Matokeo Ya Simba Yawatisha Yanga
BAADA ya juzi Ijumaa Simba kutupwa nje ya Kombe la Shirikisho (FA) na Green Warriors, watani wao Yanga wamefunguka kuwa wenyewe watafanya kweli kwenye mchezo wao wa leo wa kombe hilo dhidi ya Reha FC.
Yanga ambao watamkosa kocha wao mkuu, George Lwandamina leo Jumapili watakuwa na kibarua cha kuvaana na Reha FC kwenye muendelezo wa michezo ya FA. Mchezo huu utapigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa ameliambia Spoti Xtra kuwa: “Tuko vizuri kuelekea mechi yetu hii na Reha FC, kama benchi la ufundi tumewapa mafundisho wachezaji juu ya umuhimu wa mechi ili isije kutokea yale ambayo yaliyowakuta wenzetu Simba, walipocheza na Green Warriors.
“Wachezaji wetu ni watu wazima tunaamini kwamba wametuelewa na watafanya kweli, tunataka tupate ushindi kwa ajili ya kusonga mbele kwenye mashindano haya,” alisema Nsajigwa.
Simba walikutana na kichapo cha penalti 4-3 na Green Warriors juzi na kuondolewa kwenye michuano hiyo ya pili kwa ukubwa hapa nchini.
Comments are closed.