×

Maajabu Ya Airbus A380-800 Yanayowashangaza Watu Duniani

Ndege ya Airbus A380-800 imeendelea kutajwa kuwa moja ya ndege kubwa na za kipekee kuwahi kutengenezwa duniani kutokana na ukubwa wake, teknolojia ya kisasa pamoja na huduma za kifahari zinazowavutia wasafiri wengi duniani.

A380 ndiyo ndege kubwa zaidi ya abiria kuwahi kutengenezwa na pia ndiyo ndege ya kwanza duniani yenye ghorofa mbili kamili kwa ajili ya abiria kutoka mbele hadi nyuma.

Ndege hiyo ilianza rasmi safari zake za kibiashara mwaka 2007 ikiwa na lengo la kubeba idadi kubwa ya abiria kwa safari za masafa marefu huku ikitoa kiwango cha juu cha faraja angani.

Ndege hiyo inaweza kubeba hadi abiria 853 ikiwa itapangwa kwa mfumo wa daraja moja la uchumi, ingawa mashirika mengi ya ndege hutumia mfumo wa madaraja tofauti unaobeba kati ya abiria 500 hadi 600 ili kuongeza nafasi na huduma bora kwa wasafiri.

Ndege ya Airbus A380-800 ina zaidi ya maili 300 za nyaya za umeme ndani yake sawa na takribani kilomita 480 za cabling!

Miongoni mwa maajabu ya Airbus A380-800 ni kuwa ina zaidi ya maili 300 za nyaya za umeme ndani yake, huku ikihitaji galoni 950 za rangi ili kuupaka mwili wake wote. Pia sehemu yake ya mizigo ina uwezo wa kubeba hadi mabegi 3,000 kwa wakati mmoja.

Ndege hiyo ina uzito wa zaidi ya tani 560 inapokuwa imejaa kabisa na hutumia injini nne zenye nguvu kubwa zinazoiwezesha kusafiri zaidi ya kilomita 15,000 bila kusimama. Aidha, A380 inaweza kuruka kwa kasi ya karibu kilomita 1,020 kwa saa ikiwa angani.

Kutokana na ukubwa wake mkubwa, Airbus A380 ina mabawa yenye urefu wa zaidi ya mita 79, karibu sawa na upana wa uwanja mdogo wa mpira.

Wakati wa kupaa, mabawa yake yana uwezo wa kujikunja juu kwa kiwango kikubwa kutokana na nguvu inayotumika wakati wa kuruka.

Mashirika makubwa ya ndege duniani kama Emirates, Singapore Airlines na British Airways yameendelea kuitumia A380 kutokana na mvuto wake mkubwa kwa abiria. Baadhi ya ndege hizo zimeboreshwa kwa kuwekwa huduma za kifahari kama vyumba vya kulala, mabafu ya kuoga, baa maalum kwa abiria wa daraja la biashara, WiFi ya kasi pamoja na mfumo mkubwa wa burudani ndani ya ndege.

Airbus A380 Ina Vyumba vya Kuoga Angani

Kwa upande wa Emirates, baadhi ya ndege zake za A380 zimekuwa zikifananishwa na hoteli za kifahari zinazotembea angani kutokana na huduma za kiwango cha juu zinazotolewa kwa abiria wa daraja la kwanza na biashara.

Licha ya kupendwa sana na wasafiri kutokana na utulivu wake angani, nafasi kubwa ya kukaa pamoja na huduma za kifahari, gharama za kuiendesha zimeendelea kuwa changamoto kwa mashirika mengi ya ndege duniani. Hali hiyo ilisababisha kampuni ya Airbus kusitisha rasmi uzalishaji wa ndege hiyo mwaka 2021 baada ya kutengeneza ndege ya mwisho.

Hata hivyo, Airbus A380-800 bado imeendelea kuwa moja ya ndege zinazovutia zaidi duniani na imeacha historia kubwa katika sekta ya usafiri wa anga kutokana na ukubwa wake, teknolojia ya kisasa pamoja na muonekano wake wa kipekee.

Leave a Comment