The House of Favourite Newspapers

Barua Nzito: Ferooz Usijidanganye Mwenyewe!

0
Msanii nguli wa Bongo Fleva, Ferooz.

HABARI za leo mabibi na mabwana. Kwa rehema zake Mwenyezi Mungu ni imani yangu kuwa wote tumeamka salama na tunaendelea na jukumu letu kubwa la kulijenga taifa letu kupitia kauli mbiu yetu ya Hapa Kazi Tu!

 

Nizidi kuwashukuru wapendwa wasomaji wa safu hii kwa namna tunavyokwenda sambamba katika kuiboresha kwani kama ninavyosema kila siku, lengo letu ni kuwekana sawa pale tunapoona wadau wetu wanaenda ndivyo sivyo, kuelimisha, kuonyana na bila kusahau kukumbushana.

 

Ni kwa muktadha huo, leo nimeona niseme na ndugu yangu, kaka yangu, msanii nguli wa Bongo Fleva, Ferooz Mrisho ambaye ni mmoja wa wasanii waliounda kundi maarufu la Daz Nundaz, ambalo lilisheheni vijana wenye vipaji, wakiwemo Daz Mwalimu na Daz Baba.

 

Katika wasanii ambao waliweza kuitendea sauti yake haki, huyu ni mmoja wao kwani alifanya vyema kiasi cha kumfanya kuwa juu isivyo kawaida enzi zake.

Lakini kama ambavyo vijana wengi wa Bongo Fleva wanaanguka, ni ile tabia yao ya kujaribu kila kitu kinachofanywa na wasanii wa nje. Ferooz alijiingiza kwenye madawa ya kulevya na kuwa teja, kitu ambacho kilichangia sana kumtoa katika ramani.

 

Na jambo hili lilimfanya kuwapoteza marafiki wengi aliojitengenezea enzi zake, hivyo kujiona kama mtu aliyetengwa. Mara kadhaa, alikuwa akikataa kula ‘unga’ lakini siku zote, mla ngada hajifichi.

 

Baada ya kupotea kwa muda mrefu, alijaribu kurudi kwa kubadili staili, badala ya Bongo Fleva, akaja na Mnanda kwa kile kibao chake cha Ndege Mtini. Kama kawaida yake, aliwaomba mashabiki kumpa sapoti, akitoa ushuhuda kuwa kuwepo kwake nje ya ‘game’ kumempa mafunzo mengi hivyo hatarajii kurudia makosa.

 

Majuzi, ametambulisha kibao chake kingine cha Nakaza Roho na kama kawaida yake, amerejea wito wake kuwa anawaomba mashabiki wajitokeze kumpa sapoti, kwani bado anajiona kama mtu anayehitaji zaidi mashabiki ili aweze kurejea kwenye ramani.

 

Niseme kitu kimoja, muziki na matendo binafsi ya msanii ni vitu viwili tofauti. Nimeisikiliza kazi hii mpya ya Ferooz, ipo vizuri na kama mashabiki wataitikia wito wake wa sapoti, bila shaka itafanya vizuri sokoni.

 

Lakini kuna jambo moja la msingi ambalo linataka msanii Ferooz ajitambue mwenyewe. Kuna kipindi, aliwahi kusema inamuwia vigumu kuachana na madawa ya kulevya kutokana na kitu hicho kumsukuma kila mara ili aendelee kutumia.

 

Lakini hivi karibuni pia ameibuka na kutoa madai ya ‘kukimbiwa’ na washkaji zake, Profesa Jay na Chegge. Alisema ingawa ukweli anawasiliana na watu hao, lakini sivyo kama ambavyo ilipaswa kuwa.

 

Nimwambie kitu Ferooz, heshima anayoitaka katika muziki, itarudi iwapo tu, ataamua kuachana kabisa na madawa ya kulevya kwa sababu siku zote hayakuwahi kumuacha mtu salama.

 

Mashabiki wanaweza kujitoa kununua kazi zake kwa nguvu zote, lakini ‘kula unga’ kutamharibia.

Licha ya unga kuondoa heshima ya mtumiaji, lakini pia inahusisha fedha. Hii maana yake ni kuwa wakati mashabiki watanunua kazi zake ili apate pesa za kurekebisha maisha yake, yeye atazipeleka kwenye madawa, kitu ambacho kitawachosha.

 

Kwa jinsi nilivyokuona mara ya mwisho juzikati, ni wazi kuwa umepunguza kwa kiwango kikubwa matumizi ya madawa hayo, hivyo ni dhahiri kuwa uwezekano wa kuachana nayo kabisa upo.

 

Huwezi kuwa mla ‘poda’ halafu ukategemea marafiki zako waendelee kuwa walewale. Utaishia kuwalalamikia tu wakati ni wewe mwenyewe unawafukuza. Usijaribu kujidanganya mwenyewe, ukijitambua kila kitu kitakuwa rahisi!

BARUA NZITO NA GABRIEL NG’OSHA | RISASI MCHANGANYIKO

Leave A Reply