The House of Favourite Newspapers

Dogo Janja Anakimbia Kivuli Chake!

0
Muziki wa Bongo Fleva, msanii Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’.

MCHANA wa Ijumaa ya Desemba 24, 1993 hali ya hewa ikiwa ya manyunyu kwa mbali, katika jumba moja lililopo Pawling jijini New York, Marekani mwanamama Ruth alimshuhudia mumewe, Mch. Dk. Norman Vincent Peale pembeni ya kitanda akikata roho baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kisukari.

 

Lilikuwa pigo kubwa kwa kuwa licha ya kufariki akiwa na miaka 95, Norman alikuwa ‘kichwa’ tangu akiwa mmoja kati ya mawaziri nchini Marekani, mchungaji, mhamasishaji na mtunzi mahiri wa vitabu vya kuhamasisha watu kujikomboa na umasikini duniani.

 

Norman ndiye muanzilishi wa msemo na mbinu ya mawazo chanya (kujiongeza), moja kati ya vitabu vyake vinavyoendelea kusomwa kwa wingi duniani ni The Power of Positive Thinking.

 

Katika majukwaa ya uhamasishaji na vitabu vyake alikuwa akipenda kusema kwamba; ‘Believe in yourself! Have faith in your abilities! Without a humble but reasonable confidence in your own powers you cannot be successful or happy.’

(Jiamini! Kuwa na imani na uwezo wako, ukiwa na ujasiri bila unyenyekevu, kamwe huwezi kuwa na furaha wala kufanikiwa.)

Tukija kwenye Muziki wa Bongo Fleva, msanii Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ ni miongoni mwa wakali wa muziki huo ninaowakubali ukiachana na madogo wenzake, Young Killer na Young Dee.

 

Nimeanza kumjua Dogo Janja tangu enzi hizo ana-rap huko kwao Ngarenaro akiwa na wasanii kama Gentriez Mwakitabu, Rodgers na wengineo kabla ya kuonwa na Madee.

Ulimwengu wa Bongo Fleva, ulimtambua baada ya kutambulishwa na Kundi la Tip Top Connection mwaka 2012, kupitia kwa kinara wake, Madee aliyemtoa Ngarenaro mikononi mwa wazazi wake na kumuunganisha na wakali wengine wakiwemo Tunda Man na Keisha.

 

Niwe mkweli, dogo anaweza kurap. Lafudhi yake ya watoto wa Kiarusha inamuongezea ‘credit’ katika muziki wake, kwa sababu nayo ni kitambulisho kingine cha uwepo wake.

Wakati akitambulishwa, Madee aliwaahidi mashabiki kuwa atamlea Dogo katika njia inayofaa, ikiwa ni pamoja na kumkuza kisanii na kielimu.

Simulizi zinasema alipelekwa Makongo Sekondari jijini Dar es Salaam. Ghafla ukaibuka mzozo mkubwa baina ya Dogo na Madee, uliosababisha Chalii kurudi zake Arusha. Sina sababu ya kurudia maneno yaliyoibuliwa na pande zote mbili.

Lakini kifupi Dogo Janja alilia kufanywa mgodi, akitumika kumten-genezea hela Madee, kwamba alipiga shoo nyingi, lakini kipato akawa hakioni, kinaishia kwa mkubwa. Na Madee naye alifunguka, akimlaumu Dogo kwa kuzuzuka na jiji, kuacha shule na tabia nyingine mbaya.

 

Kwa sababu zilizo wazi, watu wengi walimuunga mkono Dogo, wakamsifu kwa kujitambua. Lakini bahati mbaya, baada ya kutoka Tip Top, akadondokea

Watanashati Entertainments akiungana na PNC ambako baadaye taarifa zilisema alifukuzwa kwa makosa yanayofanana na yale yaliyowahi kutolewa na Madee.

Mwisho wa ‘picha’, Dogo aliamua kurudisha majeshi kwenye kambi yake ya zamani ya Tip Top iliyomtoa na kumlea.

Tangu kurudi kwake, amekuwa ni mtu wa kutoa ngoma weka ngoma. Madee alimpeleka MJ Records chini ya Prodyuza Daxo Chali na kufanikisha kuibuka na ngoma ya My Life iliyoteka hisia za mashabiki wengi, haikukaa sana akaibuka na nyingine ya Kidebe, ikabamba!

 

Hakuishia hapo, alidhihirisha uwezo wake baada ya kuibuka na ngoma nyingine ya Ukivaaje na sasa ameamua kukumbuka kwao kwa kutoa Ngoma ya Ngarenaro.

Kwa maisha aliyopitia, Dogo ameonesha ni mtu wa kujiamini na jasiri, ni sekta moja ambayo inataka kumrudisha nyuma na kufuta mazuri yote aliyoanza kuyaweka sawa.

Takribani mwezi sasa unakatika, Dogo Janja (miaka 20) ameteka vichwa vya habari kwa kuwaaminisha ‘raia’ kuwa amefunga ndoa na msanii wa filamu Bongo, Irene Uwoya (miaka 30).

Ukiliangalia jambo hili kwa haraka unaweza kukubali kwa shingo upande, picha za harusi na vipande vya video vinavyomuonesha dogo amechukua ‘jiko’ vinaleta makengeza ya kuamini na kutoamini.

Katika media, Dogo akiulizwa jibu lake linabaki kuwa amefunga ndoa. Jibu hilo pia unalipata kwa Madee ambaye naye anapigilia msumali kuwa dogo kweli amemuoa Uwoya.

Ikumbukwe kuwa, Uwoya yupo katika ndoa ya Kikristo na Ndikumana, hajawahi kupewa talaka na hata katika mahojiano na media hajawahi kuanika ukweli kuwa amefunga ndoa na Dogo zaidi ya kusema ilikuwa ni kipande cha filamu.

Kwa mantiki hiyo, Dogo Janja anakimbia kivuli chake mchana kweupe. Anatumia nguvu nyingi kujaribu kuwaaminisha raia kuwa amechukua jiko wakati ni sehemu ya filamu inayotarajiwa kuanza kuoneshwa.

Kama anavyosema mhamasishaji Norman, inavyoonekana Dogo hataki kuamini uwezo wake katika muziki mpaka atumie nguvu ya ziada. Amekuwa ni jasiri aliyekosa unyenyekevu na kujiamini katika kazi zake.

 

Yapo madai kuwa, Dogo ‘amechikichia’ fungu f’lan la mshiko pamoja na bosi wake na baadhi ya mastaa walioshiriki ili waipaishe filamu hiyo, ni sawa lakini mbona Uwoya ameweza kuwaaminisha watu kwa video na picha lakini si kwa maneno na kuingia kwenye media?

 

Huenda anachokifanya Dogo kwa sasa asione madhara yake mara moja lakini baada ya filamu kutoka kama asemavyo Uwoya kuwa haikuwa ndoa kweli, akaaibika zaidi! Tusubiri tuone!

Mwandishi wa makala haya ni mdau na mchambuzi wa masuala ya burudani. Anapatikana kwa namba +255 713 133 633.

Leave A Reply