The House of Favourite Newspapers

Christian Bella: Wanaosema Natumia Madawa Walete Ushahidi

MATUMIZI ya dawa za kulevya yamezidi kukithiri katika jamii yetu inayotuzunguka na taifa zima kwa jumla ambapo watu mbalimbali wamekuwa wakihusishwa na matumizi hayo ambayo yanaleta athari kubwa katika maendeleo ya nchi.

 

Wasanii mbalimbali wamekuwa wakiripotiwa juu ya kujihusisha na dawa hizo hivyo kufanya janga hilo kuongezeka kila kukicha licha ya kupigwa vita kali.

Christian Bella ambaye ni Mwanamuziki wa Dansi hapa nchini akiwa kiongozi wa Malaika Band, ni miongoni mwa wanamuziki ambao wamekuwa wakihusishwa na matumizi ya dawa hizo ambazo zinaathiri nguvu kazi ya taifa kwa kiasi kikubwa.

 

Bella ambaye ni mzaliwa wa DR Congo, aliwahi kuhusishwa na matumizi ya dawa za kulevya mwan zoni mwa mwaka huu na taarifa hizo zilianza kusambaa baada ya kushindwa kufanya shoo katika mkesha wa mwaka huu kwenye ukumbi mmoja uliopo Magomeni jijini Dar.

 

Championi Ijumaa, lilimtafuta Bella ili kuzungumzia tuhuma hizo za kutumia dawa za kulevya zinazomkabili ambapo anasema kuwa:

“Watu waendelee kunihusisha na matumizi ya madawa ya kulevya, hii ni kama mimba, wasubiri hadi nitakapoathirika na unga ndipo watapata majibu kama natumia ama la, kwa sasa siwezi kujibu ndiyo ama hapana.

 

“Nikisema hapana au ndiyo hakuna mtu atakayeweza kuniamini, hakuna mtu anayejua na hakuna anayeweza kukubali hilo, watu wanaoniambia natumia madawa ya kulevya watoe vithibitisho, hawajui maisha ninayoishi.

“Hakuna mtu anayejua aina ya maisha yangu ninayoishi, waendelee kuongea ni kawaida tu kama navuta ama sivuti Mungu ndiye anayejua, hivyo waache wazungumze mengi kuhusu mimi. “Ninachoangalia ni maisha yangu yanaendaje na wala simfuatilii mtu.

 

“Kuhusu ushauri, siwezi kumshauri mtu mzima kuweza kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya, kila mtu anafanya kitu kulingana na anavyojisikia jinsi maisha yake yanavyomshauri kufanya.

 

“Mimi siyo mshauri wa kuweza kumshauri mtu aache kutumia, kila mtu ana maamuzi yake, kila mtu anafanya vile anavyojisikia kwa maamuzi yake binafsi, hivyo kusema mtu fulani anavuta unga ama la ni kumuingilia mtu katika mambo yake binafsi jambo ambalo silipendi.”

 

Kumekuwa na ongezeko kubwa la wasanii wa Muziki wa Bongo Fleva ambao wamekuwa wakihusishwa kuhusika na matumizi ya dawa za kulevya.

Idadi ya wasanii hao ni kubwa sana ambapo kuna wale ambao wanajulikana kwamba wanatumia dawa hizo zikiwemo bangi, mirungi, heroin na cocaine, huku kuna kundi lingine ambalo limekuwa likitumia bila ya kutambulika.

 

Championi tunaziomba taasisi zinazohusika kuendelea kutoa elimu bila kuchoka juu ya adhari ya matumizi ya madawa haya kwani yamekuwa yakiathiri sana nguvu kazi ya taifa.

Comments are closed.