Matola Apanga Kumtibulia Mfaransa Wa Simba SC
KOCHA Msaidizi wa Lipuli FC, Selemani Matola, amesema hatakubali kufanywa daraja la kuipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara wakati timu yake itakapokutana nao Jumamosi wiki hii.
Timu hizo zinatarajiwa kuvaana Jumamosi kwenye Uwanja wa Samora mkoani Iringa badala ya Ijumaa kama ilivyopangwa hapo awali.
Katika mchezo wa raundi ya kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Akizungumza na Championi Jumatano, Matola alisema katika mechi hiyo timu yake itaingia uwanjani ikiwa na morali baada ya matokeo ya ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya Singida.
Matola alisema, hataki kuona timu yake ikipoteza katika uwanja wa nyumbani, hivyo ameahidi kuifunga Simba ili kuvunja rekodi ya Simba ya kutofungwa kwenye ligi msimu huu.
“Nimemaliza mechi ya ligi dhidi ya Singida kwa ushindi wa bao 1-0 ambao kwangu nauona mkubwa, kama unavyoiona ligi msimu huu ilivyo ngumu.
“Matokeo haya ya Singida yatawafanya wachezaji wangu waingie uwanjani wakiwa na morali ya hali ya juu na kuongeza hali ya kujiamini na kupata matokeo mazuri.
“Nitaingia uwanjani nikijua Simba haijawahi kufungwa tangu ligi ya msimu huu imeanza, lakini hiyo hainifanyi niogope zaidi nitakiandaa kikosi changu kuhakikisha tunavunja rekodi yao,” alisema Matola.
Comments are closed.