwa ni ile ya kawaida ambayo mnaimaliza mapema, kwa amani na maisha yanaendelea. Kwa bahati mbaya, uhusiano wa kimapenzi wa watu wengi siku hizi, umejawa na migogoro, maudhi na karaha za mara kwa mara, hasa kwa wale wapenzi wanaoishi kwenye uhusiano wa kudumu, uwe ni uchumba au ndoa.

 

Jambo ambalo watu wengi huwa hawalijui, ni kwamba amani, upendo na maelewano huwa haviji tu, ni lazima vijengwe na wa kufanya hivyo ni wewe na mwenzi wako.

Ukiwauliza watu wengi ambao wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi usio na amani wala upendo, uliojaa maudhi, migogoro, ugomvi na kila aina ya karaha, watakimbilia kuwatupia lawama wenzi wao kwamba wao ndiyo chanzo cha yote hayo. Usichokijua ni kwamba mpenzi wako siyo malaika, ni binadamu kama wewe kwa hiyo lazima atafanya makosa, na wewe lazima utafanya makosa tu. Hakuna aliyekamilika, kinachotakiwa ni kuwa na moyo mwepesi wa kusamehe na kuwa mvumilivu kwa sababu huwezi kumpata mke au mume asiye na kasoro hata moja. Yawezekana kweli mwenzi wako ana

Mawasiliano matatizo, sawa! Lakini vipi kuhusu wewe? Huwa unajikagua na kuona makosa yako au kwa kila kinachotokea mwenzako ndiyo anakuwa na matatizo? Mother Theresa, amewahi kutoa nukuu moja ambayo ni maarufu sana; ukiwa mwepesi wa kuwahukumu wengine, huwezi kupata muda wa kuwapenda. Maana yake ni nini? Ukiwa mwepesi wa kutazama makosa ya mpenzi wako kuliko yale mazuri anayokufanyia, huwezi kumpenda! Hilo tu ni kosa linalotosha kuvunja uhusiano wenu.

 

Unapoacha kumpenda mwenzi wako kwa kutazama mabaya yake unafikiri nini kitatokea? Na unapotumia muda mwingi kumhukumu, umesahau kwamba na wewe ni binadamu ambaye hujakamilika kwa hiyo ni lazima kwa namna moja au nyingine unafanya makosa? Ninachotaka kukwambia msomaji wangu, kama umeamua kuishi na mwenzi wako, lazima utambue kwamba yeye siyo malaika, wewe pia siyo malaika. Yeye atafanya makosa, na wewe pia utafanya makosa.

 

Kama wewe ni muungwana, inapotokea amekukosea kwa jambo fulani, badala ya kutumia hiyo kama fimbo la kumchapia, kaa chini na zungumza naye kwa upole, mweleze jinsi unavyochukizwa na mambo anayokufanyia. Kama anakupenda kweli atabadilika. Hata kesho ikitokea na wewe umefanya makosa, na yeye hatakuhukumu, atakaa na wewe, atakueleza ulichomkosea na mtamaliza tofauti zenu. Lakini akifanya kosa dogo ukamhukumu utafikiri ameua, kesho na wewe ukikosea hata jambo dogo, lazima na yeye atakuhukumu, hata kama atashindwa kukuonesha lakini tambua lazima atafanya kitu kukuhukumu, mwisho unafikiri amani itakuwepo? Unapotaka kushughulikia amani ya penzi lenu, anza kwanza kwa kujikagua wewe mwenyewe. Ukishatambua kwamba kuna makosa huwa unayafanya, jitahidi kuyarekebisha, na yeye akikosea tambua kwamba siyo malaika, msamehe mara nyingi kadiri uwezavyo na endelea kumpenda, hiyo ndiyo siri kubwa ya mapenzi yenu kudumu! Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

 

Leave A Reply