Okwi, Juuko Wawazimia Simu Viongozi
WAGANDA, Emmanuel Okwi na Juuko Murshid, wameanza vituko ndani ya timu hiyo baada ya kwenda kwao na kuchelewa kurudi kujiunga na wenzao wanaojiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Prisons.
Simba ambayo ipo jijini Mbeya, itawakosa nyota hao katika mchezo wao wa kesho Jumamosi ambapo Okwi ni majeruhi, huku Juuko akiwa ni mzima, lakini hajaungana na wenzake.
Wawili hao waliondoka wiki mbili zilizopita kwenda kujiunga na timu yao ya taifa iliyokuwa inajiandaa na mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Congo Brazzaville.
Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya kambi ya timu hiyo iliyopo Mbeya, zinasema kwamba, wachezaji hao haijulikani lini watarejea huku simu zao zikiwa hazipatikani.
“Bado Okwi na Juuko hawajarudi kambini tangu walipoenda kwao kujiunga na timu ya taifa, na mpaka sasa simu zao hazipatikani hivyo taarifa zao za lini watarejea hazifahamiki,” alisema mtu huyo.
Alipotafutwa mratibu wa timu hiyo, Abass Ally, alisema: “Juuko na Okwi kweli hawajafika na sina taarifa zao, hivyo siwezi kusema lolote.”
Stori: Musa Mateja | Global Publishers