The House of Favourite Newspapers

Kafulila Asema Hajaamua Chama Cha Kujiunga Nacho (Video)

0
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) David Kafulila.

ALIYEKUWA mbunge wa Kigoma Kusini tangu 2010-15 na baadaye kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) David Kafulila, amesema kwamba pamoja na kutangaza kukihama chama chake hicho, bado hajaamua chama ambacho atajiunga nacho, lakini akasisitiza kwamba ajenda ya ufisadi aliyokuwa anaipigania upande wa upinzani imetoweka na sasa anatafuta sehemu ya kuiendeleza.

 

Kafulila aliyasema hayo wakati akihojiwa na Global TV Online jijini Dar es Salaam leo, ikiwa ni siku moja tangu atangaze uamuzi wa kuondoka Chadema.

 

“Hilo ni jambo la kawaida kwa wanasiasa duniani kuhama wakati wanatetea ajenda zao,” alisema Kafulila ambaye alipata tuzo akiwa mbunge wa kwanza kuendesha harakati  dhidi ya ufisadi  Aprili 29, 2015.

 

Aliongeza kwamba msimamo wake wa kupiga vita ufisadi tangu utotoni hadi kuingia bungeni uko palepale na atauendeleza akiwa katika chama chochote.

 

Kuhusu madai  kwamba hana imani na upinzani ambako umeshindwa kupambana na ufisadi, wakati ndipo alipopatumia kujiimarisha katika vita hiyo, mwanasiasa huyo machachari alisisitiza kwamba  ajenda ya kupiga vita ufisadi imekufa katika vyama hivyo na ameona hakuna tena matumaini ya kuifufua ajenda hiyo ambayo awali ilikuwa ndiyo nembo ya upinzani.

 

Pia Kafulila alikanusha mawazo kwamba ameondoka chama hicho baada ya kukosa maslahi kwa kutopata cheo,  ambapo amesema kama ni vyeo bado nafasi zipo Chadema na watu wanajitokeza kuvigombea, jambo ambalo yeye hakulifanya wakati akiwa huko.  Kwa hiyo, akasisitiza kwamba suala la kutopata cheo katika chama hicho siyo lililomfanya ajivue uanachama.

 

Hata hivyo, wakati akisubiri chama cha kujiunga nacho, alimsifia  Rais John Magufuli kwamba  amejipambanua katika suala la kuupiga vita ufisadi na anakubalika ndani na nje ya nchi na kwamba watu wengi wanakubaliana na hatua anazozichukua.

 

Kafulila alikuwa mwanachama wa Chadema baadaye akajiunga na NCCR-Mageuzi, akarejea tena Chadema hadi alipojivua uanachama jana.

NA WALUSANGA NDAKI

Leave A Reply