The House of Favourite Newspapers

Magonjwa Ya Tetenasi Na Kisonono Kwa Watoto

0

KISONONO KWA WATOTO

Inafahamika kwamba kisonono (gonorrhea) huwapata watu waliofanya ngono zembe lakini umewahi kusikia kwamba ugonjwa huu pia unaweza kuwapata watoto?

Watoto pia wanaweza kupata ugonjwa huu, kutoka kwa mama wakati wa kujifungua. Kama mwanamke mjamzito ana ugonjwa huu, inashauriwa atibiwe mapema na hilo lisipofanyika, lazima mtoto ataambukizwa wakati wa kuzaliwa.

Madaktari na manesi katika hospitali nyingi, hivi sasa wana utaratibu wa kuwapaka dawa ya kuzuia bakteria (antibiotics) watoto wote, ndani ya saa moja tangu kuzaliwa ili kuwalinda na kisonono na magonjwa yanayofanana na hayo ambayo kitaalamu huitwa Neonatal Conjunctivitis.

DALILI ZAKE

-Maumivu makali ya macho ambayo husababisha yawe mekundu na kuvimba

-Kutokwa na uchafu machoni ambapo mtoto hutokwa na matongotongo mengi, wakati mwingine hutokwa na usaha machoni.

-Mwili kuchemka na kupata homa kali, hali ambayo husababisha mtoto awe analia muda wote.

Kwa kawaida, dalili hizi huonekana kuanzia kipindi cha siku tano tangu mtoto alipozaliwa na kuendelea.

MATIBABU

Kama ilivyo kwa watu wazima wanaopatwa na kisonono, ugonjwa huo kwa watoto hutibiwa kwa dawa za antibiotics kama erythromycin, tetracycline, Silver Nitrate na nyingine kama hizo. Hata hivyo, wazazi wanashauriwa kutowapa watoto wao dawa yoyote mpaka watakapoonana na daktari ambaye atampima mtoto na kumuandikia dawa inayomfaa mtoto kulingana na umri na uzito wa mwili wake.

ANGALIZO

Ugonjwa huu usipotibiwa haraka na kwa ukamilifu, husababisha upofu wa kudumu kwa hiyo wazazi wanapaswa kuwa makini na watoto wao, ukiona dalili haraka muwahishe mtoto hospitalini.

  1. TETENASI KWA WATOTO

Tetenasi (Tetanus) ni ugonjwa unaoweza kumpata mtu yeyote lakini hapa tutauzungumzia zaidi kwa watoto kwa sababu ndiyo wanaosumbuliwa zaidi na ugonjwa huu.

Kutokana na michezo yao, mara kwa mara watoto hujijeruhi miili yao kwa vitu vyenye ncha, kama misumari, mabati yenye kutu, chupa na vitu vinavyofanana na hivyo. Ni kupitia majeraha hayo, ndipo bakteria waitwao Clostridium tetani wanapoingia mwilini ni kusababisha ugonjwa wa tetenasi. Bakteria hawa huishi kwenye vumbi, udongo na samadi.

DALILI

Dalili za awali za tetenasi kwa watoto, ni mwili kukakamaa, hali ambayo hutokea mara tatu au nne kwa wiki, mwili kutokwa na jasho jingi, kuumwa kichwa, homa kali, kupata shida kumeza chakula na mapigo ya moyo kwenda mbio.

Kukakamaa kwa misuli ya mwili, hutokea kwa sababu bakteria hao wanapoingia ndani ya mwili, huzalisha sumu ambayo huenda kuvuruga utaratibu wa namna misuli inavyofanya kazi.

Wengi huchanganya dalili za tetenasi kwa watoto na degedege, hata hivyo ni magonjwa mawili tofauti.

Kwa kawaida, dalili za tetenasi huanza kuonekana kuanzia siku tatu hadi 21 tangu mtoto alipopata jeraha kisha bakteria kuingia kwenye mwili wake. Utafiti unaonesha kuwa asilimia 10 ya watu wanaopatwa na tetenasi, hupoteza maisha.

MATIBABU

Kwa kawaida, mtoto anapozaliwa hupewa chanjo ya magonjwa mbalimbali, ikiwemo tetenasi. Hata hivyo, inapotokea mtoto amepatwa na ugonjwa huu hutibiwa kwa dawa iitwayo Globulin (intravenous immunoglobulin- IVIG). Pia dawa za kulainisha misuli hutumika kuzuia tatizo la mwili kukakamaa.

Endapo utaona mtoto ana dalili kama zilizotajwa hapo juu, unatakiwa kumuwahisha hospitalini. Pia wazazi wanashauriwa kujenga utaratibu wa kuwakagua watoto wao wanapotoka kucheza, ili kama wana majeraha, wakachomwe sindano za kuzuia tetenasi haraka kabla ya ugonjwa haujaibuka.

MWANDISHI WETU NA MTANDAO

PRINCE DULLY PARTY!! Mashauzi ya Mobeto ya Kumchokonoa Zari

Leave A Reply