The House of Favourite Newspapers

Okwi: Kwa Simba Hii, Ubingwa Mapema

0
Mshambuliaji mpya wa Simba Mganda, Emmanuel Okwi.

MSHAMBULIAJI mpya wa Simba Mganda, Emmanuel Okwi ametoa kauli ya kishujaa baada ya kutamka kuwa atapambana kufa au kupona kuhakikisha timu yake inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mapema tu.

Okwi raia wa Uaganda, ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Simba kuifunga Rayon Sports ya Rwanda kwa bao 1-0 lililofungwa na Mohammed Ibrahim ‘Mo’ mapema wiki hii katika mchezo wa kirafiki.

Mshambuliaji huyo ni miongoni mwa wachezaji wapya wa Simba, ambapo amesajiliwa kwa dau la dola 50,000 (Sh milioni 112) kutoka SC Vila ya Uganda.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Okwi alisema kutokana na jinsi alivyokiona kikosi chao hadi sasa, ahadi anayoitoa kwa mashabiki wa timu hiyo ni kuhakikisha wanatwaa ubingwa.

Okwi alisema, anafurahia uwepo wa baadhi ya wachezaji wenye uwezo na uzoefu mkubwa wa kucheza michuano ya ligi kuu na michuano ya kimataifa. Simba itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Alisema kwa kushirikiana na wenzake, anaahidi kuipambania Simba ili itwae ubingwa wa ligi kuu ambao mashabiki wana kiu nao baada ya kuukosa kwa miaka mitano ukienda kwa Yanga mara tatu na Azam FC mara moja.

“Nawashukuru Wanasimba kwa mapokezi waliyonipa tangu nimetua kujiunga na timu yangu hii niliyoichezea kwa vipindi viwili huko nyuma.

“Nimepanga kulipa fadhila kwa kuipambania timu kwa moyo mmoja kufa au kupona kuhakikisha inatwaa ubingwa wa ligi kuu mapema tu.

“Na hilo linawezekana kabisa kutokana na ubora wa kikosi chetu tulichokuwa nacho hivi sasa, ninafurahia kuona wachezaji wenye uzoefu na uwezo wa kupambana katika michuano ya kitaifa na kimataifa,” alisema Okwi.

Okwi anatarajiwa kuichezea Simba dhidi ya Yanga Agosti 23, mwaka huu katika mechi ya Ngao ya Jamii kabla ya kuanza kwa ligi kuu Agosti 26, mwaka huu.

Leave A Reply