The House of Favourite Newspapers

Azam FC Mmekosea Wapi? Viongozi Chukueni Hatua Mapema

WAKATI michuano ya Ligi Kuu Bara m s i m u huu ikielekea ukingoni, nichukue nafasi hii kuipongeza timu ya Simba.

Naipongeza Simba kutokana na jinsi kikosi chake kinavyopambana ili kuhakikisha safari hii ubingwa wa ligi hiyo unakuwa halali yao baada ya kuukosa takribani misimu mitano iliyopita.

 

Kipindi chote hicho ilikuwa ikiishuhudia Yanga ikichukua ubingwa huo mara nne na Azam mara moja jambo ambalo lilikuwa likiwanyima raha wapenzi na mashabiki wa timu hiyo.

 

Hivi sasa Simba inapambana kuhakikisha inakuwa bingwa na dalili tayari zinaonekana kuwa itafanya hivyo.

Kinachotakiwa kwa Simba ni kuhakikisha inafanya vizuri tu katika mechi zake zilizosalia kwani Yanga pia bado ina nafasi ya kutwaa ubingwa huo lakini nafasi hiyo siyo kubwa sana kama ilivyo kwa Simba.

 

Ukiachana na hilo, nichukue nafasi hii kuizungumzia Azam FC ambayo wengi wetu tuliamini kuwa kutokana na uwekezaji wake mkubwa ingeleta mapinduzi makubwa katika mchezo wa soka hapa nchini.

Malengo na mikakati ya viongozi wa timu hiyo waliyokuwa nayo wakati ilipopanda daraja, hakika yalituvutia wengi na kuamini kuwa sasa tumepata timu itakayoondoa ufalme ya timu kongwe za Simba na Yanga katika michuano ya ligi kuu.

 

Katika msimu wake wa kwanza, Azam ilimaliza ligi nafasi ya tatu na ilitoa ushindani mkubwa kwa Simba na Yanga.

Lakini katika msimu wake wa nne wa ligi kuu ambao ulikuwa ni 2011/12, i l i f a n i k i w a k u a n d i k a rekodi baada ya kumaliza ligi hiyo ikiwa katika nafasi ya pili baada ya kujikusanyia pointi 56 nyuma ya Simba ambayo ndiyo iliyokuwa bingwa msimu huo ikiwa na pointi 62.

Hali hiyo iliifanya ipate tiketi ya kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika huku Simba ikishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuiacha Yanga ambayo ilimaliza katika nafasi ya tatu baada ya kujikusanyia pointi 49.

 

Msimu uliofuata wa 2012/13 ilimaliza pia katika nafasi ya pili, huku Yanga ikichukua ubingwa wa ligi hiyo, S i m b a y e n y e w e ilimaliza ikiwa katika nafasi ya tatu.

Hali hiyo i l i a n z a k u w a v u t i a wengi kwani i l i o n y e s h a wazi ni jinsi gani imedhamiria k u l e t a mapinduzi ya kweli katika soka la Tanzania na kuondoa ufalme wa Simba na Yanga.

 

Katika msimu wa 2013/14, Azam ilifanikiwa kuvunja ufalme huo baada ya kufanikiwa kuchukua ubingwa wa ligi kuu kwa mara ya kwanza huku pia ikiandika rekodi ya kumaliza ligi hiyo bila ya kupoteza mchezo.

Jambo hilo liliwavutia watu wengi na zaidi ni wale waliokuwa wamechoka kuziona Simba na Yanga ndiyo pekee zikitawala soka la Bongo kwa muda mrefu.

 

Hali hiyo pia iliivutia Benki ya NMB kuamua kuwekeza klabuni hapo ikiamini kuwa kutokana na malengo na mikakati ya timu hiyo pia itafaidika kwa kujitangaza ndani na nje ya nchi kwa sababu tayari ilikuwa imeonyesha mwanga baada ya kufanya vizuri mara tatu mfululizo.

 

Hata hivyo, sijui timu hiyo hivi karibuni imekumbwa na nini kwani imeonekana kuanza kupoteza mwelekeo.

Kwa sasa siyo tena timu ya ushindani kama ilivyokuwa hapo nyuma, kiwango chake ni cha kawaida kwani tangu msimu wa 2014/15 imekuwa ikiporomoka kila wakati na kuanza tena kuruhusu kurejea kwa ufalme wa Simba na Yanga.

 

Katika mchuano ya ligi kuu msimu huu matokeo ambayo imekuwa ikiyapata katika baadhi ya mechi zake hakika yamekuwa yakiwashangaza wengi ambao waliamini kuwa kutokana na uwekezaji wake hivi sasa ingekuwa inachuana vikali na Simba kuwania ubingwa wa ligi kuu.

MAKALA: Mohammed Hussein

Badala yake hivi sasa Simba inapambana na Yanga ambayo haikuwa vizuri kiuchumi msimu huu pia haikuwa na wachezaji wengi wa kutumainiwa ukilinganisha na Azam ambayo ipo vizuri kiuchumi kushinda timu zote kwa sasa zinazoshiriki ligi hiyo.

 

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Azam unatakiwa kujipanga na kuangalia ni wapi wanakosea ili kasi yao ile ya nyuma waliyoanza nayo katika michuano ya ligi kuu waweze kuirudisha.

Comments are closed.