The House of Favourite Newspapers

Ama Huku Ama Kule, Simba vs Yanga

0
Kikosi cha timu ya Yanga.

MSIMU wa 2017/18, unafunguliwa leo Jumatano kwa mchezo wa Ngao ya Jamii utakaozikutanisha Simba na Yanga ambao utapigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.

Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi bora wa msimu uliopita, Elly Sasii, huku Ferdinand Chacha na Hellen Mduma wakiwa wasaidizi wake na Israel Nkongo akiwa mwamuzi wa akiba.

Shabiki mpya wa Yanga, Mack Yanga.

Wakati timu hizo zikijiandaa na mechi hiyo, zilikwenda kupiga kambi Zanzibar ambapo Simba ilikuwa Visiwa vya Unguja na Yanga ikajichimbia Pemba.

Makocha wa timu hizo zote mbili, wamezungumza na Championi Jumatano kuhusiana na mechi hiyo inayobeba hisia za mashabiki wengi wa soka wa ndani na nje ya Tanzania.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina, alisema: “Tunacheza mechi ya kwanza kabisa ya msimu wa 2017/18 dhidi ya Simba katika Ngao ya Jamii, hiyo ni nzuri kwetu kwani kuanza tu msimu unakutana na timu nzuri inakuwa kipimo tosha kwako.

Wachezaji wa Simba wakiwa katika mazoezi.

 

“Wao wamefanya usajili mzuri na sisi pia tumesajili vizuri, siku hiyo tutapima vikosi vyetu, lakini kwa upande wangu baada ya mchezo huo nitajua kikosi changu kina uwezo kiasi gani na msimu huo tutafanya nini.”

Baadhi ya nyota wapya wa Yanga ambao wanatarajiwa kucheza mechi ya leo ni Ibrahim Ajibu, Papy Kabamba Tshishimbi, Raphael Daud na Gadiel Michael.

Kwa upande wa Simba, kocha mkuu wa kikosi hicho, Joseph Omog, raia wa Cameroon, amesema: “Katika zile mechi zetu za kirafiki, nilikuwa nikiwajaribu wachezaji wangu wote kuona mfumo gani nitautumia ambao utakuwa rahisi kutupatia matokeo mazuri, na tayari hilo nimeshamaliza, kwa sasa siwezi kusema moja kwa moja nani na nani watakuwa kwenye kikosi cha kwanza.

Wakiwa hoi baada ya mazoezi.

“Niseme tu kwa sasa tupo tayari kwa ajili ya kucheza na Yanga, kwa sababu maandalizi yote yamekamilika kwa asilimia zote. Hatuna presha na wapinzani wetu kwa sababu natambua huko nyuma tumeshacheza nao na tumepata matokeo mazuri mbele yao, imani yangu ni kwamba lazima tutapata matokeo mazuri tena.”

Simba inatarajiwa kuongozwa na nyota wake wapya kama Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, Aishi Manula, Ally Shomary na wengineo.

Kwenye mchezo huu, Kocha wa Yanga, George Lwandamina ataingia akiwa na nia ya kutaka kulipa kisasi mbele ya mpinzani wake, Joseph Omog wa Simba kutokana na mara ya mwisho kukutana aliambulia kichapo cha mabao 2-1.

Yanga itamkosa Mzambia, Obrey Chirwa, Benno Kakolanya na Geofrey Mwashiuya ambao wote ni majeruhi. Kwa upande wa Simba, Shomary Kapombe ambaye ni majeruhi muda mrefu atakosekana, huku John Bocco akiwa na hatihati ya kucheza kutokana na hivi karibuni kupata majeraha.

Stori; Omary Mdose | Championi Jumatano

Leave A Reply